Dar es Salaam. Salehe Jinga, maarufu kwa jina la utani Karosi, amefariki dunia baada ya kuigonga  treni ya abiria katika eneo la Tabata Mwananchi jijini Dar es Salaam.

Ajali hiyo imetokea saa moja asubuhi ya leo Jumatatu, Februari 23, 2026, wakati marehemu aliyekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 40 hadi 50 akivuka reli huku treni ya abiria ikitokea Mabibo kuelekea Buguruni.

Kwa mujibu wa mashuhuda, treni hiyo lilikuwa likipiga honi mfululizo kumuonya, lakini aliendelea kuvuka reli kabla ya kuigonga na kuburuzwa umbali wa futi kadhaa, na kufariki dunia papo hapo kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata.

Mama mmoja anayefanya biashara ya chakula eneo hilo amesema alishuhudia tukio hilo kwa macho yake.

“Nimemwona akivuka reli huku treni ikipiga honi sana. Ilikuwa karibu kabisa naye, ghafla akaigonga na kumburuzwa. Mwili wake umevunjika vibaya, viungo mbalimbali vimetengana na kupoteza maisha papo hapo,” amesema shuhuda huyo.

Taarifa zilizothibitishwa na wafanyakazi wenzake zinaeleza kuwa marehemu alikuwa mkazi wa Buguruni na mfanyakazi wa Kampuni ya Oilcom iliyopo jirani na eneo la tukio.

“Ni mfanyakazi mwenzetu Oilcom, anaitwa Salehe Jinga, maarufu Karosi, anakaa Buguruni. Ameigonga, maaskari wa TRC (Shirika la Reli Tanzania), wakashuka wakaja kumuangalia kisha wakaondoka wakisema wanashughulikia,” amesema mmoja wa wafanyakazi wenzake ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Mwandishi wa Mwananchi aliyefika eneo la tukio ameshuhudia mwili wa marehemu ukiwa kando ya reli umefunikwa kwa nguo huku wananchi wakijikusanya kuzunguka eneo hilo.

Tayari, askari wa Jeshi la Polisi wamefika katika eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *