
Novemba 5, 2008, Viwanja vya Grant Park, Chicago, Illinois, Marekani, ilikuwa siku yenye msisimko mkubwa. Umati mkubwa ulikusanyika viwanjani hapo. Inakadiriwa watu zaidi ya 240,000 walihudhuria. Wamarekani zaidi ya 71 milioni, waliganda kwenye televisheni.
Historia ilikuwa imeandikwa. Rais wa kwanza mwenye asili ya Afrika (Mmarekani mweusi), alikuwa amechaguliwa. Wamarekani na walimwengu walitaka kumsikia mtu huyo aliyeandika rekodi ya aina yake, angezungumza nini? Jumuiya ya Wamarekani weusi ilikuwa na furaha isiyomithilika.
“Haloo Chicago,” alianza kwa salamu. “Kama yupo mtu yeyote, ambaye bado ana shaka kuwa Marekani ni sehemu ambayo yote yanawezekana. Ambaye bado haamini kama ndoto ya waasisi wetu bado ipo hai katika nyakati zetu. Ambaye bado anahoji nguvu ya demokrasia yetu. Leo ni jibu lako.”
Shangwe la hadhira lilikuwa juu sentensi kwa sentensi, wakati mwingine neno kwa neno. Barack Hussein Obama, mtoto wa Mjaluo wa Kenya, Baraka Hussein Obama Sr (baba), na Stanley Ann Dunham (mama) wa Wichita, Arkansas, alikuwa anatoa hotuba yake ya ushindi wa kiti cha urais dhidi ya John McCain, katika uchaguzi uliofanyika Jumanne, Novemba 4, 2008.
Hotuba ya Obama ilipofika dakika ya nne na sekunde saba, kwa waliokuwa wakitazama moja kwa moja kupitia televisheni, kamera zilimleta kwenye picha, Baba Mchungaji, Jesse Louis Jackson. Alikuwa akipiga makofi, kuonesha kukoshwa na hotuba. Takriban mara tatu, kamera zilimwonesha Jesse Jackson.
Hotuba ilipokamilika, Obama akawa anazunguka kusalimia kwa kuipungia mkono kaumu iliyohudhuria. Mara, Joe Biden, aliyekuwa mgombea mwenza na Makamu wa Rais mteule, alitokeza, akakumbatiana na Obama. Wakaungana kuusabahi umma. Kisha, akafuata mke wa Obama, Michelle, na mke wa Biden, Jill.
Ni kipindi ambacho kamera zilimwonesha Jesse Jackson, akitokwa machozi. Yalikuwa machozi yenye mguso wa raha ya kutua mzigo mzito. Naam, hatimaye furaha. Yes, happy at last! Machozi ya Jesse Jackson yalimaanisha kutimia kwa ndoto iliyosubiriwa kwa muda mrefu iwe kweli.
Kutoka Novemba 5, 2008, mpaka Februari 17, 2026, ikiwa imepita miaka 17, miezi mitatu na siku 12, Jesse Jackson, amelala usingizi wa dawamu.
Hii maana yake, aliishi mihula yote miwili ya Rais kwanza mweusi Marekani. Akaushuhudia muhula wa mweusi mwingine, Kamala Harris, akiweka rekodi kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais.
Agosti 28, 1963, shujaa wa wakati wote wa mapambano ya haki za raia Marekani, Mchungaji Martin Luther King Jr, alitoa hotuba maarufu ambayo ilibeba matumaini kwa watu weusi. “I Have A Dream” – “Nina Ndoto”, ndiyo jina la hotuba. Hotuba hiyo, King aliitoa Lincoln Memorial, Washington, D.C.
Ni hotuba ya wakati wa kilele cha maandamano kwa ajili ya ajira na uhuru. Maandamano hayo yalifanyika kuadhimisha miaka 100, tangu Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, alipotoa tamko la kuharamisha biashara ya utumwa, na kumtambua mtu mweusi kuwa ni binadamu, siyo bidhaa (Emancipation Proclamation).
King alisema: “Nina ndoto kwamba siku moja juu ya milima myekundu ya Georgia, watoto wa mtumwa wa zamani na watoto wa mmiliki wa zamani wa watumwa, wataweza kuketi pamoja kwenye meza ya undugu.”
Ilikuwa ndoto kuwa ingefika siku, maisha ya ubaguzi, na kutenganishwa huduma baina ya weupe na weusi, yangefika mwisho, na jamii zote kuishi kama ndugu.
Aprili 4, 1968, akiwa kwenye Hoteli ya Lorraine, Memphis, Tennessee, King alipokea pigo la risasi iliyoingia shavuni, ikashuka kwenye taya, ikakita begani. King alifariki dunia akifanyiwa upasuaji, Hospitali ya Mtakatifu Joseph, Memphis. Aliondoka ndoto yake haijatimia.
Hata hivyo, aliwaacha washirika wake kwenye mapambano. James Bevel, Vincent Harding, Stokely Carmichael, Ralph Abernathy, na Coretta Scott King (mke wa King), waliendeleza harakati za kuipigania ndoto. Pamoja nao, ni mwanafunzi wa King, Jesse Jackson.
Carmichael, Abernathy na Coretta, hawakushuhudia ndoto ikitimia. Walifariki dunia Obama hajawa Rais. Bevel alifariki dunia mwezi mmoja baada ya ndoto kutimia. Harding, aliishi kuiona ndoto ya King, lakini alifariki dunia mwaka 2014, kipindi Obama akiwa nusu ya muhula wake wa pili. Jesse Jackson, aliona utimilifu wa ndoto, na sasa naye amekwenda kupumzika.
Jesse Jackson ameondoka bila deni. Makutano ya maisha baada ya kifo yakijiri, Jesse atamwambia King kuwa Marekani ya sasa, haiishii kwenye ndoto ya kuona watoto wa watumwa na watoto wa wamiliki wa watumwa wanaketi meza moja, bali imewezekana Marekani kuongozwa na mtu mweusi.
Ndoto ilitimia, mtoto wa mmiliki wa zamani wa watumwa (Biden), kumteua mtoto wa mtumwa wa zamani (Kamala), kuwa mgombea mwenza wake. Walishinda kiti na kwenda kufanya kazi pamoja ya kuongoza nchi. Kisha, Kamala, akabeba bendera ya Democrats kuwania urais mwaka 2024.
Usingeyaelewa machozi ya Jesse Jackson, kama hukufahamu walipitia yapi. Maandamano kwa maandamano, migomo na migomo. Jesse aliyatoa sadaka maisha yake kupigania haki ya mtu mweusi. Wakati King alijikita kuhubiri usawa, Jesse alijielekeza moja kwa moja kutetea na kupambania hadhi ya mtu mweusi.
Zama za ubaguzi mkubwa. Kutoka watu weusi kunyimwa au kupunjwa huduma, mpaka kupata sawa na weupe lakini bila kuingiliana. Sheria ya Separate But Equal (tenganisha lakini kwa usawa). Sheria zilizosababisha weusi wajenge shule, vyuo mpaka hospitali zao.
Zilikuwa zama ambazo Wazungu waliona kinyaa kuchanganyika na Wamarekani wenye asili ya Afrika. Jesse Jackson alipambana na hali hiyo kwa sauti na kisheria.
Alianzisha kampeni ya Push-Excel, kuunganisha Operesheni Push na Muunganiko wa Kitaifa. Zote zilikuwa operesheni za kumwamsha mtu mweusi kujitambua na kuweka msukumo wa kudai haki na hadhi zao.
Push ilisimama badala ya maneno, People United to Save Humanity, yaani umoja wa watu kwa ajili ya kuokoa ubinadamu. Jesse alikuwa mtu mwenye nguvu kubwa ya ushawishi, na sauti yake ilivutia kusikiliza. Hiyo ndiyo sababu King alichagua kumweka karibu yake.
“Mimi ni mweusi, mzuri, najivunia, lazima niheshimiwe, lazima nilindwe, mimi ni mtu,” Jesse alirejea shairi hili mara kwa mara, na kuukaririsha umma wa Wamarekani Weusi, kujivunia walivyo, na kamwe wasijione wao ni watu daraja la pili.
Safari ilianzia Greenville
Oktoba 8, 1941, kwenye Jiji la Greenville, South Carolina, ndiyo Jesse alizaliwa. Mama yake, Helen Burns, alipokuwa na umri wa miaka 18, akiwa ni mwanafunzi wa high school, alipewa ujauzito na jirani yao, Noah Louis Robinson, 33. Robinson alikuwa bondia, na alikuwa na jina kwenye jumuiya ya Wamarekani Weusi.
Jesse, alipokuwa na umri wa mwaka mmoja, mama yake aliolewa na Charles Henry Jackson, ambaye alimwasili. Ni kuanzia hapo Jesse alianza kutumia ubini wa Jackson. Kipindi cha ukuaji, Jesse alitaniwa sana na wenzake kwa sababu alizaliwa nje ya ndoa. Alisema, utani huo ndiyo ulimpa hamasa ya kuongeza juhudi ili kufanikiwa.
Alisoma shule ya utenganisho wa weupe na weusi, Sterling High School, iliyopo Greenville. Alitoka wa 10 darasani kwenye mitihani yake ya high school. Jesse, pia alikuwa mwanamichezo. Alipokea mwaliko wa kucheza baseball, kikapu na American football. Michezo yote hiyo alifanya vizuri.
Mwaka 1959, alijiunga na Chuo Kikuu cha Illinois, alikopewa ufadhili wa masomo kupitia mchezo wa American Football. Alisoma muhula mmoja tu. Hakuridhishwa na chuo hicho kwa sababu kilitawaliwa na wazungu. Jesse, alihamia Chuo Kikuu cha North Carolina A&T, ambacho ni cha Wamarekani weusi.
Mwaka 1964, Jesse alihitimu shahada ya kwanza ya Sosholojia, kisha akajiunga na Seminari ya Thiolojia Chicago. Mwaka 1966, aliacha chuo ili ajikite kwenye harakati, akiwa amebakiza madarasa matatu atunukiwe shahada ya uzamili.
Mwaka 2000 Seminari ya Thiolojia Chicago, walimtunuku shahada ya uzamili kwa kuunganisha rekodi zake alipokuwa anasoma, na uzoefu wake wa kikazi.
Mwaka 1965, Jesse alishiriki matembezi ya mshikamano ya Selma hadi Montgomery, yaliyochukua siku 19. Matembezi hayo yaliongozwa na King, ambaye alivutiwa haraka na Jesse.
Bila kusubiri, King baada ya kushauriana na Bevel, alimteua Jesse kuwa kiongozi wa taasisi yao ya Southern Christian Leadership Conference (SCLC), tawi la Chicago.
Mwaka 1967, King alimteua Jesse kuwa mkurugenzi kitaifa wa taasisi ya kibiashara ya SCLC, iliyokuwa inaitwa Operation Breadbasket.
King alipofariki dunia, umma wa Wamarekani weusi ulimtazama Jesse kama mrithi wake. Hali hiyo ilisababisha mgogoro mkubwa ndani ya SCLC, hasa baina ya Jesse na washirika wa King, aliowakuta kwenye taasisi hiyo. Jesse, alilazimika kuachia ngazi na kuanzisha taasisi zake.
Mwaka 1984 na 1988, Jesse alijitokeza kusaka tiketi ya kuwa mgombea urais kupitia chama cha Democratic bila mafanikio. Pamoja na hivyo, nguvu yake kimataifa na kidiplomasia ilidhihirika mwaka 1983, alipokwenda Syria kujadiliana na Rais Hafez al-Assad, ili kumwachia rubani wa ndege za kijeshi wa Marekani, Luteni Robert Goodman, aliyekuwa anashikiliwa mateka.
Wengi walidhani Jesse asingefanikiwa, kinyume chake Rais aliyekuwa madarakani Ronald Reagan, aliwaita Jesse na Goodman, Ikulu, White House, kuwapokea rasmi baada ya kurejea Marekani. Alimpongeza Jesse kwa kuokoa maisha ya rubani huyo.
Juni 1984, Jesse alifanya mazungumzo na aliyekuwa Rais wa Cuba, Fidel Castro, yaliyofanikisha kuachiwa huru mateka 22 wa Marekani waliokuwa wakishikiliwa nchini humo. Mwaka 1991, Jesse alifika Iraq na kumshawishi aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Saddam Hussen, awaachie raia wa kimataifa, aliokuwa anawashikilia.
Desemba 31, 1962, Jesse alifunga ndoa na Jacqueline Lavinia Brown, na katika ndoa yao walifanikiwa kupata watoto watano, ambao ni Jesse Jackson Jr, Jonathan Jackson, Yusef DuBois Jackson, Santita Jackson na Jacqueline “Jackie” Lavinia Jackson. Jesse ana mtoto mwingine nje ya ndoa ambaye anaitwa Ashley Jackson.
Kifo cha Jesse Jackson, hakipaswi kuchukua tafsiri kuwa “duniani tunapita”, bali ni hadithi ya maisha yenye kusudi, yanavyofika tamati. Wamarekani Weusi hasa kizazi kipya, wanaweza kuona maisha rahisi kwao, ni kwa sababu Jesse na wengine, walitoa maisha yao sadaka kupigania haki na hadhi ya watu weusi. Jesse, ameondoka duniani akiwa na umri wa miaka 84, miezi minne, na siku tisa. Usiku mwema shujaa wa wakati wote, Jesse Jackson.