Shinyanga. Sakata la kusuasua kwa ujenzi wa barabara ya Mwawaza na stendi kuu ya mabasi mkoani Shinyanga limechukua sura mpya baada ya Mbunge wa Shinyanga Mjini na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, kumtaka mkandarasi ajiandae ‘kumkabili’, kutokana na kile alichokiita uzembe unaowaumiza wananchi.
Kauli hiyo imekuja kufuatia mkandarasi kushindwa kutekeleza maagizo yaliyotolewa Januari 9, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, baada ya mradi huo kuchelewa kwa muda mrefu. Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, aliagiza mkandarasi na mshauri wa mradi huo kuwekwa ndani kwa madai ya kupuuza maelekezo ya Serikali.
Akizungumza leo Februari 22, 2026 katika mkutano wa hadhara wa Manispaa ya Shinyanga, Katambi amesema mradi huo ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi 14 tangu kusainiwa kwa mkataba, lakini umesimama bila sababu za msingi. “Kesho nitaenda eneo la tukio, mkandarasi ajiandae,” amesema, akisisitiza kuwa hatavumilia miradi ya maendeleo kukwamishwa.
Amesema atasimamia haki na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa manufaa ya wananchi. Aidha, ametangaza kuanza kwa ujenzi wa chuo kikuu mkoani Shinyanga kitakachochukua wanafunzi kati ya 1,500 hadi 3,300 kwa gharama ya Sh11 bilioni, ambapo Sh8 bilioni tayari zimetolewa.
Wananchi wakiwa katika mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Patrobas Katambi, uliofanyika viwanja vya Zimamoto mkoani Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, ameiomba Serikali kurudisha uratibu wa utoaji wa vitambulisho vya Taifa (Nida) ngazi ya kata ili kupunguza foleni wilayani. Naye Mtatiro ameahidi kuwahudumia wananchi saa 24 na kupokea malalamiko yao moja kwa moja.
Wananchi wameeleza kuwa kusuasua kwa ujenzi wa barabara ya Mwawaza kumesababisha kero kubwa hasa wakati wa mvua. Jerald Mshandete amesema hali ya barabara imekuwa changamoto wakati wa kuwapeleka wagonjwa hospitalini, akitaka mradi huo ukamilike haraka.