
Miezi mitatu baada ya kuanza mpango mpya wa kubadilisha usajili wa vyombo vyote vya moto kwenda kwenye usajili wa namba mpya, zimekusanywa Sh1.7 bilioni katika kipindi hicho.
Makusanyo hayo yamefanyika kupitia Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) ambayo imepewa mamlaka hayo, na katika kipindi hicho jumla ya vyombo 19,337 tayari vimeshafanyiwa usajili wa namba mpya; kati ya hivyo, magari ni 13,060 na vyombo vingine 6,277.
Hayo yamebainishwa leo Februari 20, 2026, na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Hamad Omar Bakar wakati akijibu swali la mwakilishi wa Chambani, Mahmoud Shineni Ali (ACT Wazalendo), katika mkutano wa pili wa Baraza la 11 la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.
Katika swali lake la msingi, Mahmoud alihoji Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imepata wapi mamlaka ya kisheria ya kufanya uamuzi huo, kampuni iliyopewa zabuni, na tathmini ya idadi ya vyombo vilivosajiliwa pamoja na mapato yaliyokusanywa tangu kazi hiyo ianze.
Katika majibu yake, Naibu Waziri amesema ZRA inayo mamlaka ya kisheria kufanya hivyo; hii ni kutokana na kupewa uwakala wa kuisimamia Sheria ya Usafiri Nambari 7 ya mwaka 2003. Sheria hii ya usafiri wa barabarani imempa mamlaka Waziri anayeshughulikia miundombinu, mawasiliano, na usafiri kufanya mabadiliko kama haya.
Kampuni iliyopata zabuni ya kuzalisha vibati vya namba ni Budda Auto Parts, na mkataba wake ni kulingana na idadi ya vibati atakavyozalisha. Kwa seti moja ya vibati vya vyombo vya moto (magari) ni Sh32,510, kwa seti moja ya vibati vya vyombo (pikipiki) ni Sh26,680, na kwa seti moja ya vibati vya vespa na stika ya kibati cha namba ni Sh20,240.
Kuhusu serikali kulazimisha kubadilisha namba ilhali wananchi hawataki, amesema ni matakwa ya sheria na kuweka usalama, kwani serikali haibadilishi namba kwa matakwa yake isipokuwa kuna mambo mengi yanayochunguzwa, ikiwemo masuala ya usalama.
Wakati huohuo, Serikali imesema hakuna kodi inayotozwa kwa wawekezaji wazalendo (wazawa) katika sekta ya usafirishaji uwanja wa ndege na baharini.
Majibu hayo yalitokana na swali la mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayoub (CCM), aliyehoji kwanini wawekezaji wazalendo wanatozwa kodi zinazofanana (katika huduma moja) na mpango wa serikali wa kufanya mapitio ya kodi za namna hiyo na kuziondoa ili kupunguza mzigo wa wawekezaji wazalendo.
Jaku amesema, licha ya jitihada za kufungua milango ya vivutio kwa wawekezaji mbalimbali, wakiwemo wazalendo, kuna malalamiko ya wawekezaji wazawa katika sekta ya usafirishaji uwanja wa ndege na bandarini kutozwa kodi zinazofanana, kama vile ongezeko la asilimia mbili ya bei ya tiketi na Sh10,000 ya kodi ya uwanja.
Kadhalika, upande wa bandarini amesema kila tiketi kuna ongezeko la Sh5,000, wakati huo huo wawekezaji kutoka nje hawatozwi kodi hizo.
Akifafanua hoja hizo, Naibu Waziri wa Fedha amesema kwa upande wa usafiri wa baharini kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara hutozwa ada ya bandari ya Sh2,000, kodi ya miundombinu Sh2,000, na ada ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Sh1,000, hivyo kufanya jumla kuu iwe Sh5,000 inayotozwa kwa msafiri.
Kwa upande wa usafiri wa viwanja vya ndege kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara, hutozwa Sh10,000 ikiwa ni ada ya uwanja wa ndege.
“Kwa upande wa asilimia mbili ya mauzo ghafi ya tiketi, hutozwa ushuru wa stempu kwa wawekezaji wazalendo na wageni waliowekeza katika sekta ya usafirishaji,” amesema Naibu Waziri.
Kwa mujibu wa Dk. Hamad, Serikali hufanya mapitio ya kodi, tozo, na ada kila mwaka wa fedha ili kurahisisha ufanyaji wa biashara na uwekezaji nchini, kupunguza mzigo wa kodi kwa wananchi, pamoja na kuongeza ufanisi katika usimamizi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.