Bwana Yesu asifiwe. Nakusalimu katika jina la Yesu. Naamini Mungu amekulinda na kukuvusha wiki nzima hadi kufika Jumapili hii tulivu mbele zake yatupaswa kumshukuru. Ninaitwa Mwalimu Erasto Maliganya

Wapo wanaosoma ujumbe huu wakiwa nchini Tanzania lakini katika mazingira magumu huenda ni gerezani au kwingine kokote lakini neno la Mungu ni taa na kumbuka siku zote penye taa hutakosa kuona njia.

Mungu wetu ni mwema wakati wote mshukuru Mungu pekee aliyethibitika, usilione tatizo lililopo mbele yako bali mtazame yeye aliye juu ya vyote kwa maana ndiye Muumba wetu na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Zingatia neno ‘vyote’ hakuna kilichobainishwa labda kile au hiki hakuhusika bali ni vyote.

Siku ya leo tumepewa somo linalosema “Kwa neno lako nitazishusha nyavu”.

Bila haka neno hili linatuelekeza mimi na mimi kusikia sauti na maagizo ya Mungu katika mazingira uliyopo haijalishi ni magumu kwa kiasi gani pamoja na kutenda kwa imani huku tukiliamini neno la Mungu.

Katika maisha kuna nyakati unapita kwenye kipindi ambacho kila unachofanya kinaonekana hakizai matunda. Unafanya kazi, unajitahidi, unatumia nguvu na rasilimali zako, lakini matokeo hayaonekani. Unaanza kujiuliza, “Je, nafanya kazi bure?”

Leo natamani tuutazame mfano wa Biblia unaotufundisha nini cha kufanya katika hali kama hiyo.

Andiko kuu: Injili ya Luka 5:1–11.

Yesu alikuwa akifundisha kando ya ziwa la Galilaya. Baada ya kumaliza, alimwambia Simoni Petro aingize mashua majini na kushusha nyavu. Petro, akiwa mvuvi mzoefu, akasema:

 “Bwana, tumejitahidi usiku kucha wala hatukupata kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.”

Walikuwa wamefanya kazi usiku kucha bila mafanikio. Uchovu ulikuwepo, kukata tamaa kulikuwepo, na walikuwa tayari kuosha nyavu zao. Lakini kwa sababu ya neno la Yesu, Petro aliamua kujaribu tena.

Alipotii, walipata samaki wengi kiasi cha nyavu kutaka kukatika. Mashua zikajaa hata zikaanza kuzama. Petro akaanguka miguuni pa Yesu akisema, “Ondoka kwangu, Bwana, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi.” Yesu akamwambia, “Usiogope; tangu sasa utakuwa ukivua watu.” Petro akaacha vyote akamfuata.

Hawa walikuwa wavuvi wenye uzoefu. Tatizo halikuwa vifaa wala maarifa. Tatizo lilikuwa hawakuwa bado wamepokea neno la Mungu juu ya kazi yao siku ile.

Kuna wakati huhitaji kubadili kazi, biashara au huduma; unachohitaji ni kusikia sauti ya Mungu katika kile unachofanya.

Tunajifunza nini kutoka kwa Petro?

1. Sikiliza sauti ya Mungu

Petro aliweka neno la Yesu juu ya uzoefu wake. Mafanikio huanza pale tunapoweka Neno la Mungu juu ya maarifa yetu binafsi. Unaweza kuwa na uzoefu mkubwa, lakini bila mwongozo wa Mungu unaweza kuchoka bila matokeo.

2. Kushindwa siyo mwisho

Walijaribu usiku kucha bila mafanikio, lakini hilo halikumzuia Petro kujaribu tena.

Wakati mwingine muujiza wako uko baada ya jaribio la mwisho. Usikate tamaa kwa sababu jana hukufanikiwa. Jaribu tena ukiwa umebeba neno la Mungu.

 3. Neno la Mungu hubadilisha hali

Usiku wa kushindwa ukageuka asubuhi ya baraka kwa sababu ya utii.

Ukiruhusu neno la Mungu lifanye kazi ndani yako na ukalifanyia kazi, linaweza kubadilisha hali ile ile uliyo nayo bila kubadilisha eneo au kazi.

4. Mafanikio yalete unyenyekevu

Baada ya muujiza, Petro hakujivuna. Aliinama mbele za Yesu.

Mafanikio ya kweli humleta mtu karibu na Mungu, si kumweka mbali. Ubarikiwe lakini ubaki mnyenyekevu.

Hatua za mafanikio ya Petro

Hatua ya 1: Kumpa Mungu nafasi

Petro alimruhusu Yesu kutumia mashua yake. Mafanikio huanza kwa kumpa Mungu nafasi katika maisha yako.

Hatua ya 2: Utii wa imani

“Kwa neno lako…”

Fanya hata kama hali haionekani kuendana na mantiki. Imani mara nyingi haiendani na mazingira ya sasa.

Hatua ya 3: Kuchukua Hatua

Petro alishusha nyavu.

Imani bila matendo haizai matokeo. Baada ya kusikia sauti ya Mungu, lazima uchukue hatua.

Hatua ya 4: Ushirikiano

Aliwaita wenzake kusaidia. Mafanikio makubwa yanahitaji watu. Ukiwa peke yako unaweza kwenda haraka, lakini ukiwa na watu utaenda mbali.

Ninaamini ujumbe huu ni kwa mtu anayehisi amechoka, amefanya kazi bila kuona matunda na anafikiria kukata tamaa. Leo Mungu anakusemesha: jaribu tena, lakini safari hii jaribu ukiwa umebeba neno lake.

Umejaribu na kushindwa haimaanishi Yesu ameshindwa. Ukitembea na neno lake, atadhihirisha utukufu wake kwenye kazi yako.

Pia, hata katika maisha ya kila siku, palepale ambapo awali uliona kuna mkwamo, rudi kwa imani ukimtanguliza Mungu, mtu yule yule aliyetaka kukwamisha mambo yako, ukimuendea kwa kumshirikisha Mungu, Mungu atakupa njia hadi watu washangae.

Naomba Mungu akuvushe kutoka eneo la kukata tamaa kwenda eneo la matokeo. Ukaone mavuno katika kazi ileile uliyodhani haina matunda. Kwa neno lake, shusha nyavu tena. Na Mungu atakupa samaki wengi, atakufanikisha kwa kila jambo ambalo umemtanguliza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *