
WAKATI ikijiandaa kwa ajili ya mechi za duru la pili la Ligi Kuu Bara, kocha mkuu wa Coastal Union, Mohammed Muya amesema ‘Wagosi wa Kaya wameimarika’ na wapo tayari kwa vita ya ngwe ya lala salama ya ligi hiyo inayotoa bingwa na wawakilishi wa nchi katika michuano ya CAF.
Coastal inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Singida Black Stars katika mechi itakayopigwa Machi 2, ikiwa ni ya 16 kwao na ya 11 kwa wageni waliotoka kushiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Muya amesema wamepata mapumziko yaliyosaidia kusawazisha makosa na kuongeza ubora kwa wachezaji wa timu hiyo ambao juzi walipata nafasi ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Nkim FC na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 ikiwa ni sehemu ya maandalizi.
Muya amesema baada ya kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB na kupata ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Nyumbu, hawatacheza mechi nyingine hadi Jumatatu ijayo na badala yake atatumia muda uliosalia kurekebisha dosari zilizojitokeza katika mechi zilizopita kwa ajili ya kujiweka fiti kuikabili Singida.
“Tumefanyia kazi mambo mbalimbali, kila unapofanya mazoezi, unapata nafasi ya kuelekeza mbinu mpya, tuseme mapumziko tuliyoyapata yamekuwa na tafsiri chanya upande wetu, yametusaidia kujiimarisha, sasa tuko tayari kuendelea na mapambano,” amesema Muya.
Akizungumzia mechi hiyo ijayo, Muya amesema wamejipanga kurejesha furaha kwa mashabiki wao na kupambania pointi muhimu kwenye kila mchezo ili waweze kumaliza msimu wakiwa katika nafasi nzuri na kujihakikishia kucheza ligi msimu ujao.
Muya amesema wachezaji wote wamejiandaa kukutana na ushindani katika hatua hiyo ya pili kwa sababu kila upande unahitaji kutimiza malengo yake na wao hawataki kufanya makosa.
“Hatukuwa na mwendelezo mzuri mzunguko wa kwanza kwenye mechi 15 tulizocheza hadi sasa, tumepitia wakati mgumu, lakini sasa tunaahidi kurejea kwa furaha, tunajua haitakuwa rahisi, lakini tuko tayari kuipambania timu yetu na hatimaye kufikia malengo.”
Coastal yenye pointi 15 iko katika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, imeshinda mechi tatu, sare sita na kupoteza sita pia ikiwa imeshuka uwanjani mara 15, huku ikifunga mabao 12 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 17.