
Same. Stephano Zawadi (43), mkazi wa Kitongoji cha Kambeni, Kata ya Myamba, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro amefariki dunia kwa kupigwa radi wakati alipokuwa akimfuata mkewe shambani kuzuia tumbili wasile mahindi.
Imeelezwa mwanaume huyo baada ya kurudi ibadani jioni ya leo Februari 22,2026, alimfuata mke wake shambani alikokuwa akilinda tumbili wasile mazao yao na wakati yupo njiani alipigwa na radi na kufariki dunia.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Mishaeli Kisaka amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Ni kweli kuna mvua kidogo na radi ni nyingi, na imeleta madhara hapa kwetu jioni hii saa 10 na dakika kadhaa , kijana mmoja amefariki wakati akienda shambani kumfuata mke wake, ameungua kifuani na shingoni,” amesema mwenyekiti huyo.
Baba wa marehemu, Zawadi Nkuku, amesema kijana wake huyo amefariki dunia kwa kupigwa na radi hatua chache kutoka nyumbani kwake wakati alipokuwa akimfuata mke wake shambani.
“Mvua ilikuwa inanyesha sasa mtoto wangu alipotoka kanisani alikuja nyumbani, baadaye kidogo akatoka kwenda shambani maana kuna ulinzi wa tumbili wanaokula mahindi ili apokezane na mke wake aje aandae chakula cha jioni,yeye abaki alinde tumbili.”
“Wakati anatoka nyumbani kulikuwa na radi sana, hakufika hata shambani ndio akapigwa na radi njiani akafariki,” amesema.
Amesema kwa sasa mwili upo nyumbani wanaangalia utaratibu wa kuuhifadhi.