ARUSHA: ZAHANATI yenye gharama ya zaidi ya Sh milioni 180 inajengwa ndani ya ukuta wa migodi ya madini ya Tanzanite iliyopo katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani mkoani Arusha.
Lengo ni kuwazogezea huduma ya matibabu wachimbaji na tiba za huduma ya kwanza za ajali migodini.
Zahanati hiyo inajengwa na Kampuni ya Franone Mining inayomilikiwa na Mkurugenzi Mtendaji Onesmo Mbise na inachimba mgodi wa Kitalu C kwa ubia na serikali.
Akizungumza baada ya kukagua zahanati hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala aliipongeza kampuni hiyo na kusema kujengwa kwa zahanati hiyo mpango wa kupitia uwajibikaji kwa jamii (CSR), na ameipongeza kampuni ya Franone na wakurugenzi wake.
Ameeleza kwamba zahanati hiyo itakamilika baada ya miezi mitatu, wadau wa madini ya Tanzanite wa eneo hilo watapatiwa huduma za afya kwa urahisi baada ya kupangiwa wataalamu wa afya wenye sifa stahiki kuwahudumia wagonjwa.

Alisema changamoto ya ukosefu wa huduma ya afya kwenye eneo hilo ni ya muda mrefu ila baada ya kukamilika kwake wachimbaji watapata huduma ya afya karibu na kuacha kusafiri mrefu wa kwenda Moshi na Arusha kusaka tiba.
“Franone wametuwahi tuu kwani serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ilikuwa na lengo la kujenga zahanati huku migodini lakini sio mbaya kwani hayo yote ni matunda ya serikali katika uwekezaji,” alisema Lulandala.
Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa Franone,Vitus Ndakize amesema wanajenga zahanati hiyo kwa lengo la kuhudumia jamii kupitia CSR na ujenzi wake umefikia asilimia 50 na utakamilika ndani ya miezi mitatu ijayo na wachimbaji watafurahi huduma ya matibabu katika zahanati hiyo.

Ndakize amesema pamoja na kuwa wamesaidia jamii kupitia miradi mbalimbali ya CSR ya eneo hilo wameona kwa wakati huu ni vyema wakajenga zahanati ili kusaidia wachimbaji kwa upande wa afya.
Mhandisi wa Majengo wa Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Grace Munuo ameeleza kwamba huwa wanakagua ujenzi unavyoendelea na endapo kukilazimika kufanyika kwa marekebisho wanaelekeza na kufanywa hivyo lengo ni kutaka ujenzi wa zahanati hiyo kuwa bora.
Wadau wa madini ya Tanzanite wa kitalu D na kitalu B wameipongeza kampuni ya Franone kwa hatua hiyo kwani katika migodi ya Tanzanite hawana hospitai, kituo cha afya wala zahanati katika eneo hilo, hivyo wanawashukuru wakurugenzi wa Franone kwa kujenga zahanati hiyo na uamuzi huo unapaswa kupongezwa.