Barcelona, Hispania. Mgombea wa urais wa Barcelona, Victor Font, amezungumza kuhusu dhamira yake ya kumrudisha lejendi wa klabu hiyo, Lionel Messi astaafu soka akiwa katika viunga hivyo na apate heshima ya kuagwa inavyostahili.

Gwiji huyo wa Argentina aliondoka Camp Nou mwaka 2021 katika mazingira ya kusikitisha, baada ya vigogo hao wa Catalonia kushindwa kufikia naye makubaliano ya mkataba mpya kutokana na matatizo ya kifedha. Messi alitimkia Paris Saint-Germain ambako alicheza kwa misimu miwili kabla ya kwenda Inter Miami ya Marekani anakocheza hadi sasa.

Nyota wa Argentina, Lionel Messi wakati alipokuwa anakipiga Barcelona. Picha na Mtandao

Messi ambaye ni mmoja kati ya wachezaji bora wa muda wote duniani, alivunja rekodi nyingi za ufungaji mabao na kushinda mataji lukuki akiwa na Barca.

Hata hivyo, licha ya kuonekana kama angestaafia Barcelona, matatizo ya kifedha yalimlazimu mshindi huyo wa Kombe la Dunia kuondoka kama mchezaji huru mwaka 2021.

Tangu aondoke, Messi amekuwa akihusishwa mara kwa mara kurejea tena Barcelona. Font, ambaye ni mgombea wa urais katika uchaguzi ujao wa klabu hiyo, amesisitiza kuwa anaweza kumrudisha Messi mwenye umri wa miaka 38 ili kuhakikisha anaagwa kwa heshima inayolingana na hadhi yake kama mchezaji bora zaidi kuwahi kuichezea Barca.

Nyota wa Argentina, Lionel Messi wakati alipokuwa akicheza PSG baada ya kuondoka Barcelona msimu wa 2021/2022. Picha na Mtandao

Akizungumza  na AS, Font amesema: “Ni ukweli usiopingika kwamba Messi hawezi kurudi katika timu hii iwapo Joan Laporta ataendela kuwa madarakani, ila mimi nikishinda uchaguzi, uwezekano wa Messi kurudi ni mkubwa. Messi ni mfano wa kuigwa si tu kama mchezaji wa soka bali pia kama binadamu.

Tusisahau kwamba Messi alijaribu kutaka kurudi mwaka 2023, wakati timu ipo chini ya Xavi Hernandez, lakini dili likafeli. Messi hawezi kumaliza safari yake na Barca kwa kuaga kwenye chumba kilichofungwa. Haiwezekani, ni lazima astaafu akiwa uwanjani. Mbali ya kumuaga pia tunaweza kumpendekeza kuwa, Rais wa Heshima wa Klabu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *