PAMOJA na kuchekelea matokeo ya ushindi katika mechi mbili mfululizo, Tanzania Prisons inakabiliwa na kibarua kingine kigumu wikiendi hii itakapoialika Simba kwenye Uwanja wa Sokoine kwa mechi ya Ligi Kuu Bara.

Awali Prisons ilipanga kuutumia Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma baada ya Sokoine kufungiwa kutokana na kukosa sifa za kikanuni, lakini juzi jioni TFF ilitangaza kuufungulia na kutoa nafasi kwa maafande hao kuwapokea Mbeya katika mechi isiyotabirika.

Hata hivyo, licha ya ratiba ya michezo hiyo miwili, Maafande hao bado wana kiporo dhidi ya Yanga kabla ya kukamilisha michezo 15 ya mzunguko wa kwanza katika Ligi Kuu, huku ikiwa na matarajio ya kubaki salama.

Timu hiyo haijawa na matokeo mazuri, japokuwa kwa sasa imeonekana kurejea kwenye fomu baada ya kushinda mechi mbili dhidi ya Namungo 3-2 na kuilaza Biashara United 3-1 katika mechi ya hatua ya 64 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho.

Prisons inakutana na Simba huku rekodi zikiwabeba wageni, kwani katika michezo sita ya misimu mitatu mfululizo, Wekundu wa Msimbazi wameshinda mechi tano ikiwamo kipigo kizito cha mabao 7-1, Desemba 30, 2022, huku Prisons akishinda mmoja 2-1, Machi 6, 2024.

Ofisa Mtendaji wa Prisons, Godfrey Madegwa aliliambia Mwanspoti baada ya kufanya vizuri mechi mbili mfululizo, wameona ari na morali katika kikosi chao, hivyo matarajio yao ni kuendeleza ushindi ili kujinasua nafasi za chini.

Madegwa amesemaupande wa uongozi umeshakamilisha mipango katika kuongeza hamasa na wanafahamu ukubwa na ugumu wa Simba, akitoa matumaini lazima wapate pointi tatu.

“Upande wetu uongozi kila kitu kipo sawa, tumekuwa na utaratibu wetu wa kuweka bonasi pale tunaposhinda mchezo wowote na timu yoyote hata kwa Simba hakuna mabadiliko, tunaamini kwa maandalizi yetu tutabaki na pointi tatu,” amesemaMadegwa.

Kwa upande wake Straika wa timu hiyo, Oscar Mwajanga amesemawanaiheshimu Simba, lakini hawaiogopi na mkakati wao ni kuendelea kushinda ili kujinasua nafasi za chini baada ya kutokuwa na mwanzo mzuri.

“Makosa yaliyokuwapo benchi la ufundi liliyafanyia kazi, tunawaheshimu Simba ila tuko tayari kupambana nao kusaka ushindi, hatuko nafasi nzuri hivyo kwa sasa kila mchezo ni fainali kwetu,” amesemanyota huyo mwenye mabao mawili.

Prisons ipo nafasi ya 14 kwa pointi 12 baada ya mechi 13, huku Simba ikiwa nafasi saba kwa pointi 19 ikicheza mechi nane za Ligi Kuu na sasa wapinzani watakutana katika vita nzito ya pointi tatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *