
London, England. Tottenham Hotspur itawakosa nyota tisa tegemeo leo wakati itakapokuwa kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Tottenham kuikabili Arsenal katika mchezo wa Ligi Kuu England.
Pamoja na uhakika wa kumtumia Richarlison, Spurs itawakosa Cristian Romero, Ben Davies, Destiny Udogie, Pedro Porro, Rodrigo Bentacur, Lucas Bergvall, Dejan Kulusevski, James Maddison na Mohammed Kudus.
Wachezaji nane kati ya hao, watakosekana kwa sababu ya majeraha tofauti yanayowakabili lakini nahodha Cristian Romero yeye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu.
Lakini wakati Spurs ikiwakosa nyota hao tisa, Arsenal yenyewe ina habari njema ya uhakika wa kuwatumia Bukayo Saka na Leandro Trossard ambao walionekana kuumia katika mchezo uliopita dhidi ya Wolves lakini pia kuna uwezekano mkubwa ikawa na Kai Havertz na Martin Odegaard ambao walikuwa majeruhi.
Ni mchezo wa kwanza wa Watani wa Jadi wa Kaskazini mwa London kwa Meneja wa Spurs, Igor Tudor ambaye alipewa kibarua cha kuinoa timu hiyo hivi karibuni akichukua nafasi ya Thomas Frank aliyetimuliwa.
Ushindi katika mchezo huo utaifanya Arsenal ifikishe pointi 61 ambazo zitaifanya iendelee kuongoza msimamo wa ligi wakati kwa Spurs utaifanya ifikishe pointi 32.
Ukiondoa mchezo huo, Crystal Palace itaikaribisha Wolves na Nottingham Forest itakuwa nyumbani kucheza na Liverpool.
Sunderland itakuwa mwenyeji wa Fulham na kesho, Everton itakuwa nyumbani kucheza na Manchester United.