SIKU chache zilizopita, kocha mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amesema hafurahishwi na namna wachezaji anaowapa nafasi ya kucheza kisha wanashindwa kuonyesha kupambana kwao huku akiwataka kuacha kuridhika.
Hiyo ilikuwa baada ya kushinda 2-0 dhidi ya Cosmopolitan katika hatua ya 64 ya Kombe la Shirikisho (FA).
Lakini sasa baada ya ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Namungo, Pedro amekuja na jipya akilia na washambuliaji kushindwa kutumia nafasi licha ya kutengeneza na kutawala mchezo huku akimtaja Allan Okello.
Yanga juzi ilikuwa ugenini ikicheza dhidi ya Namungo katika mechi ya Ligi Kuu kwa kupata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Laurindo Aurelio ‘Depu’ kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi likiwa ni bao lake la nne kupitia mechi tatu za Ligi alizocheza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro alisema anashukuru wamepata pointi tatu kama mipango yao ilivyokuwa, lakini hajaridhishwa na utumiaji wa nafasi kwa safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, huku akimtaja Okello kuwa, licha ya kufanya kazi kubwa ya kukimbia eneo kubwa la uwanja na kutengeneza nafasi nyingi, alishindwa kufunga.
“Haukuwa mchezo rahisi, tumekutana na timu nzuri ambayo benchi lilikuwa na mbinu nzuri pia, lakini mchezo ulikuwa wazi zaidi upande wetu, wachezaji walijitahidi kufika mara kwa mara lango la wapinzani lakini walishindwa kutumia nafasi,” alisema Pedro raia wa Ureno na kufafanua;
“Shida hii haijaanza jana (juzi), ipo na nimekuwa nikiifanyia kazi, sitaacha kufanya hivyo, nitaendelea mara kwa mara, naamini itafanya kazi kwenye mechi zilizo mbele yetu. Mfano Okello alikuwa bora sana akikimbia eneo kubwa la uwanja na kutengeneza nafasi nyingi lakini ameshindwa kuzifanya yakawa mabao.”
Pedro alisema ushindi walioupata umeongeza morali kwa ajili ya mechi zilizo mbele yao, lakini bado ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha nafasi zinazotengenezwa zinazaa mabao, kwani katika kupambania kutetea taji lao, lazima wawe imara kila idara hasa katika ufungaji mabao ya kutosha.
“Ushindani ni mkubwa, mabao mengi yanaweza kutupa taji kulingana na idadi ya pointi tunazokusanya katika kila mchezo, hivyo ili tuwe bora na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea mataji tunatakiwa kushinda kwa idadi kubwa ya mabao,” alisema Pedro.
Akizungumzia mechi ya kesho Jumatano dhidi ya JKT Tanania kwenye Uwanja wa KMC Complex, Pedro alisema hautakuwa rahisim, kwani wanakutana na timu bora yenye uwezo mkubwa wa kutumia nafasi, pia inaongoza msimamo wa Ligi, hivyo wanahitaji kuwa bora ili kuchukua pointi tatu dhidi yao ili irejee kilele kabla ya Dabi ya Karikoo itakyopigwa Jumapili hii huko Zanzibar.
“Tunakutana na mshindani mkubwa ambaye amefanya kazi nzuri hadi amesimama wa kwanza kwenye msimamo, mbinu bora na wachezaji bora ndio watakaoamua hatma ya kuongoza ligi kwani naamini tukipata matokeo dhidi ya mpinzani huyo tunaweza kuongoza ligi kwa idadi ya mabao jambo ambalo nimetoka kulizungumza kuwa ni muhimu,” alisema Pedro na kuongeza;
“Kucheza na mpinzani bora inaongeza ubora kwa wachezaji na mbinu baina ya benchi na benchi, natarajia mchezo mzuri na wa ushindani kutoka kwa wapinzani wetu, nina kazi ya kufanya kusawazisha makosa kabla ya kuivaa timu hiyo.”
Yanga inayoshikilia taji la Ligi Kuu kwa msimu wa nne mfululizo kwa sasa ipo nafasi ya pili katika msimamom, ikikusanya jumla ya pointi 25 baada ya kucheza mechi tisa, ikishinda nane na kutoka sare moja na kesho itaikaribisha JKT Tanzania inayoongoza msimamo ikiwa na pointi 28.
Katika mechi za msimu uliopita za Ligi, Yanga ilishinda mechi moja na nyingine iliyokuwa ya kwanza ikiisha kwa suluhu kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.