
Dar es Salaam. Katika Jiji la Dar es Salaam, palipo na mzunguko wa maisha usiozimika, Viwanja vya Mnazi Mmoja viligeuka kuwa kimbilio la wanyonge kuanzia Februari 16 hadi 22, 2026.
Chini ya anga la jiji hilo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ilifungua milango ya Kliniki ya Sheria sio kwa ajili ya kutibu maradhi ya mwili, bali kuponya majeraha ya kisheria yaliyokuwa yakiwasumbua wananchi kwa miaka mingi.
Siku ya uzinduzi, shamrashamra zilijaa matumaini. Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji walimiminika wakiwa na bahasha za kaki, mabegi na mikebe ya plastiki, ndani yake zikiwa na nyaraka zilizobeba migogoro ya muda mrefu. Lengo lilikuwa moja: kusogeza huduma za kisheria karibu na mwananchi wa kawaida bila gharama yoyote.
Kufikia kilele cha kliniki hiyo leo Jumapili, Februari 22, 2026, takwimu zilizotolewa na ofisi hiyo zinaonyesha mwitikio mkubwa wa wananchi. Jumla ya mashauri 526 yalipokelewa na kufanyiwa kazi ndani ya siku sita.
Migogoro ya ardhi imeibuka kuwa changamoto kubwa zaidi, ikiongoza kwa mashauri 228, sawa na asilimia 43 ya malalamiko yote yaliyowasilishwa. Hii inaashiria kuendelea kuwepo kwa changamoto za umiliki wa ardhi nchini.
Kati ya mashauri hayo, mgogoro wa ardhi wa eneo la Mbopo, Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni, uliwapa furaha zaidi ya wananchi 400 baada ya mgogoro wa umiliki wa eneo waliloishi kutatuliwa, ambapo watu wawili walikuwa wakidai umiliki wa eneo hilo.
Baada ya ardhi, mashauri ya madai yalishika nafasi ya pili kwa mashauri 83, yakifuatiwa na masuala ya mirathi yaliyosajili mashauri 76.
Katika moja ya mashauri ya madai, Frida Raphael anayedai Sh50 milioni kutoka Halmashauri ya Ubungo kupitia kampuni yake ya Morah Supplies and Manufacturer, alisema alishinda zabuni, akatekeleza majukumu yake kikamilifu, lakini malipo yakawa changamoto iliyomlazimu kufuatilia haki yake kwa miaka minane bila mafanikio.
Kliniki hiyo pia ilishughulikia migogoro ya kifamilia na mahali pa kazi. Mashauri ya ndoa yalikuwa 50, huku migogoro ya ajira ikiwa 47.
Katika mashauri ya ndoa, mojawapo lilihusisha wanandoa waliotengana vyumba kwa miaka minne, huku upande mmoja ukidai kunyanyaswa na kudharauliwa ndani ya nyumba yao.
Kwa upande wa ajira, wafanyakazi watatu waliokuwa wakidai zaidi ya Sh17 milioni ikiwa ni malimbikizo ya mishahara na mafao, walipata ahueni baada ya shauri lao kusuluhishwa na kulipwa stahiki zao.
Kliniki hiyo pia ilishughulikia mashauri 11 ya matunzo ya watoto, pamoja na mashauri manne ya ukatili wa kijinsia yaliyopokelewa na kupatiwa miongozo ya kisheria.
Akizungumza na Mwananchi Februari 22, 2026, Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu wa Kliniki ya Sheria, Ipyiana Mlilo, alisema migogoro ambayo haijapatiwa ufumbuzi itaendelea kufuatiliwa na kukabidhiwa kwa Kamati za Ushauri wa Kisheria za Mikoa na Wilaya ili kuhakikisha haki inapatikana.
Aliongeza kuwa ofisi yao imeweka mfumo maalumu wa kurekodi na kufuatilia mashauri yote yanayoletwa katika kliniki hizo, ili kuhakikisha hakuna shauri linalopotea njiani.
“Tunarekodi migogoro yote katika mfumo maalumu, jambo linalotusaidia kufuatilia kila kesi hadi mwisho na kuhakikisha kila anayestahili haki anaipata,” alisisitiza.