
LICHA ya mwenendo mbaya wa African Sports ‘Wanakimanumanu’ msimu huu katika Ligi ya Championship, ila kocha wa kikosi hicho, Khalid Adam, amesema ataendelea kuipigania timu hiyo hadi mwishoni, ili ibakie Ligi ya Championship msimu ujao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Khalid, amesema hadi sasa kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kiuchezaji tofauti na mwanzoni, ingawa matokeo wanayopata hayaendani na kiwango cha timu inachokionyesha, jambo analoendelea kupambana nalo kwa haraka.
“Malengo yangu ni kuinusuru timu na janga la kushuka daraja kwa sababu kutoka Championship hadi Ligi Daraja la Kwanza ni kitu ambacho nisingependa kitokee, bado tuna nafasi kutokana na kutopishana pointi nyingi na wenzetu pia,” amesema Adam.
Kocha huyo aliyewahi kuzifundisha Mwadui na Fountain Gate, amesema aliingia katika timu hiyo kwenye kipindi kigumu cha kuitengeneza ili iendane na ushindani wa Championship, japo alikutana na wachezaji wengi vijana wanaohitaji muda zaidi.
Khalid aliyechukua nafasi ya Sharifu Joseph Ndokezi, ana kibarua cha kuinusuru timu hiyo, kwa sababu kabla ya mechi ya jana dhidi ya Kagera Sugar, ilikuwa imeshinda mitatu, sare miwili na kupoteza 13, kati ya 18, ikiwa nafasi ya 15 na pointi 11.