Wabunge wa Marekani huenda wakapiga kura mapema wiki ijayo juu ya muswada unaolenga kumzuia Rais Donald Trump kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran bila idhini ya wazi ya Bunge la Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Reuters iliyochapishwa siku ya Ijumaa, wabunge wa chama cha upinzani Democratic pamoja na idadi ndogo ya wale wa chama tawala cha Republican wamekuwa wakijaribu mara kwa mara kupitisha maazimio ya mamlaka ya vita ambayo yangemzuia rais kuanzisha hatua za kijeshi dhidi ya serikali za kigeni bila ridhaa ya wabunge. Jitihada hizo hata hivyo zimekuwa zikikwama, huku washirika wa Trump ndani ya chama cha Republican wakisisitiza kuwa Bunge halipaswi kuweka mipaka kwa mamlaka ya rais katika masuala ya kijeshi.

Seneta wa Democratic Tim Kaine na Seneta wa Republican Rand Paul waliwasilisha azimio la Seneti mwishoni mwa mwezi uliopita likilenga kuzuia uhasama wa kijeshi dhidi ya Iran isipokuwa kama umetolewa idhini rasmi kupitia tamko la vita la Bunge.

Kaine alisema katika taarifa yake siku ya Ijumaa kwamba: “Ikiwa baadhi ya wenzangu wanaunga mkono vita, basi wanapaswa kuwa na ujasiri wa kupigia kura vita hivyo, na kuwajibika mbele ya wapiga kura wao, badala ya kujificha chini ya meza zao.” 

Msaidizi wa Kaine amesema kuwa bado hakuna ratiba rasmi ya lini Seneti itajadili azimio hilo. Hata hivyo, katika Baraza la Wawakilishi, Mbunge wa Republican Thomas Massie na Mbunge wa Democratic Ro Khanna wamesema wanapanga kulazimisha kura juu ya hatua kama hiyo wiki ijayo.

Khanna aliandika katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X kwamba: “Maafisa wa Trump wanasema kuna uwezekano wa asilimia 90 wa mashambulizi dhidi ya Iran. Hawezi kufanya hivyo bila idhini ya Bunge.” 

Kauli hizo zimekuja wakati zana za kijeshi za Marekani zikiendelea kuelekezwa karibu na Iran.

Maafisa wa Marekani walisema tarehe 12 Februari kwamba Wizara ya Vita ilikuwa inatuma manowari nyingine ya kubeba ndege za kivita, manoari za kufyatua makombora pamoja na maelfu ya wanajeshi na ndege za kivita karibu na Iran.

Trump alisema hivi karibuni, akiashiria manowari ya USS Gerald R. Ford kwamba: “Iwapo hatutafikia makubaliano, tutaihitaji.”

Vitisho hivyo vya kijeshi vya Marekani vinakuja sambamba na mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington huko Geneva. Oman, ambayo imekuwa mpatanishi katika mazungumzo hayo, imesema kuwa duru ya hivi karibuni ilikuwa chanya, hatua inayofungua njia kwa mazungumzo zaidi katika siku zijazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *