KIKOSI cha Simba kimecheza mechi saba mfululizo za mashindano bila kupoteza, kitendo hicho kimemfanya kocha mkuu, Steve Barker kupata tumaini jipya Msimbazi, akisema hali ya kujiamini kwa wachezaji inazidi kuimarika kila uchao, japo kuna jambo analifanyia kazi zaidi ili wakae sawa akisisitiza ni eneo la ushambuliaji.
Juzi usiku Simba ilipata ushindi wa saba msimu huu katika Ligi ikiilaza Tanzania Prisons kwa mabao 2-0 na kufikisha pointi 22 ikishika nafsi ya nne katika msimamo, lakini ni kama vile kocha Barker hajaridhika nayo, licha ya kuona mwanga kulinganisha na mechi zilizopita.
Kocha huyo alisema licha ya ushindi huo unaendeleza rekodi ya kucheza mechi saba mfululuzo kwa mashindano yote bil kupoteza, lakini amewataka washambuliaji kuongeza makali katika kutumia nafasi wanazoitengeneza.
Mabao ya Seleman Mwalimu ‘Gomez’ na Rushine De Reuck yalitosha kuifanya Simba kushinda mechi ya tatu mfululizo katika ligi hiyo na kufikisha jumla ya pointi 22 ikishika nafasi ya nne ikishuka uwanjani mara tisa, imeshinda mechi saba, sare moja na kuchapwa mara moja.
Ushindi huo wa juzi unaifanya Simba kucheza mechi saba mfululizo za mashindano tofauti bila ya kupoteza kwani tangu mara ya mwisho Januari 25, 2026 kufungwa 1-0 ugenini dhidi ya Esperance katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imekuja kushinda tano na sare mbili. Katika mechi ilizoshinda, haijaruhusu nyavu zake kutikiswa.
Akizungumza na Mwanaspoti, wakati akikiandaa kikosi hicho kwa ajili ya mechi ijayo ya ligi dhidi ya Dodoma Jiji itakayochezwa kesho Jumatano, Barker alisema: “Nimefurahishwa na ushindi (dhidi ya Prisons) lakini ukweli ni kwamba tunatengeneza nafasi nyingi na hatuzitumii ipasavyo. Lazima tuwe na makali zaidi mbele ya lango, napenda kumaliza mechi mapema.”
Kocha huyo aliongeza: “Timu inaendelea kuimarika na ninaamini tutaendelea kufanya vizuri zaidi ya sasa, nina furaha kuona vijana wakipambana kila mmoja katika nafasi yake, akionyesha vile anaweza kuwa msaada kwa timu.”
Barker alisema katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons, kulikuwa na nafasi kadhaa za wazi ambazo walishindwa kuzitumia.
Kwa mujibu wa kocha huyo, tofauti ya mabao inaweza kuwa na uzito mkubwa mwishoni mwa msimu, hasa katika ligi yenye ushindani kama Tanzania Bara.
“Wakati mwingine ubingwa unaamuliwa kwa tofauti ya mabao, hivyo hatupaswi kuridhika na ushindi wa bao moja au mawili kama kunakuwa na nafasi za kufunga zaidi,” alisema.
Kwa pamoja washambuliaji wa kati wa Simba, Mwalimu (4) na Jonathan Sowah (3) wamefunga jumla ya mabao saba kati ya 18 yaliyofungwa na timu hiyo katika ligi, sawa na mchango wa asilimia 38.
Mbali na hilo, Barker aliwapongeza wachezaji kwa kujituma na kuonyesha nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya uwanja.
“Nina kikosi chenye morali nzuri na kwa sasa ukitazama hata wachezaji wapya wameanza kuzoeana na wenzao, niwe mkweli kila mmoja katika timu anaonyesha njaa ya ushindi na hilo linanipa matumaini na kuona tupo katika mwelekeo sahihi,” alisema Barker.
Simba sasa inajiandaa kuivaa Dodoma Jiji, ikijua kuwa ushindi mwingine utawaweka katika nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo wa ligi kabla ya kukutana na watani zao, Yanga kwenye Dabi ya Kariakoo, Machi Mosi mwaka huu.
Katika mechi saba mfululizo ambazo Simba imecheza bila ya kupoteza, imezifunga Mashujaa (2-0), KMC (2-0) na Tanzania Prisons 2-0 (zote za Ligi Kuu). Pia ikashinda 1-0 dhidi ya Stade Malien katika Ligi ya Mabingwa na ushindi wa 3-0 mbele ya Green Land kunako Kombe la Shirikisho (FA), huku ikitoka sare dhidi ya Esperance (2-2) na Petro Atletico (1-1) zote za Ligi ya Mabingwa.