Dodoma. Farida amekuwa akisifika kama mtoto mwenye nidhamu kwa wazazi wake. Mara zote Farida amekuwa msikivu, mtii mwenye heshima kwa watu. Mpaka anamaliza darasa la saba, Farida hakuwahi kupishana na wazazi kwa namna inayozua tahayaruki.

Mambo yalianza kubadilika Farida alipoanza kidato cha pili. Siku moja wakati saa ya kwenda kanisani imefika, Farida hakuonekana kuwa na haraka tofauti na kawaida yake.

“Unafanya nini muda wote jamani mbona kama huna haraka?” aliuliza mama yake kwa hasira.

“Nipo najiandaa mama,” Farida anajibu huku akiendelea kutengeneza nyusi zake. Dakika 15 zinapita. Farida hajatoka chumbani kwake. Hali inaanza kubadilika.

“Muda umeisha Farida na tunachelewa ibada,” baba aliamua kuingilia kati.

Farida hasemi. Ukweli ni kwamba Farida hakuwa na nia ya kwenda kanisani akiambatana na wazazi wake. Farida anakosa ujasiri wa kulisema hili wazi wazi kwa wazazi wake.

Baada ya dakika 10 za kusubiri, baba alikumbushia kwa hasira: “Unafanya nini chumbani saa zimeenda?”

‘Basi tangulieni baba. Mie nitakuja mwenyewe!’ Hicho ndicho alichokuwa anakitaka. Hakupenda kuambatana na wazazi wake.

Katika umri wake wa miaka 14, Farida ameanza kujenga umbali na familia yake. Wazazi wake hawajaligundua hili.

Hata wanapozungumza naye, Farida haonekani kufuatilia wanachokisema. Tofati na ilivyokuwa zamani, kwa mfano, Farida alikuwa mchangamfu katika mazungumzo. Siku hizi ameanza kuwa mkimya kupindukia hasa anapokuwa nyumbani.

Hata hivyo, anapokuwa shuleni akiwa na marafiki zake, Farida ni mwongeaji mzuri. Huwezi kuamini ni Faida huyu mkimya anayeonekana kuwa mpweke na mkimya anapokwa nyumbani. Kwa nini basi Farida anakuwa mkimya anapokuwa nyumbani?

Ukweli ni kwamba Farida ana mahangaiko mengi moyoni mwake kama kijana chipukizi. Matamanio ya kujihakikishia hadhi sawa na mtu mzima yanamfanya ahisi wazazi wake hawamwelewi. Wanaposisitiza kwenda naye kanisani, hiyo kwake ni sawa na kumchukulia kama mtoto asiyeweza kujisimamia. 

Kwa upande mwingine, wakati wazazi wake wanafikiri kuambatana naye ni kumjali, Farida anahitaji uhuru zaidi. Wasiwasi wa wazazi wake unatokana na hatari ya uhuru ambao bila shaka Farida anauhitaji. Wazazi wanaamini Farida bado ni mtoto anayehitaji uangalizi wa karibu. Changamoto, hata hivyo, wanapomsogelea Farida anajisikia ‘kufuatwa fuatwa.’ Hili linawaacha kwenye dunia mbili tofauti.

Je, wazazi wafanye nini kuwasiliana na binti yao Farida? Swali hili ni gumu maana ni kweli unaweza kuzungumza na mtu msiyewasiliana. Mawasiliano ni tofauti na mazungumzo.

Unaweza kuzungumza na yeyote. Msingi wa mazungumzo ni kile kinacholengwa. Mawasiliano, kwa upande mwingine, ni uwezo wa kufikisha ujumbe kwa namna inayomfanya mlengwa ajisikie kueleweka na kutambulika. Ili hili liwezekane, hatua ya kwanza ya mawasiliano ni kugusa hisia za mtu.

Hisia zinatawala sehemu kubwa ya maamuzi yetu. Ingawa tunapenda kujichukulia kama watu tusioongozwa na hisia, ukweli wa kisayansi ni kwamba nyuma ya maamuzi yetu mengi kuna mkusanyiko mkubwa wa hisia.

Usipoweza kuelewa hisia za mtu huwezi kuwasiliana naye. Farida ana hisia zake ambazo wazazi wake hawajazielewa. Ingawa wanazungumza na Farida, bahati mbaya hawajaweza kuelewa kwa nini Farida ‘anajivuta vuta’ chumbani kwake na haonekani kuwa na haraka. Kutokuelewa hisia za mtu unayewasiliana naye kunaweza kukuzuia kufikisha ujumbe kama ulivyokusudia.

Kama kuna eneo muhimu kwa sisi wazazi kulizingatia ni kuelewa hisia za watoto kabla hatujawapa maelekezo, maagizo na mawaidha. Hili linalifanyia kazi kuanzia makala inayofuata.

Jambo la pili ni kuelewa kwamba hisia za watoto hubadilika kadri mtoto anavyokua. Hisia za mtoto wa miaka minne zinaweza kuwa tofauti sana na mtoto wa miaka minane na kadhalika na kadhalika. Tukitaka kuwasiliana na watoto kwa namna inayofikisha ujumbe tunalazimika kujifunza hisia zao.

Kuna umri, mathalani, hatuhitaji kuzungumza zaidi. Tukitaka kuwasiliana na mtoto tunahitaji kumsikiliza. Kadri anavyokua, mahitaji yake ya kihisia nayo yanabadilika. Ili tuwasiliane naye tunahitaji kuelewa hisia zilizo nyuma ya matendo yake, maneno yake, matarajio yake na kadhalika na kadhalika.

Fuatilia makala kadhaa zinazofuata kujifunza zaidi kuhusu hisia na namna ya kuzitumia kuimarisha mawasiliano naye kulingana na umri wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *