Shinyanga. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linatarajia kuingiza kwenye gridi ya Taifa umeme unaozalishwa kwa nishati ya jua kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake.

Hayo yameelezwa jana Jumamosi, Februari 22, 2026 na Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Lazaro Twange alipofanya ziara ya siku moja kukagua miradi ya uzalishaji, upoozaji na usambazaji umeme katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga.

Twange amesema mradi huo uliopo Kijiji cha Ngunga, Wilaya ya Kishapu mkoani Simiyu, umegharimu Sh118 bilioni na unatarajiwa kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa kuanzia Machi mwaka huu.

Umeme huo wa jua utaiwezesha nchi kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati 4,300 zilizokuwapo awali hadi kufikia megawati 4,350 kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani.

Amesema huo ni mradi wa kwanza mkubwa wa uzalishaji umeme wa jua unaomilikiwa na Serikali, akibainisha kuwa, tangu uhuru, miradi ya aina hiyo imekuwa ikitekelezwa zaidi na sekta binafsi pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), lakini si kama mradi kamili wa Serikali kupitia Tanesco.

Twange amesema awamu ya pili itatekelezwa katika eneo hilo na itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 100.

Pia, amesema shirika hilo liko katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi wa mradi huo, huku zaidi ya Sh200 bilioni zikitarajiwa kuwekeza katika utekelezaji wake.

“Tayari fedha zimeshapatikana na wakati wowote mwaka huu tutasaini mkataba na mkandarasi ili kuanza kazi,” amesema Twange.

Pia, ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa ushirikiano uliotolewa katika upatikanaji wa eneo la mradi, akieleza kuwa, licha ya wananchi 112 kuhamishwa kupisha utekelezaji wake, hadi sasa hakuna malalamiko wala migogoro iliyoripotiwa, huku Sh302 milioni zikitumika kulipa fidia.

 Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi amesema utekelezaji wa mradi huo ni faraja kwa wananchi kwa kuwa unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuongeza ajira na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Amesema wilaya hiyo bado inahitaji nishati zaidi, ikiwamo megawati 100 zitakazozalishwa katika awamu ya pili kutokana na ongezeko la vijana wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji madini zinazohitaji umeme wa kutosha na wa uhakika.

Masindi pia ametoa wito kwa wananchi wa maeneo mengine kuiga mfano wa wakazi wa Ngunga kwa kutoa maeneo yao kwa hiari pale Serikali inapohitaji kutekeleza miradi ya maendeleo, akieleza kuwa kusuasua kwa baadhi ya wananchi kuachia maeneo kumekuwa kukichelewesha utekelezaji wa miradi.

Kaimu Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme wa Jua cha Kishapu, Mariana Mrosso amesema kituo hicho kitaongeza uthabiti wa volteji Kanda ya Ziwa.

Amesema Kishapu ilichaguliwa kutokana na kuwa na mwanga wa jua wa kutosha na pia ukosefu wa miradi mingine ya uzalishaji wa umeme katika kanda hiyo, isipokuwa Kituo cha Nyakato kinachotumia mafuta.

Katika hatua nyingine, Twange ameonesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Shinyanga kwenda kituo cha kupooza umeme cha Simiyu. Amesema mradi huo ulioanza Oktoba mwaka jana ulipaswa kuwa umefikia asilimia 47 ya utekelezaji, lakini hadi sasa umefikia asilimia 27 pekee, huku ukitarajiwa kukamilika Juni mwaka huu.

Kutokana na hali hiyo, amesema atakutana na mkandarasi ili kubaini changamoto zilizokwaza utekelezaji wa mradi huo, licha ya malipo kufanyika kwa mujibu wa makubaliano.

Kituo hicho cha kupooza umeme kinajengwa kwa lengo la kutatua tatizo la umeme usio na nguvu katika Mkoa wa Simiyu.

Uamuzi wa kujenga kituo hicho ulitokana na ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyofanya mkoani humo Juni mwaka jana, alipokea malalamiko ya wananchi kuhusu umeme hafifu na kuidhinisha Sh7 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

Kwa muda mrefu, Mkoa wa Simiyu umekuwa ukipokea umeme kutoka maeneo ya mbali, ikiwamo Shinyanga, hali inayosababisha kupungua kwa nguvu ya umeme unapowafikia watumiaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *