Hatimaye, Mirambo Yusuf amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Chama cha Wananchi (CUF) baada ya kupata kura 257 alizopigiwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa dharura wa chama hicho, uliofanyika katika Ukumbi wa Lekham, Buguruni, jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo Jumapili Februari 22, 2026.

Hata hivyo, mshindani wake aliyefuatia kwa wingi wa kura, Othman Omar Dunga, alipata kura 177 na ameonyesha wasiwasi kwa wajumbe walioshiriki katika uchaguzi huo, akidai kuwa ana mashaka nao kwa kuwa wengi wao hawakuwa wajumbe halali kwa mtazamo wake.

Mirambo, ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Kigoma Mjini, amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa nne wa chama hicho, akirithi rasmi mikoba ya Profesa Ibrahim Lipumba katika nafasi hiyo. Mgombea wa tatu, Nkunyunyika Siwale, alipata kura 6 kati ya jumla ya kura 448 zilizopigwa, huku kura sita zikiharibika.

Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Miraji Mtibwiliko amepata kura 264 na kuwashinda Mohammed Ngulangwa aliyepata kura 88 pamoja na Mussa Mbarouk aliyepata kura 82.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar imechukuliwa na Haroub Mohamed Shamsi aliyepata kura 256, akimshinda Mbarouk Seif Salim aliyepata kura 171, huku Amina Rashid Salim akijitoa kabla ya upigaji kura.

*Wasifu*
Mirambo, ni mkazi wa Kigoma na mzaliwa  wa mkoani Tabora mwaka 1971. Kitaaluma ni Mwandishi wa Habari, mtaalamu wa lugha za Kiswahili, Kifaransa na Kiarabu,  pia ni mwalimu wa mpira wa miguu.

Mbali na hivyo amekuwa Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kigoma Ujiji kwa miaka 10 sasa, ambapo alikiongoza chama katika vuguvugu la Muungano Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), katika Uchaguzi Mkuu 2015, uliohusisha vyama vya Chadema na NLD.

Baada ya kunyakua wadhifa huo, amesema atahakikisha ndani ya chama kunakuwa na matumizi sahihi ya fedha za chama. Kipaumbele chake kitakuwa ni kuhakikisha watumishi wanalipwa kwa wakati ili wapate ari na morali ya kazi, kisha kuimarisha ngazi za chini za chama.

“Nataka kutengeneza taasisi inayoaminika na kupata wadau sahihi watakaosaidia chama kupiga hatua kwa kupata fedha,” amesema.

Katika maelezo yake amesema kuwa siasa za Tanzania zinapaswa kuwa siasa za ukombozi kwa kujenga mtandao wa chini utakaopanua wigo wa kura, badala ya kujikita zaidi katika siasa za upinzani.

“Mimi ni muumini wa siasa za ukombozi na ninaamini zinaweza kutuvusha kutoka hapa tulipo ili tuweze kuvuka hatua hii. Nitakuwa kiongozi mzuri kupitia fursa nitakayopata ili tufikie maendeleo endelevu,” amesema.

Pia, amesema amejipanga kutatua migogoro ya chama hicho kwa kuanza kuchunguza chanzo chake, ili kupata suluhu ya kudumu kupitia njia sahihi zitakazowezesha kufikia hatua bora.

“Kwanza nitajenga mtandao sahihi wa kukutana na wananchi. Nitatumia fedha kwa weledi kuwafikia wananchi na kumaliza migogoro. Nikipewa nafasi, nitafanya mageuzi makubwa kwa maslahi ya chama na taifa,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *