
ALIYEKUWA kocha wa Yanga, Miloud Hamdi huenda akarejea tena kufundisha timu ya Ligi Kuu, huku ikidaiwa mabosi wa TRA United wanaangalia pia uwezekano wa kumpata, kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije.
Taarifa kutoka miongoni mwa watu wa karibu na kocha huyo, aliliambia Mwanaspoti, Hamdi aliyeachana na Ismaily ya Misri tangu Januari 26 anafanya nayo mazungumzo, licha ya makubaliano kati ya pande hizo mbili kutofikiwa.
“Hakuna makubaliano yaliyofikiwa hadi sasa juu ya suala hilo, kwa sababu wapo makocha wengi ambao wanaendelea kufanyiwa mchujo na kuangalia mwenendo wa timu kwa mechi tatu zijazo, hivyo, baada ya hapo ndipo tutajua,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua, mbali na Hamdi, ila mwingine aliyekuwa katika kinyang’anyiro hicho ni aliyekuwa pia Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Abdihamid Moallin ‘Master Lecturer’, aliyeondoka kikosini humo tangu, Julai 27, 2025.
Moallin mwenye uraia wa Somalia, kwa sasa yupo mapumziko Marekani tangu alipoachana na Yanga Julai 27, 2025, akiwa ni Mkurugenzi wa Ufundi na kabla ya hapo amewahi pia kuzifundisha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC na KMC.
Kwa upande wa Hamdi, aliitumikia Ismaily ya Misri kwa miezi sita tangu alipojiunga nayo Julai 3, 2025, akitokea Yanga na alishinda mechi nne tu kati ya 19, alizoiongoza katika mashindano yote, huku ikitoka sare miwili na kupoteza 13.
Katika mechi hizo 19, timu hiyo ilifunga idadi ya mabao 13, huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 26 na Hamdi, aliiongoza Yanga kwa msimu wa 2024-2025, kuchukua mataji mawili, ambayo ni Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la FA.
Kwa mara ya kwanza, Hamdi alitua nchini na kujiunga na Singida Black Stars akichukua nafasi ya Kocha Mbelgiji, Patrick Aussems aliyeondoka Novemba 29, 2024, ingawa Februari 4, 2025, alitua Yanga kurithi mikoba ya Mjerumani Sead Ramovic.
Hamdi mwenye miaka 54, akiwa na leseni ya Ukocha ya UEFA Pro, amezifundisha pia Al-Khaldiya SC ya Bahrain, JS Kabylie, CS Constantine na USM Alger zote za Algeria, Al Salmiya (Kuwait), Al Ettifaq (Saudia Arabia) na RS Berkane ya Morocco.