
Dar es Salaam. Wakati Neema Mashimba, mtoto wa aliyekuwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Ernest Mashimba akiiomba Serikali kuingilia kati eneo lao lililotwaliwa na mfanyabiashara, Ally Rubea kwa madai amepangishwa kwa miaka 99, mlalamikiwa mwenyewe amejibu akisema aliuziwa eneo husika.
Akielezea hali ilivyokuwa, Neema amesema baada ya Rubea kuingia kwenye eneo lao lililopo Ploti Na 9 Ursino Estate Msasani Wilaya ya Kinondoni, kama mpangaji alibomoa nyuma yao na kufanya maegesho ya magari.
Kufuatia madai hayo, Mwananchi ilimtafuta Rubea ambaye amesema ukweli kwenye jambo hilo unapotoshwa kwani aliuziwa eneo hilo na familia baada ya kutangazwa kupitia madalali.
“Jambo hili lilikuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama Kuu, tuna uamuzi wa mahakama zote, nia ya kwanza kwenye ardhi ile ilikuwa ni kununua, mke wa marehemu alitangaza kuuza nyumba ile kupitia madalali niliingia huo mtego nikakubaliana na huyo mama kununua ardhi ile.
“Katika kubadilisha hati tulikwama kwa sababu nyumba ile ilitakiwa kubadilishwa majina baada ya miaka 25, yote haya yalifanywa na mwanasheria wa mama husika, sasa baada ya huo mkwamo tukakubaliana kuingia mkataba wa miaka 99,” amesema.
Rubea amesema walikubaliana na mama huyo kuuziana nyumba hiyo na sio kupangishiana kama inavyoelezwa.
Amesema mama huyo alipatiwa nyumba mbili eneo la magomeni yenye thamani ya Sh420 milioni, viwanja viwili, gari aina ya prado pamoja na Sh200 milioni ambazo alizipokea zote kwa njia mkataba.
Madai ya mlalamikaji
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumapili Februari 22, 2026 kuhusu sakata hilo, Neema amesema baada ya baba yao kufariki 2010 kulikuwa na msimamizi wa mirathi ambaye alikabidhiwa mali kuzitunza kwa niaba yao.
Amesema mwaka 2021 walikabidhiwa mali na Msajili wa hati Mkoa wa Dar es Salaam, Bakari Rajabu kama wamiliki halali yeye na Suzana Mashimba baada ya suala la mirathi kukoma.
“Tulipatiwa hati ya umiliki namba 58933, Ally Rubea anasema ana mkataba alioingia na msimamizi wa mirathi kwa miaka 99 tangu 2012 sisi ndio wamiliki na hatuna tena msimamizi wa mirathi.
“Upo ujanja tena Rubea ameufanya badala sisi tutambulike ndio wamiliki wa ardhi tunaitwa tena wasimamizi wa mirathi, tunaomba Serikali itusaidie kupata haki yetu,”amesema.
Kwa upande wake wakili aliyejitolea kumsaidia mtoto huyo, Peter Madeleka amesema Rubea anapaswa kuwafuata alioandikishana nao mkataba wa kukaa kwenye ardhi hiyo kwa muda anaoutaja.
Amesema msimamizi wa mirathi sio mmiliki wa eneo husika akidai hakuna msimamizi wa mirathi ambaye anapokea fedha kutoka kwa Rubea.
Mirathi ilivyokuwa
Madeleka amesema baada ya Mashimba kufariki dunia mirathi namba 425 ya mwaka 2010 ilifunguliwa Mahakama ya Mwanzo Kinondoni Dar es Salaam ambapo mke wa marehemu Rose Mashimba, Happines Mashimba na Goodluck Mashimba ambao ni watoto wa marehemu waliteuliwa kuwa wasimamizi wa mali hizo.
“Uteuzi wa wasimamizi wa mirathi ulifanyika mwaka 2010 na shauri lilidumu mahakamani kwa miaka 11 na lilifungwa rasmi Julai 30,2021 na warithi wakagawiwa mali kama ilivyoorodheshwa,”amesema
Amesema nyumba iliyopo Kinondoni waligawiwa watoto wa marehemu Neema na Suzana na mahakama ilitoa haki kwa wasimamizi wa mirathi kubadili hati ya umiliki wa nyumba iliyokuwepo kwenye kiwanja hicho kwenda kwa wamiliki wapya.
Baada ya kiwanja hicho kubadilishwa, Madeleka amesema wamiliki wapya walitajwa kuwa ni Rose Mashimba mke wa marehemu, Happyness na Goodluck Mashimba watoto wa marehemu.
“Wakati wasimamizi wakiendelea na shughuli zao akaibuka mtu anaitwa Ally Rubea ambaye alikuwa jirani yao alikwenda kupanga nyumba hiyo na wasimamizi wa mirathi, mkataba wake ni kulipa Sh1.5 milioni kwa mwezi,”amesema.
Madeleka amesema baada ya kupangishwa nyumba hiyo, mwaka 2013 Rubea alikwenda kuomba ruhusu ya kuibomoa wakati yeye sio mmiliki wa nyumba hiyo huku suala la mirathi likiwa linaendelea mahakamani.
“Mwaka 2021 mirathi ilipokoma na umiliki halali wa nyumba ile ulikuwa chini watoto wa marehemu, mpangaji (Rubea) kwa mara nyingine alikula njama na kuwabadili wamiliki kuwa wasimamizi wa mirathi,”amesema.
Madeleka ameeleza lengo la kufanya hiyo kwa mpangaji huyo, ni mkataba wake anaodai alipangishwa na wasimamizi wa mirathi uendelee kuwa na nguvu.
Amesema kuanzia 2021 watoto hao walipopewa umiliki wa mali zao na walianza kulipia serikalini kodi hadi 2023 walipoambiwa wao ni wasimamizi wa mirathi na sio wamiliki.
Kufuatia hali hiyo, Madeleka amempa siku 14 Rubea kuliachilia eneo hilo kwani hakuna mkataba wa namna hiyo na hakuna mtu aliyewahi kumlipa kodi yake.