
Balozi wa Marekani katika utawala Israel amesema itakuwa “sawa tu” iwapo utawala wa Kizayuni wa Israel utapanua mipaka yake kote katika Asia Magharibi chini ya mpango wa “Israeli Kubwa.”
“Itakuwa sawa tu iwapo watachukua ardhi yote,” alisema Mike Huckabee katika mahojiano na mchambuzi wa kihafidhina Tucker Carlson yaliyorushwa hewani Ijumaa, alipoulizwa kuhusu nia ya Tel Aviv ya kupanuka kutoka Mto Nile hadi Mto Frati.
Huckabee, anayejulikana kama Mkristo Mzionisti mwenye msimamo mkali, alishinikizwa kueleza ni wapi hasa mipaka ya kijiografia ya utawala wa Israel ipo.
Akasema tena, “Ingekuwa vizuri wakichukua yote.”
‘Ardhi iliyoahidiwa’ ambayo Waisraeli wanalenga kuinyakua inajumuisha nchi zote zilizoko kati ya Mto Frati nchini Iraq na Mto Nile nchini Misri ambazo ni Lebanon, Syria, Jordan, Iraq, pamoja na sehemu za Saudi Arabia, Uturuki, na Misri za kisasa.
Carlson, aliyeshangazwa na jibu hilo, alimuuliza kama anaidhinisha mpango wa utawala wa Israel wa kunyakua maeneo yote ya Asia Magharibi.
Huckabee akajibu kwa kusema: “Hawataki kuyachukua. Hawajaomba kuyachukua. Lakini wakishambuliwa na nchi hizi zote, wakashinda vita hiyo na wakachukua maeneo hayo, jambo hilo litakuwa sawa.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwa muda mrefu amekuwa akitangaza wazi wazo la upanuzi wa mipaka ya kile kinachojulikana kama “Israel Kubwa”, akisema anafuata maono ya kihistoria na ya kiroho kuhusu kile ambazo Waisraeli wanadai ni ‘Ardhi Iliyoahidiwa.’
Katika mahojiano ya televisheni ya mwaka 2025, Netanyahu alisema anaamini katika maono hayo, akisisitiza kwamba ni “jukumu la kihistoria na la kiroho” kwake, akijumuisha maeneo yaliyokaliwa ya Palestina na sehemu za nchi jirani za Kiarabu.
Vilevile, mwaka 2023, Waziri wa Fedha wa Israel Bezalel Smotrich alizua hasira za kimataifa alipojitokeza katika hafla yenye ramani iliyojumuisha ardhi za Palestina pamoja na sehemu za Lebanon, Syria, na Jordan kama sehemu ya Israel.