Utekelezaji wa mradi wa kusambaza gesi asili katika eneo la Kisemvule, wilayani Mkuranga mkoani Pwani, umeendelea kuibua matumaini mapya kwa Wananchi wa eneo hilo ambapo zaidi ya shilingi bilioni 6.8 zimewekezwa katika kusambaza gesi asilia katika maeneo yaliyopitiwa na mkuza wa bomba la gesi asilia.
Mradi huo umejengwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kufadhiliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia.
Akizungumza baada ya kutembelea na kukagua Mradi huo; Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu, amesema utekelezaji wa Mradi huo unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuboresha maisha ya Wananchi na kulinda mazingira.
Amesema Bodi ya Nishati Vijijini inajivunia kuona mwitikio mkubwa wa Wananchi wanaene kuhamasika kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia gesi asili, ambayo ni salama, nafuu na rafiki kwa mazingira.
“Huu ni Mradi wa kimkakati unaotekeleza maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuona Watanzania wengi wanatumia nishati safi, tunapaswa kulinda miundombinu hii kwa kuwa imegharimu fedha nyingi za Serikali,” amesema Balozi Kingu.
Kwa mujibu wa REA, mradi huo wa mfano ulilenga kuhudumia kaya 2,000 huku hadi sasa kaya 530 zikiwa zimefikiwa na huduma hiyo katika eneo la Kisemvule lenye wakazi zaidi ya 64,000 hali inayotoa fursa ya kupanua zaidi wigo wa huduma hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi, Hassan Saidy amesema taasisi hiyo imeiomba TPDC kufanya tathmini katika maeneo yenye idadi kubwa ya watu ambako bomba la gesi limepita ili kuanzisha miradi ya ubia itakayowezesha wananchi wengi zaidi kuunganishwa na huduma hiyo.
(Feed generated with FetchRSS)