
ALIYEKUWA Kocha wa Songea United, Meja Mstaafu, Abdul Mingange, amesema ameamua kuachana na timu hiyo kwa makubaliano ya pande mbili, licha ya kutofikia malengo aliyojiwekea tangu mwanzoni mwa msimu ya kuipandisha Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Mingange aliyezifundisha pia Ndanda, Mbeya City na maafande wa Tanzania Prisons, amesema uamuzi huo ni wa kwake mwenyewe baada ya kuona kuna vitu haviendi sawa na matarajio anayotaka, hali inayosababisha timu hiyo kutokuwa na mwenendo mzuri.
“Kuna vitu vingine sio vizuri kuviweka wazi, lakini ukweli ni kwamba ni mimi mwenyewe niliyeamua kuondoka kwa makubaliano ya pande mbili, matarajio yalikuwa makubwa sana, ila kwa bahati mbaya sikuweza kufikia malengo hayo,” amesema.
Mingange anayekumbukwa msimu wa 2022-2023, baada ya kuwapandisha maafande wa Mashujaa Ligi Kuu Bara, amesema mwanzo mwa msimu ulikuwa mgumu kutokana na wingi wa wachezaji wapya, ingawa kwa sasa ameiacha ikiwa tayari wamezoeana kiuchezaji.
Kocha huyo alijiunga na timu hiyo Desemba 10, 2024, akitokea Stand United ili kurithi mikoba ya Ivo Mapunda, ambapo kwa msimu huu ameiongoza katika mechi 18, akishinda tano, sare sita na kuchapwa saba, ikiwa nafasi ya tisa kwa pointi 21.