
Wawakilishi wa Russia na China katika mashirika ya kimataifa yenye makao yake mjini Vienna Austria wamesisitiza suluhisho la kidiplomasia kwa suala la nyuklia la Iran.
Kulingana na Shirika la Habari la Mehr, likinukuu gazeti la Izvestia, Mikhail Ulyanov, mwakilishi wa kudumu wa Russia katika mashirika ya kimataifa huko Vienna, amesema: “Wawakilishi wa nchi hizo tatu, Russia, China, na Iran, wamesisitiza katika mkutano wao na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, juu ya udharura wa kutatuliwa kwa njia ya kidiplomasia suala la miradi ya nyuklia la Iran.”
Maafisa hao wa China na Russia wameeleza kwamba, njia bora ya kuipatia ufumbuzi kadhia ya nyuklia ya Iran ni mchakato wa kidiplomasia.
Hivi majuzi pia Sergei Lavrov Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia kwa mara nyingine aliionya Marekani kuhusu matokeo mabaya ya chokochoko yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran. Lavrov alisema kwamba chaguo la kijeshi dhidi ya Iran halidhamini usalama wa nchi yoyote.
Katika wiki za hivi karibuni, hasa kutokana na ongezeko la kupelekwa wanajeshi wa Marekani katika sehemu mbalimbali za Asia Magharibi, Moscow imetoa maonyo makali ya kidiplomasia kwa Washington kuhusu matokeo mabaya ya hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran.
Hadi sasa kumefanyika duru mbili za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja baina ya Marekani na Iran na pande zote mbili zimetoa kauli zinaoonyesha kwamba, kwa namna fulani kumekuwa na hatua nzuri zilizopigwa katika mazungumzo hayo.