Tunduru. Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Kaskazini wamemuomba Mbunge wa jimbo hilo, Ado Shaibu kuwasaidia kupata daraja katika Mto Mlingotini ili kuwanusuru watoto wao wanaosoma katika shule za msingi Nakayaya na  Muungano.

Ombi hilo limetolewa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Baraza la Iddi, leo Jumapili, Februari 22, 2026. Akizungumza kwa niaba ya wananchi, mkazi wa Kata ya Kigamboni, Zaituni Omary amesema watoto hao hupata shida kuvuka mto huo wakati wa mvua, hali inayosababisha baadhi yao kusombwa na maji.

Ameiomba Serikali kupitia mbunge huyo kuchukua hatua za haraka kwa kujenga daraja katika Mto Mlingotini ili watoto waweze kufika shuleni kwa usalama na bila changamoto yoyote.

“Mheshimiwa Mbunge, tunakuomba utusaidie kutujengea daraja katika Mto Mlingotini ili watoto wetu waweze kwenda shule bila changamoto. Shule ya Msingi Nakayaya na Muungano zipo upande wa pili wa mto, hivyo watoto wanaoishi Kigamboni hulazimika kuvuka kufuata masomo,” amesema Omary.

Akijibu hoja hiyo,  Ado Shaibu amesema zaidi ya Sh70 milioni zimetengwa katika Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Amesema fedha hizo zitatumika kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Wananchi wa Tunduru wakimsikiza mbunge wa jimbo hilo kwenye mkutano wa hadhara uliyofanyika kwenye viwanja vya baraza la iddi, Halmshauri ya Tunduru.

“Mimi mabosi zangu ni watu wa Tunduru Kaskazini. Mkiniambia nifanye hivi nafanya, mkiniambia nisifanye sifanyi. Fedha za Mfuko wa Jimbo zimetolewa na zipo tayari; nitazipeleka kwenye miradi ya maendeleo nanyi mtakuwa mashahidi. Pia sitasahau wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mikopo,” amesema Shaibu.

Aidha, amewahakikishia waendesha pikipiki ‘bodaboda’ kuwa watapatiwa mikopo ya pikipiki waweze kujipatia kipato na kuboresha maisha yao.

Mbunge huyo pia ameahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wake, hususan tatizo la maji na umeme ambalo amesema limekuwa kero kwa muda mrefu.

“Natambua kuwa maji na umeme ni tatizo kubwa katika mji wetu. Nitajitahidi kuwapambania mabosi zangu ili kurudisha heshima ya Tunduru yetu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *