
MWANARIADHA nyota wa kimataifa wa riadha wa Tanzania, Gabriel Geay amefanya kweli katika Mbio za Daegu Marathon 2026 kwa kutetea ubingwa wa mbio hizo kwa mara ya pili mfululizo zilizofanyika asubuhi ya leo Korea Kusini.
Geay alimaliza akiwa nafasi ya kwanza akiwa sambamba na Muethiopia Chimdesa Gudeta kila mmoja akitumia muda wa saa 2:08:08, huku Mtanzania mwingine Emmaneul Dinday akimaliza wa tatu kwa muda wa 2:08:16.
Ushindi huo umemfanya Geay kuvuna Dola 200,000 (zaidi ya Sh514 milioni) na medali ya dhahabu, huku Dinday akipata Dola 45,000 (Sh115 milioni) na medali ya shaba, wakati mshindi wa pili akizoa Dola 80,000 na medali ya fedha.
Hii ni mara ya pili kwa Geay kufanya kweli katika mbio hizo za Daegu kwani mwaka uliopita aliandika rekodi kwa kutumia muda wa saa 2:05:22 na kuzoa medali ya dhahabu pamoja na kitita cha fedha mbele ya Addidu Gobena pia wa Ethiopia.
Katika mbio hizo za leo Jumapili, Geay na Chimdesa walikuwa wakichuana ng’adu kwa ng’adu tangu mwanzo na haikushangaza kumaliza ndani ya muda sawa, japo Mtanzania huyo alikuwa wa kwanza kugusa mstari kuliko mwenzake na kunyakua medali ya dhahabu na mpinzani wake kunyakua medati ya fedha.
Geay pia ndiye Mtanzania anayeshika rekodi ya kukimbia mbio ndefu kwa muda mfupi zaidi aliyoiweka mwaka 2023 katika mbio za Boston Marathon akikimbia kwa saa 2:03:00 na kwa mwaka huu amemaliza kwa saa 2:08:04.
Mtanzania mwingine ambaye ni mdogo wa Geay, anayeitwa Bernado Geay alimaliza nafasi ya 13 katika mbio za Daegu Marathon zilizokuwa na kilimoita 42 zikishirikisha wanariadha mbali mbali na kwa upande wa wanawake, Mkenya Lilian Kasait akinyakua ushindi wa kwanza kwa muda wa 2:19:33, huku Meseret Belete wa Ethiopia akishika nafasi ya pili kwa muda wa 2:19:52 na Mkenya Evaline Chirchir akishika nafasi ya tatu kwa kutumia muda wa 2:20:42.