
Arusha. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa amesema mafanikio ya benki ni kujenga mazingira wezeshi ya kuwafikia wananchi waliosahaulika katika huduma za kifedha kwa kuwapa elimu sahihi ya kifedha na kunufaika na mikopo kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Amesema hayo leo Jumanne, Februari 24, 2026 wakati akifungua tawi la Benki ya Maendeleo jijini Arusha ambalo ni tawi la sita na la kwanza kufunguliwa nje ya Mkoa wa Dar es Salaam tangu kuanzishwa kwake mwaka 2013.
Askofu Malasusa amesema licha ya kuwa benki hiyo ni mali ya KKKT lakini inawahudumia watu wote bila kujali itikadi zao za kiimani kwa sababu wajibu wa kanisa ni kutoa huduma za kiroho na kimwili kwa watu wote.
“Benki ya Maendeleo inao uzoefu sana kwa wananchi waliosahaulika katika huduma za kifedha, imefanya kazi na makundi ya waendesha bodaboda, mama lishe na hivyo tutaendelea kuwajumuisha kwenye masuala ya kifedha na ndio sera na dira yetu.
“Kinachokosekana hapo ni elimu ya kifedha, watu wengi hawajajifunza juu fedha, wanazo lakini hawajui wazitumieje wengine wanao muda lakini hawajui wautumieje na wanafanya biashara na mambo mengi, nitoe wito kwa Benki ya Maendeleo kuwakumbuka hawa ambao hawajafikiwa na huduma za kifedha,” amesema Askofu Malasusa.
Amewataka wafanyakazi wa benki hiyo na taasisi zingine za kanisa hilo kuwa waaminifu kwenye kazi wanayoifanya kuwahudumia wananchi, licha ya kuwa taasisi hiyo ipo kwenye ushindani na taasisi zingine za kifedha na kusisitiza uaminifu na uadilifu na kufanya kazi kwa kumtegemea Mungu.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo, Lomnyaki Saitabau amesema benki hiyo imeorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ikiwa ni benki ya kwanza ya ndani kuorodheshwa katika soko hilo, ilianza na mtaji wa mali za Sh4 bilioni na sasa ina jumla ya mtaji wa Sh.26.6 bilioni na mali ya Sh.202.5 bilioni, kwa hesabu za kabla ya ukaguzi wa mwaka 2025.
Mkurugenzi huyo amesema mpango mkakati wa mwaka 2025 hadi 2030 ni kuunda benki imara, bunifu na jumuishi, kufikia mali zenye thamani ya Sh500 bilioni na kuwezesha ukuaji endelevu kwa wateja, wanahisa na wafanyakazi.
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Godson Mollel amesema kufunguliwa kwa tawi hilo jijini Arusha kunaonyesha ukuaji wa benki hiyo nchini na kutambua Mkoa wa Arusha ndio uliokua wa kwanza kuanzishwa kwa dayosisi wakati huo ikiitwa Sinodi.
“Mkoa wa Arusha umepokea tawi hili kwa heshima kubwa na nitoe wito kwa wakuu wote wa majimbo pamoja na taasisi zote zilizo chini ya KKKT kufungua akaunti kwenye benki hii, ambayo inafanya kazi kwa uadilifu na inayokua kwa kasi,” amesema Dk Mollel.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Benki ya Maendeleo, Anna Mzinga amesema kufunguliwa kwa tawi hilo ni ushahidi wa utekelezaji wa mpango mkakati wa benki hiyo wa mwaka 2025 hadi 2030 unaolenga kuimarisha huduma zao na kupanua wigo wa kifedha na kuwa karibu na wateja wao.