BEKI wa zamani wa Yanga Princess, Noela Luhala, ametambulishwa rasmi kujiunga na timu ya wanawake ya MFA Zalgiris ya Lithuania, hatua inayomfungulia ukurasa mpya katika soka la Ulaya.

Noela anajiunga na timu hiyo akitokea 1207 Antalya Spor Kulubu ya Uturuki ambayo inaelezwa beki huyo alivunja mkataba alipocheza mechi 12 za ligi na kufunga bao moja.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 20 aliwasili jijini Vilnius mapema mwezi huu na tayari amecheza mechi tatu. Luhala alianza mechi yake ya kwanza Februari 8 kwenye mashindano ya Winter Cup dhidi ya Kauno Rajono Futbolo Akademija, akiifungia bao katika ushindi wa mabao 6-0, mechi nyingine alicheza dhidi ya MFK na Saku Sporting.

Akizungumza baada ya kutambulishwa, Luhala amesema ameanza kuzoea haraka maisha ya Lithuania, akiwasifu wachezaji wenzake pamoja na benchi la ufundi kwa kumpokea vizuri.

“Nashukuru Mungu niko vizuri hapa wachezaji ni marafiki na wamenisaidia kuzoea mazingira mapya, makocha ni wataalamu wa kweli, na mazoezi ni ya kuvutia changamoto kubwa pekee ni baridi,” amesema Noela.

Beki huyo anajiunga na timu hiyo akitokea kuandika rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kuitumikia ligi hiyo na kabla ya hapo aliitumikia pia Asa Tel Aviv inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Israel.

Zalgiris ni moja ya majina makubwa katika soka la Lithuania, likiwa na historia ndefu katika mpira wa wanaume na wanawake. Timu ya wanawake ya klabu hiyo imekuwa ikishiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini humo inayojulikana kama A Lyga Women ambayo ni ligi kubwa.

Kwa miaka ya hivi karibuni, Zalgiris Women imekuwa ikijijenga kama moja ya timu zenye ushindani mkubwa kwenye ligi hiyo, ikipambana mara kwa mara kuwania ubingwa na nafasi za kushiriki michuano ya Ulaya.

Mbali na ligi ya ndani, timu hiyo pia mara kadhaa imeshiriki Kombe la Wanawake la Lithuania, mashindano ya mtoano yanayozikutanisha timu bora kutoka madaraja mbalimbali ya nchi hiyo.

Klabu hiyo pia imelenga kujenga ushindani wa kimataifa, ambapo timu bingwa wa ligi hupata nafasi ya kuiwakilisha Lithuania katika michuano ya UEFA Women’s Champions League kuanzia hatua za awali za mtoano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *