Songwe. Watu watatu akiwamo mwanafunzi wa darasa la pili, wamefariki dunia kufuatia mvua zinazoendelea katika maeneo mbalimbali mkoani Songwe huku Jeshi la Polisi likiwakumbusha wananchi kuchukua tahadhari.

Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo Februari 21, 2026 imeeleza kuwa matukio ya vifo, hivyo yametokea   Februari 20, 2026 katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kufuatia mvua zinazoendelea likiwataka wananchi kuchukua tahadhari.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa tukio la kwanza lilitokea saa 10 jioni katika Kijiji cha Ssenga, Kata ya Halungu wilayani Mbozi ambapo mtu mmoja, Said Kamwela (62) alifariki dunia kwa kuzama kwenye maji.

Imefafanua kuwa Kamwela alifariki dunia wakati akioga kwenye mto Halumu kutokana na kina kikubwa cha maji kilichosababishwa na mvua iliyonyesha na kusababisha kifo chake.

Tukio lingine lilimuhusisha mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Migombani, Janeth Tarimo baada ya kuteleza na kutumbukia katika korongo lililokuwa na maji mengi alipokuwa akitoka shuleni kisha kusombwa na maji hayo, saa 10 jioni huko Kaloleni wilayani Momba.

Pia, imeeleza kuwa saa 1 usiku, mtu mmoja ambaye hajafahamika jina lake anayekadiriwa kuwa na miaka 30, alifariki dunia baada ya kuteleza na kutumbukia kwenye korongo lililokuwa likitiririsha maji kutokana na mvua zinazoendelea.

Kufuatia matukio hayo, Jeshi la Polisi mkoani humo, limewataka wananchi kuchukua tahadhari kipindi hiki cha mvua nyingi, ikiwa ni kuepuka kuvuka mito na madaraja yasiyo imara na makorongo yanayopitisha maji.

“Waepuke kutembea au kukatiza katika maeneo yenye miteremko mikali na mikondo ya maji, vilevile linawataka wazazi na walezi kufuatilia kwa karibu watoto wanapokwenda na kurudi shuleni na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi wanapoona hatari ya miundombinu.

“Jeshi la Polisi litashirikiana na mamlaka au idara husika kuhakikisha usalama wa wananchi unaimarishwa kwa kipindi chote, ili Mkoa wa Songwe uendelee kuwa salama,” imeeleza taarifa hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *