Dar es Salaam. Ikiwa wameadhimisha mwaka mmoja wa ndoa hivi karibuni, Jux ameendelea kutoa nyimbo ambazo kwa asilimia kubwa jumbe zake amezielekeza kwa mkewe Priscilla ambaye naye ameonyesha ushirikiano.
Tayari Jux ametoa nyimbo tano maalum kwa Priscilla huku bibie akitokea katika video zake zote. Je, nyimbo hizo ni zipi?, zinazungumzia nini hasa na zilitoka wakati gani?.
1. Ololufe Mi (2024) – Picha Linaanza
Katika video ya wimbo huu, Jux na Diamond Platnumz wamecheza kama watoto wa Mfalme mwenye nguvu kubwa kiutawala. Baba yao huyo amewachagulia wanawake wa kuoa ila tayari kila mmoja ana chaguo lake.
Jux amempenda Priscy kutokea Nigeria ambaye alijuana naye kupitia mitandaoni, huku Diamond akiangukia kwa mtumishi anayefanya kazi katika Ufalme wao kitu ambacho ni kinyume na matakwa ya baba yao.
Wanajadili ikiwa ni sawa kuacha urithi wa Ufalme ili kufuata kule walipopenda, Diamond anamshauri Jux kuusikiliza moyo wake ingawa yeye mwenyewe mwanzoni alipanga kuheshimu chaguo la mfalme.
Mwisho wa siku wote wanafuata nyoyo zao na sio matakwa ya baba yao, kufikia hapo mfalme anakuwa hana jinsi zaidi ya kubariki uamuzi wa watoto wake na hivyo ndoa mbili zinafungwa ambapo Jux anamuoa Priscilla.
2. Si Mimi (2025) – Uchumba
Jux alitoa wimbo huu muda mfupi baada ya kumchumbia Priscilla, humu anasema yote anayomfanyia mkewe si yeye ni akili yake, moyo wake, mawazo, na labda ni roho yake.
Video yake inaonyesha tukio la Jux kuvishwa pete Priscilla, tukio ambalo lilihudhuriwa na baadhi ya watu mashuhuri kutoka Tanzania pamoja na Nigeria.
Ikumbukwe uhusiano wao ulianza kuonekana hadharani hapo Julai 2024, ikiwa ni baada ya Jux kuachana na aliyekuwa mpenzi wake, Karen Bujulu ambaye walidumu kwa takribani mwaka mmoja.
3. God Design (2025) – Shukrani Kwa Mungu
Ni wimbo wa kwanza kuachiwa kutoka katika Extended Playlist (EP) yake Jux, A Day To Remember (2025) ambayo kwa sehemu kubwa imezungumzia maisha yake ya sasa pamoja na Priscilla.
Na moja ya picha walizopiga katika harusi yao huko Lagos, Nigeria ndio imetumika katika cover la EP hiyo yenye nyimbo saba zenye mahadhi ya Bongofleva na Afrobeats.
Sasa wimbo huu, God Design (2025) akimshirikisha Phyno kutokea Nigeria, Jux anaelekeza shukrani zake kwa Mungu kwa kumpatia mwanamke mrembo huku akitoa ahadi ya kumfanya kuwa wake wa milele.
Video yake yenye kusisimua chini ya Director Kenny imefanyika Lagos, Nigeria ikionyesha hadithi ya kweli ya mapenzi ya Jux na Priscilla kutoka kwenye harusi yao ya jadi iliyofanyika Aprili 17, 2025.
4. Thank You (2025) – Shukrani Ya Mtoto
Baada ya kutangaza wanatarajia mtoto wao kwanza, ndipo Jux alitoa wimbo huo ambao katika video yake Priscilla ameonekana akifurahia hatua ya kuelekea mama, hatua ambayo aliifikia salama.
Thank You ni wimbo uliotumia Jux kueleza hisia zake za kuwa baba kwa mara ya kwanza. Anamuombea mtoto wake baraka kwa Mungu, huku akimueleza kuwa anajivunia kuwa baba yake, na atampenda siku zote.
Ikumbukwe wawili hao walitangaza wanatarajia kupata mtoto hapo Julai 24, 2025 kupitia Instagram, na kufikia mwishoni mwa Agosti, wakatangaza kuwa wamejaliwa mtoto wa kiume na kumpa jina la Rakeem.
5. See Body (2026) – Uzuri Pia Unachangia
Katika wimbo huu Jux anamsifia mwanamke mrembo kwa jinsi alivyopendeza, na bila shaka huyu si mwingine bali mkewe Priscilla, binti wa mwigizaji maarufu wa Nollywood, Iyabo Ojo.
Jux anayejulikana kwa uwezo wake wa kuchanganya vionjo vya Kiafrika na muziki wa R&B, katika video ya wimbo huo ameonekana tena pamoja na mkewe ikiwa ni video ya sita kufanya pamoja.
Kutokana na melodi yake tamu na utayarishaji mzuri, ni wazi kuwa ‘See Body’ unaosherehekea urembo, mvuto na kujiamini, unaweza kuwa wimbo rahisi hata kwako kuupenda na kuusikiliza mara kwa mara.
Ikumbukwe Priscilla amesomea na kurithi kazi ya uigizaji kutoka kwa Mama yake mzazi, Ojo ambaye tangu mwaka 1998 yupo katika tasnia ya uigizaji akishiriki katika filamu zaidi ya 150 na kutoa zake binafsi 14.