
Dar es Salaam. Mwenyekiti mpya Chama cha Wananchi (CUF), Mirambo Yusuf ataongoza kikao cha Baraza Kuu la chama hicho chenye lengo la kubariki majina ya makada waliopendekezwa kuteuliwa kuwa watendaji akiwemo anayefaa kushika wadhifa wa Katibu Mkuu.
Majina mengine yatakayowasilishwa kwenye kikao hicho leo Jumapili, Februari 22, 2026 ni ya Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.
Kabla ya kuwasilishwa katika kikao hicho, Mirambo atakuwa ameshafanya mashauriano na Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Miraji Mtibwiliko, pamoja na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Haroub Mohamed Shamsi.
Hatua hiyo inafuatia ushindi wa viongozi hao watatu katika uchaguzi uliofanywa jana Jumamosi na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, uliofanyikia ukumbi wa Lekham, Buguruni jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuziba nafasi za juu za uongozi.
Uchaguzi huo ulifanyika baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutengua matokeo ya uchaguzi uliokuwa umeuweka madarakani uongozi uliopita.
Sababu ya kutengua uchaguzi huo uliomweka madarakani Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye alikiongoza chama hicho kwa miaka 27, pamoja na wenzake watatu, ni kwamba kura walizopata hazikufikia zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa.
Kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, matokeo hayo yalilazimu mchakato wa uchaguzi kurudiwa.
Katika mkutano wa leo, Mirambo na wenzake watawasilisha majina hayo mbele ya Baraza Kuu ili yajadiliane na kupima iwapo yanakidhi mahitaji ya sasa ya chama, hasa katika kipindi hiki ambacho kinakabiliwa na changamoto za uongozi na kifedha.
Baada ya mkutano huo, Mirambo atawatangaza rasmi watendaji hao watatu, ambao kwa pamoja wataunda kamati tendaji ya chama. Kisha, wataendelea na vikao vya ndani kwa ajili ya kufanya uteuzi wa watendaji wengine wa kila siku katika makao makuu ya chama.
Mkutano wa jana, ambao Msajili wa Vyama vya Siasa hakuhudhuria kama ilivyo desturi katika chaguzi nyingine za vyama, ulitawaliwa na matukio yaliyoibua maswali mengi kuhusu mustakabali wa chama hicho, hasa kutokana na migogoro ya uongozi inayokikumba.
Licha ya mkutano kuanza ukumbini na baadaye wajumbe kutolewa nje huku kura zikihesabiwa katika makao makuu ya chama, kulikuwa na kauli za vijembe kutoka kwa baadhi ya wajumbe, waliodai kuwa huo ni wakati wao ‘kula matunda ya chama’.
Baadhi yao walieleza wamepitia changamoto nyingi wakidai haki ndani ya chama, huku wakidai kutengwa kwa muda mrefu.
Hata hivyo, kuna kundi linaloamini kuwa chama hicho hakina mustakabali mzuri iwapo kitaendelea kuendeshwa kwa mfumo unaodaiwa kupokea maelekezo kutoka katika mifumo ya dola.
Mjadala huo uliibuka pia wakati wa kampeni za wagombea wa nafasi za juu, ambapo baadhi walionya kuwa endapo chama kitaendelea kwa mfumo huo, huenda kikawa katika hali mbaya zaidi kuliko kilipotoka.
Ingawa Mwenyekiti huyo mpya, katika hotuba yake na hata kwenye kuomba kura, moja ya ahadi yake ambayo ameitoa ni kuhakikisha anakiunganisha chama hicho kwa kufanya kazi nao wote pamoja bila kujali yuko upande ambao haukubaliani na msimamo wake.
Ndani ya chama hicho yapo makundi mawili ambayo kwa kiasi fulani yalikuwa tangu muda mrefu ingawa yamekuja kulipuka kufuatia uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa Februari 13, 2026, baada ya kutoa uamuzi wa kubatilisha uchaguzi uliomweka madarakani Profesa Lipumba na wenzake.
Katika makundi hayo kundi la Profesa Lipumba lenyewe linadai linaenda mahakamani kupinga uamuzi wa Msajili kwa kuwa wanadai imefanyika bila kuzingatia haki ya msingi ya wao kupewa nafasi ya kusikilizwa, ingawa baadhi yao waligeuka na kwenda kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa jana, hata hivyo hawakushinda.
Kundi lingine linakubaliana na uamuzi wa Msajili ndiyo maana lilikuja mstari wa mbele kukubali kuingia katika mchakato wa kuandaa uchaguzi huo wa zimamoto (dharura) kuziba nafasi hizo za juu, kwa hoja waliyoeleza kuwa kukiacha chama bila uongozi kinaweza kuchukuliwa na mateka.
Kazi iliyobakia ni Mirambo ambaye anakuwa Mwenyekiti wa nne wa chama hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 1992, kukiunganisha chama hicho kuwa kitu kimoja na taswira ya kuvuka hatua hiyo itaanza kujionyesha kwa kuangalia nafasi hizo za kitendaji za juu.
Ingawa atakabiliwa na ushindani kutoka kwa wafuasi wake waliomweka madaraka ambao kimsingi dhamira yao na msimamo wao ni kuwa enzi za Profesa Lipumba zimeisha hivyo ni wakati wao wa kula neema na waliokuwa wakifaidika ni wakati wa kupitia nyakati ngumu (kuimba kulia kupokezana).
Endelea kufuatilia Mwananchi