MAAFANDE wa Polisi Tanzania, wamevunja rekodi ya Geita Gold ya kutopoteza mchezo wowote (Unbeaten) katika Ligi ya Championship msimu huu baada ya jana Februari 22, 2026 kuichapa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Ushirika uliopo Moshi mkoani Kilimanjaro.
Ushindi huo umehitimisha mwendo wa Geita Gold iliyokuwa haijapoteza tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi ya Championship 2025-2026.
Bao la kwanza lilifungwa na Jamal Mtegeta dakika ya 19 akimalizia shambulizi la haraka, kisha Tariq Kiakala aliongeza la pili dakika ya 64 na kuipa Polisi alama tatu uwanja wa nyumbani.
Kabla ya kipigo hicho, Geita Gold ilikuwa kinara katika Ligi ya Championship ikicheza mechi 18 bila kupoteza, ikishinda 14 na sare nne, ikijikusanyia alama 46 kileleni mwa msimamo.
Sare ilizopata Geita ni dhidi ya Kagera Sugar (1-1), KenGold (2-2) na Transit Camp (1-1) ikiwa nyumbani Uwanja wa Nyankumbu, pamoja na sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Bigman FC iliyochezwa Uwanja wa Ilulu, Lindi.
Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana, ilikuwa Novemba 8, 2025 kwenye Uwanja wa Nyankumbu katika mzunguko wa kwanza wa Ligi ya Championship ambapo Geita Gold ilishinda mabao 2-0 yaliyofungwa na Maulid Shabani dakika ya 49 na Yusuf Muhilu dakika ya 56.
Katika mechi ya jana, Polisi Tanzania iliingia uwanjani ikiwa na morali kubwa baada ya kutoka kuifunga Stand United ‘Chama la Wana’ mabao 2-0, kwenye Uwanja wa Ushirika, huku Geita Gold ikitoka kushinda 2-1 dhidi ya Mbeya Kwanza.
Mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza Geita Gold ilipoteza penati baada ya nahodha wake, Ali Ali kushindwa kuuweka mkwaju wake wavuni kutokana na kosa la mchezaji mmoja wa Polisi Tanzania kuushika mpira katika harakati za kuokoa hatari.
Geita Gold iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024 kutoka Ligi Kuu Bara, ilimaliza nafasi ya nne kwenye Ligi ya Championship msimu uliopita 2024-2025 ikiwa na pointi 56 chini ya Kocha Mkuu, Mohamed Muya, lakini ikashindwa kupanda Ligi Kuu Bara baada ya kuondoshwa kwenye mechi za mchujo ‘Play off’
Katika ‘playoff’ hiyo, Geita ilitolewa na Stand United kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare ya 2-2 nyumbani na kupoteza 2-0 ugenini.
Kwa upande wa Polisi Tanzania, msimu wa 2024-2025 haukuwa mzuri baada ya kumaliza Ligi ya Championship nafasi ya 10 kwa pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13, huku ikifunga mabao 44 na kuruhusu 33. Timu hiyo inasaka kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2022-2023.
Akizungumza baada ya mechi, Kocha wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata, alisema ushindi huo umeongeza morali kwa kikosi chake kuelekea mchezo ujao wa ugenini dhidi ya Bigman FC kabla ya kuikaribisha Kagera Sugar.
“Tumeweza kuwazuia Geita kucheza kwa uhuru wao. Ushindi huu na ule wa mechi iliyopita umetupa kujiamini kuelekea malengo yetu,” alisema Makata.
Kocha Mkuu wa Geita Gold, Zuberi Katwila, alisema wamejifunza kutokana na matokeo hayo na sasa wanaelekeza nguvu katika maandalizi ya mechi ijayo ugenini dhidi ya Gunners.
Katika msimamo wa Ligi ya Championship, Kagera Sugar inaongoza ikiwa na pointi 46, sawa na Geita Gold iliyo nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao. Nafasi ya tatu inashikiliwa na Mbeya Kwanza yenye pointi 41, ikifuatiwa na Transit Camp iliyo ya nne kwa pointi 37, huku Polisi Tanzania ikibaki nafasi ya tano na pointi 36.
Mbio za kuwania kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao 2026-2027 zimezidi kunoga baada ya Ligi ya Championship kuendelea wikiendi iliyopita ambapo jana Jumapili zimepigwa mechi saba na moja ikitarajiwa kupigwa leo Jumatatu kuhitimisha raundi ya 19.