Mbeya. Watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya, wamefukuzwa kazi kwa tuhuma za utovu wa nidhamu, ikiwamo utoro wa muda mrefu kazini.
Uamuzi huo umetolewa leo na Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo, ukiongozwa na Mwenyekiti Gabriel Mwakagenda, baada ya kuwasilishwa mashauri manne ya kinidhamu, ambapo matatu yalipendekeza adhabu ya kufukuzwa kazi.
Imeelezwa kuwa shauri moja limerejeshwa katika ngazi husika kwa hatua nyingine za kiutumishi kwa mujibu wa kanuni na sheria za utumishi wa umma.
Mwakagenda amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya madiwani kupitia kwa kina taarifa za mashauri hayo na kujiridhisha na mapendekezo yaliyowasilishwa.
Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe wakiwa kwenye kikao cha robo ya pili kupitia taarifa mbalimbali.
“Baraza lilibaini makosa mbalimbali ya watumishi hao, yakiwamo utovu wa nidhamu na utoro wa muda mrefu kazini. Hata hivyo, shauri moja limerejeshwa kwa ajili ya kuendelea na taratibu za kiutumishi,” amesema.
Katika hatua nyingine, amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma, akisisitiza kuwa Serikali imewaamini kuwahudumia wananchi kwa uadilifu.
“Nitoe wito kwa watumishi wote kutambua dhamana waliyonayo na kuwahudumia wananchi kwa weledi na uaminifu,” amesema.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu, amepongeza jitihada za halmashauri hiyo kwa kushirikiana na wataalamu kuandaa rasimu ya bajeti inayozingatia maono ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025/2026.
Wakati huohuo, Baraza hilo limepitisha bajeti ya Sh69.3 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, hususan katika sekta za elimu na afya.