Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amewaelekeza watendaji wa kata jijini Mbeya kuwachukulia hatua wazazi wanaokwamisha usajili wa watoto waliokidhi vigezo vya kwenda shule.
Pia, amewataka wakuu wa shule na walimu kwa ujumla kutowatoza fedha zozote wazazi, akibainisha kuwa Serikali imejipambanua kugharamia elimu bure, vinginevyo meza ya mkuu wa wilaya ndiyo ina mamlaka ya kufanya hivyo.
Akizungumza jijini Mbeya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa wakati wa mahafali ya 19 ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Ivumwe, Itunda amesema wazazi wanaoamua makusudi kukwamisha shughuli hiyo wasifumbiwe macho.
“Kwa sasa tupo zaidi ya asilimia 86 ya usajili wa watoto ngazi ya awali, msingi na kidato cha kwanza, ikiwa imebaki mwezi mmoja kumaliza shughuli hii, kila mzazi mwenye mtoto aliyekidhi vigezo apelekwe shule.
“Nawaelekeza watendaji wa kata zote Wilaya ya Mbeya kwenye maeneo yao, hakuna mtoto aliyekidhi kwenda shule kuwa mtaani, mzazi yeyote anayekwamisha shughuli hii achukuliwe hatua za kisheria, lakini mzazi anapaswa kuchangia chakula na hili halina mjadala,” amesema.
Ameongeza kuwa: “Hakuna mwalimu au mkuu wa shule anayeruhusiwa kuwatoza michango holela wazazi kwani Serikali imejipambanua kugharamia elimu bila malipo na ikitokea ni meza ya Mkuu wa Wilaya pekee na si vinginevyo, kwani kuna baadhi ya walimu wanatengeneza mazingira ya kupata pesa.”
Mkuu huyo amewaasa wanafunzi hao kuendelea kujilinda kuhakikisha wanatimiza malengo na ndoto zao, huku akiwapongeza kwa taaluma nzuri waliyoonyesha kwa wakati wote hadi kufika kidato cha sita, akieleza kuwa anatarajia ufaulu mzuri kutokana na msingi walioandaliwa.
“Mtakapomaliza mitihani yenu inayotarajia kuanza Mei 4, mkifika huko mtaani msikubali kutolewa kwenye reli, wapo watu wa makundi mawili, wazuri na wabaya, shirikianeni na wenye nia njema ili kuweza kufikia malengo na ndoto zenu, matarajio yangu ni kuona mnafaulu kwa kiwango cha juu,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda (kushoto) akiangalia na kuwasikiliza wanafunzi, Emirio Samuel na Estha Steven wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Ivumwe wakifanya majaribio mbali mbali ya kisayansi kwa kutumia vifaa vya kisasa baada ya Shule hiyo kuongeza tahasusi za kisayansi.
Akitoa taarifa ya shule, mkuu wa shule hiyo, Oscar Mwaihabi amesema Ivumwe imekuwa na ufaulu wa kupanda kila mwaka na kwa sasa wamefuta daraja sifuri kwa miaka mitatu mfululizo kwa madarasa ya mitihani ikiwa ni kidato cha pili, cha nne na cha sita.
Amesema shule hiyo imekuwa na mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia hali inayoongeza chachu kwa wanafunzi kupenda masomo na kuongeza ufaulu akieleza kuwa uongozi umejipanga kuendeleza taaluma bora.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa shule hiyo, Peter Mbilinyi amesema wanafunzi walianza wakiwa 169, lakini wanaotarajia kuhitimu ni 174 ikiwa ni ongezeko kubwa kutokana na elimu bora na maadili na mafunzo mengine shuleni hapo.
“Tumefanya mitihani mingi ya kujiandaa kwa ndani na nje na ufaulu umepanda, tumepata ongezeko la tahasusi kwa masomo ya sayansi ikiwa ni sehemu ya kuongeza ufanisi kwa wanafunzi,” amesema Mbilinyi.