
Dar es Salaam. Kuvunjika kwa ndoa ni tukio linalotikisa misingi ya familia na kuacha maumivu makubwa kwa wanandoa, lakini kwa mujibu wa wataalamu wa saikolojia ya mtoto, madhara makubwa zaidi huwakumba watoto endapo wazazi hawatakuwa makini katika kipindi cha mpito.
Kona ya Mzazi ya Mwananchi leo Jumapili inaangazia mbinu sahihi za malezi baada ya talaka, huku wataalamu wakisisitiza kuwa ustawi wa mtoto unapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kuliko tofauti za wazazi.
Akizungumzia hilo nilipomdodosa nilipokutana naye hivi karibuni, mtaalamu wa saikolojia ya familia, Dk Rose Mwakyembe aliniambia kwamba, mtoto anayeshuhudia migogoro ya wazazi au kukosa upendo kutoka kwa mmoja wao, hukua akiwa na majeraha ya kihisia yanayoweza kudumu hadi utu uzima.
“Talaka si chanzo cha tatizo kubwa kwa mtoto, bali ni namna wazazi wanavyoshughulikia talaka hiyo. Mtoto huhitaji kujua bado anapendwa na wazazi wake wote,” anasema.
Kwa mujibu wa wataalamu, nilichokibaini, kosa la kwanza linalofanywa na wazazi wengi ni kuwahusisha watoto katika migogoro yao.
Ni jambo lisilo na kificho na limeshuhudiwa na linaendelea kushuhudiwa na wengi. Wapo baadhi ya wazazi huwatumia watoto kama wajumbe wa maneno makali au kama nyenzo ya kulipiza kisasi.
Mtoto anapolazimishwa kumchagua mzazi mmoja, hupoteza usalama wa kihisia na huanza kujilaumu kwa mgogoro ambao hakuuanzisha yeye, bali unawahusu wazazi wake tu.
Lakini wataalamu wanasisitiza umuhimu wa mawasiliano yenye heshima kati ya wazazi hata baada ya kuachana.
Hili linathibitishwa na Dk Mwakyembe ambaye aliniambia kwamba, wazazi wanapaswa kujifunza kuzungumza kwa utulivu kuhusu masuala yanayomhusu mtoto kama elimu, afya na nidhamu. “Matusi au lawama mbele ya mtoto humfundisha chuki badala ya maadili ya maelewano.
Anasea mbinu nyingine muhimu ambayo mzazi anaweza kuitumia ni ya kudumisha utaratibu na ratiba anayompa mtoto wake ambayo inaweza kuwa dira ya maisha yake. Hoja hii inaungwa mkono na mtaalamu wa makuzi na maendeleo ya mtoto, Profesa Joseph Mhando ambaye anasema watoto huhitaji uthabiti ili kujenga hali ya usalama.
“Mabadiliko ya ghafla ya makazi, shule au mlezi bila maelezo, huongeza hofu na msongo wa mawazo kwa mtoto,” anasema.
Ili kuliepuka hilo, anashauri wazazi kukubaliana na ratiba ya kuonana na mtoto na kuizingatia bila kuyumbishwa na migogoro yao binafsi.
Katika malezi baada ya talaka, wataalamu pia wanahimiza wazazi kuwaruhusu watoto kueleza hisia zao.
Katika hili, mara nyingi huwa tunashuhudia watoto wengi hukosa mtu wa kuwasikiliza, hivyo huamua kujifungia kimya. Kuepusha hilo, mzazi anapaswa kusikiliza bila kuhukumu na kumhakikishia mtoto kuwa talaka si kosa lake.
Aidha, ushirikiano wa wazazi katika malezi unatajwa kuwa nguzo muhimu ya kumlinda mtoto kimaadili. Hata kama wazazi hawaishi pamoja, wanapaswa kushirikiana katika maamuzi muhimu.
Mtoto anayewaona wazazi wake wakishirikiana, hujifunza thamani ya uwajibikaji na heshima.
Hata hivyo, ni lazima wazazi waliotalakiana wakachukua tahadhari dhidi ya tabia ya kutumia zawadi au fedha kama njia ya kujijengea nafasi kwa mtoto.
Wazazi mkumbuke kwamba upendo wa kununua huathiri nidhamu na maadili ya mtoto. Uwepo wa mzazi na muda anaoutenga kwa mtoto vina thamani kubwa kuliko mal.
Na kwa wazazi wanaopitia changamoto kubwa, wataalamu wanashauri kutafuta msaada wa kitaalamu.
Ushauri wa kisaikolojia, viongozi wa dini au washauri wa familia wanaweza kusaidia mzazi na mtoto kuvuka kipindi hiki kwa usalama.
Kwa ujumla, ndoa inaweza kuvunjika, lakini wajibu wa malezi hauvunjiki. Mtoto anayelelewa katika mazingira ya upendo, heshima na ushirikiano wa wazazi, ana nafasi kubwa ya kukua akiwa imara kimaadili na kihisia. Huo ndio msingi wa wa familia yenye afya na mustakabali imara hata ikiwa katika mtamziko wa wazazi kupeana talaka.