Wakati kitendawili kikiwa kigumu kutegua kuhusu waziri mkuu mashuhuri aliyembaka Virginia Giuffre, utata zaidi unaendelea. Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Barak, ametajwa kwenye Mafaili ya Epstein, kupitia nyaraka za mahakamani kuwa aliwazawadiwa binti mrembo na Jeffrey Epstein.

Binti mwenyewe ni Virginia. Hapa, kuliweka jambo sawa lazima kupitia taarifa za Mafaili ya Epstein, na kitabu cha maisha ya Virginia, kinachoitwa “Nobody’s Girl: A Memoir of Surviving Abuse and Fighting for Justice” – “Si msichana wa yeyote: Kumbukumbu binafsi za kunusurika ukatili na kupambana kwa ajili ya haki.”

Ndani ya kitabu, Virginia amesimulia alivyobakwa na waziri mkuu mashuhuri. Katika Mafaili ya Epstein, imeonesha Virginia alitoa maelezo mahakamani kuwa alisafirishwa kwenda kumhudumia kimapenzi Barak. Je, ni huyo waziri mkuu mashuhuri? Mafaili ya Epstein yamewataja pia mawaziri wakuu wengine wa zamani; Gordon Brown (UK) na Thorbjørn Jagland (Norway).

Virginia ameandika kuwa mwanzo alifundishwa kumstarehesha mwanaume ambaye husikia raha mwanamke anapopitia maumivu makali (sadomasochism). Kipindi alipolazimishwa kufanya ngono, alitakiwa kuvumilia ili mbakaji astarehe.

Machi 10, 2001, Virginia alipokuwa kwenye ratiba ya kumstarehesha mwanamfalme wa UK, Andrew Mountbatten-Windsor, alipata matatizo ya mimba kutunga nje ya mji wa uzazi. Epstein aliagizwa apelekwe hospitali. Akiwa hospitalini alipoteza fahamu. Alipozinduka, Epstein na mshirika wake, Ghislaine Maxwell, walimwambia mimba ilitoka.

Hata hivyo, baadaye aligundua kuwa mimba haikutoka. Badala yake, Epstein aliagiza itolewe ili asiharibu biashara yake. Alimtegemea Virginia kumpeleka kwa wateja wake ili awastareheshe, safari ya uzazi, miezi tisa, jumlisha changamoto zake, uamuzi ambao Epstein aliona wa busara ulikuwa kuitoa mimba.

Hiyo haikuwa mara moja. Mara kadhaa aligundua alitolewa mimba bila idhini yake. Kisha tena, alibaini mpango wa Epstein na Ghislaine, wa kumfanya abebe mimba lakini mtoto awe wao, yaani surrogate mother. Kwa maana hiyo, Epstein alipaswa kumpa ujauzito Virginia, baada ya kujifungua, mtoto angemilikiwa na wapenzi ambao hawakutaka kubebeshana mimba, Epstein na Ghislaine.

Mipango hiyo ya kumfanya Virginia kuwa surrogate mother, ilikwenda na maji baada ya kumpeleka Thailand kwa ajili ya kumsomesha zaidi taaluma ya masaji. Akiwa Thailand alikutana na Robert Giuffre, raia wa Australia, wakapendana, wakakubaliana kufunga ndoa. Walikwenda Australia na kufunga ndoa. Virginia akakata mawasiliano na Epstein, pamoja na Ghislaine.

Simulizi ya Virginia kuhusu kutolewa mimba bila idhini, ni sehemu ya ukatili mkubwa wa Epstein kwa wasichana wadogo. Taarifa zinasema kuwa alipata watoto 10 kutoka kwa mabinti tofauti aliowaingiza kwenye maksri yake kwa ajili ya ngono.

Katika Mafaili ya Epstein, upo ushuhuda wa msichana aliyenyang’anywa mtoto baada ya kujifungua, na hakuwahi kumwona tena. Swali tata ni: je, watoto hao Epstein amewaweka wapi?

Mtu pekee anayeweza kujibu swali hilo ni Ghislaine, ambaye yupo jela akitumikia kifungo cha miaka 20, baada ya kukutwa na hatia ya kushirikiana na Epstein kufanya usafirishaji haramu wa binadamu kwa ajili ya ngono, na kuwatumikisha mabinti wa wadogo kingono. Ghislaine alikuwa mshirika namba moja wa Epstein.

Mark Epstein ni kaka wa Epstein. Februari Pili, 2026, Mark alifanya mahojiano na Business Insider, na kukanusha taarifa kwamba ndugu yake alipata kuwa na mtoto.

Mark alisema, katika miaka yote 66 ambayo Epstein aliishi dunia, hakuna taarifa yoyote ndani ya familia yake iliyoonesha aliwahi kuwa na mtoto. “Kama Epstein angekuwa na mtoto, ningejua,” alisisitiza Mark.

Kanusho la Mark lilifuata baada ya rundo la ujumbe katika Mafaili ya Epstein, kuonesha mawasiliano mbalimbali, ikiwemo pongezi kwa Epstein kupata mtoto wa kiume. Hii inaonesha kuwa pamoja na Mark kujinasibu, hakujua mambo yote.

Katika ujumbe uliotumwa Septemba 2011, ukiwa na saini ya “Sarah XX”, na cheo cha “The Duke”, kikitajwa. Ni ujumbe wa mtandao wa BlackBerry Messenger (BBM). Jina la mtuma ujumbe na barua pepe vimehaririwa na Wizara ya Haki Marekani (DOJ). Hata hivyo, ukiunganisha ujumbe, jina “Sarah”, na cheo “The Duke”, unaweza kuelewa wahusika.

Vyombo vya habari vya UK, ikiwemo BBC, wamekwenda mbele bila kupindisha kuwa Sarah aliyepeleka ujumbe wa BBM kwa Epstein ni Sarah Ferguson, mtalaka wa Andrew (mwanamfalme wa UK). Na “The Duke” ni “Duke of York”, cheo cha heshima cha Andrew, alichopewa na mama yake, Malkia Elizabeth II.

“Sijui kama bado upo kwenye hii BBB, lakini nilisikia kutoka kwa Duke kwamba ulipata mtoto wa kiume,” ujumbe mmoja uliandikwa hivyo na Sarah, aliendelea: “Hata kama hujataka kuendelea kuwasiliana nami, mimi bado nipo kwa upendo, urafiki, na nakupongeza kwa kupata mtoto wa kiume.”

Sehemu nyingine ya ujumbe, Sarah anamlaumu Epstein kwa kumtumia yeye ili awe karibu na Andrew, kitu ambacho kilimuumiza sana, kugundua kwamba Epstein alijenga urafiki kama chambo kwenye ndoano ili kunasa samaki. Andrew ndiye samaki mwenyewe.

“Umepotea. Sikujua hata kama una mtoto,” aliandika Sarah, kisha akalaumu: “Ni dhahiri kabisa kwangu kwamba ulikuwa rafiki yangu ili umpate Andrew. Na hilo kwa hakika limeniumiza kwa kiwango kikubwa. Zaidi ya utakavyojua.”

Ukiacha suala la watoto, kitendawili kingine ni jinsi ambavyo Epstein alijiweka karibu na matajiri wakubwa, wanasiasa wenye nguvu kubwa ya ushawishi, na watu wengine mashuhuri, kisha kuwaingiza kwenye mtego wake.

Ukipitia nyaraka za Mafaili ya Epstein, unaweza kupata jibu ni kwa namna gani mhalifu huyo wa ngono alikuwa na uwezo mkubwa wa kuteka watu kisaikolojia.

Epstein alikuwa akijipambanua kuwa “mkusanya watu.” Alipo, watu wangemzunguka. Alipofahamiana na tajiri mmoja, angehakikisha matajiri wengine katika mtandao wa yule wa kwanza, nao wanakuwa kwenye duara lake. Alikuwa mzuri kutambua haraka kile ambacho mtu alikuwa akinahitaji, kisha angejitokeza kama mwenye suluhisho.

Namna ya kwanza ni kama yalivyo manung’uniko ya Sarah kuwa Epstein alimtumia ili amfikie Andrew, na baada ya kumpata, hakutaka kuendelea na mawasiliano naye. Maana yake, Epstein aliwatumia watu kuwapata aliowahitaji, na alipofanikisha malengo, hakuendelea na ule wa mwanzo, hasa alipoona haukuwa na faida kwake.

Mpango mwingine alioutumia Epstein kunasa watu ni kwa njia ya zawadi zenye thamani kubwa. Mfano, zawadi kubwa iliyoonekana kwenye Mafaili ya Epstein ni saa. Mtu aliyehitaji kumvuta, angemtumia saa, na pale alipobaini mtu husika alipendelea aina fulani ya vitu, alimtafutia akipendacho ili kumteka na kujenga ukaribu naye.

Baada ya kumpata mtu aliyemlenga, Epstein alijipambanua mbele yake kama mwenye msaada mkubwa katika maisha yake ya kila siku. Angejionesha kuwa alikuwa na maarifa makubwa ya fedha na kodi, au alivyojuana na watu wengi mashuhuri, hasa matajiri, na wafanya uamuzi serikalini. Hatua iliyofuata ingekuwa kumuingiza kwenye dhambi ya kufanya ngono na mabinti wadogo.

Itaendelea kesho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *