Dar es Salaam. Kwa kiwango anachokionesha mshambuliaji wa Namungo, Fabrice Wa Ngoy ni dhahiri kabisa upepo umembadilikia nyota huyo ndani ya kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’ kinachonorewa na kocha Juma Mgunda. Ngoy alijiunga na Namungo msimu wa 2023/2024 akitoka Kitayosce iliyobadilishwa jina na kuitwa Tabora United na sasa TRA United.

Mshambuliaji huyo alitua nchini kwa mara ya kwanza msimu wa 2022-2023, akitokea Real Nakonde FC ya Zambia na msimu uliopita wa 2024-2025, akiwa na kikosi hicho cha Namungo alifunga mabao mawili ya Ligi Kuu Bara. Hata hivyo, msimu huu umeonekana kumwendea tofauti mshambuliaji huyu ambaye hadi sasa ameonyesha kiwango cha hali ya juu tofauti na msimu uliopita.

Hadi sasa amehusika na pointi 14 kati ya 19 alizoivunia Namungo katika Ligi Kuu Bara, Ngoy alisema mafanikio ya ubora yanatokana na kuamini katika kujaribu na ushirikiano uliopo kati yake na wenzake. Nyota huyu wa Kimataifa kutokea DR Congo, amefunga mabao saba kwenye Ligi Kuu akiwa ndiye kinara wa upachikaji mabao kwa sasa akimshusha Saleh Karabaka wa JKT Tanzania.

Ngoy ameandika rekodi ya kufunga mabao muhimu kwa Namungo ambayo yamezalisha pointi 14 kati ya 19 ilizokusanya timu hiyo. Mechi alizofunga ni dhidi ya Tanzania Prisons (1-0, pointi 3), Azam FC (1-1, pointi 1), Mbeya City (1-0, pointi 3), Coastal Union (1-0, pointi 3), KMC (1-0, pointi 3), Fountain Gate (1-1, pointi 1) na Tanzania Prison waliyopoteza kwa kichapo cha 3-2 wakitoka bila pointi huku yeye akitupia bao moja.

Kocha wa Namungo, Juma Mgunda (kushoto), kulia ni mshambuliaji, Fabrice Ngoy wakati alipokuwa akipatiwa maelekezo katika moja ya michezo ya Ligi Kuu. Picha na Namungo

Akizungumza kuhusu ubora wake, Ngoy amesema hawezi kuwa bora bila wachezaji wenzake 10 uwanjani, hivyo anaamini ushirikiano mzuri walionao ndio siri ya mafanikio wanayoyapata chini ya kocha Juma Mgunda.

“Najivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya timu yangu. Nitapambana hadi mwisho kuhakikisha tunafikia malengo. Namshukuru kocha Mgunda kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kucheza mbele ya wachezaji wengine bora waliopo Namungo.

“Natumia fursa hii kuonyesha kuwa nafasi ninayopewa nastahili, lakini pia napambania timu iweze kufikia malengo kwa kujaribu kutumia kila nafasi ninazotengenezewa. Lengo ni kuona tunakwepa changamoto ya kushuka daraja au kumaliza katika nafasi mbaya kwenye msimamo,” alisema Ngoy.

Akizungumzia ligi kwa ujumla na mpango wake msimu huu katika kufumania nyavu, Ngoy alisema atafunga kila atakapopata nafasi na hayupo tayari kuweka idadi ya mabao atakayofunga, kwani anaweza kuvuka idadi atakayotaja au akashindwa kufikia.

“Kufunga siyo bahati, ni kutumia nafasi. Hivyo sipo tayari kutaja ni idadi gani ya mabao natamani kufunga msimu huu. Ahadi yangu ni kufunga kila nitakapopata nafasi ili kuisaidia timu kufikia malengo.

“Ligi ni ngumu sana msimu huu, timu zimejipanga kutokana na sajili zilizofanywa, hivyo mikakati sahihi ya wachezaji na benchi la ufundi ndio itakayotufanya tuweze kufikia malengo. Nitapambana kwa kushirikiana na wenzangu kuhakikisha Namungo inakuwa bora na timu tishio msimu huu,” alisema mshambuliaji huyo.

Mshambuliaji wa Namungo, Herieter Makambo, ambaye pia amewahi kuzichezea Yanga na TRA United (zamani Tabora United). Picha na Namungo FC

MAKAMBO ANAVYOMPIGA TAFU

Ngoy alisema kucheza timu moja na mshambuliaji mwenzake raia wa DR Congo, Heritier Makambo kunampa motisha kuhakikisha anaendelea kupambana katika kikosi cha kwanza, kila anapopata nafasi uwanjani.

Kauli ya nyota huyo inajiri baada ya kuongezewa washambuliaji wengine akiwemo Makambo aliyewahi kuichezea Yanga na msimu uliopita alicheza Tabora United (kwa sasa TRA United) na kuifungia mabao matano ya Ligi Kuu Bara.

“Makambo ni kaka yangu ambaye kila siku najifunza kutoka kwake, msimu huu ni mgumu kuanzia ushindani wa Ligi Kuu Bara na hata wachezaji wenyewe, kwangu inanipa motisha ya kupambana kila ninapopata nafasi uwanjani,” alisema Ngoy.

Uongozi wa Namungo pia ulimwongeza aliyekuwa mshambuliaji wa TMA ya Arusha, Abdulaziz Shahame ‘Haaland’, ambaye msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Championship akiwa na mabao 18.

Idadi hiyo ya mabao 18 aliyofunga Shahame anayefananishwa na mshambuliaji wa Klabu ya Manchester City ya England, Erling Braut Haaland, ni sawa pia na ya nyota wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh na Andrew Simchimba aliyekuwa anacheza Geita Gold.

Mshambuliaji wa Namungo, Fabrice Wa Ngoy. Picha na Namungo FC

ALIVYOIBUKIA KWENYE SOKA

Kila mchezaji huwa na historia yake katika soka, kwa ujumla wengi tumezoea kusikia wachezaji wengi wametokea katika kazi au mazingira duni, lakini kwa Fabrice Ngoy imekuwa tofauti kwani mshambuliaji huyu yeye aliamua kuachana na kazi ya Ualimu na kuibukia katika soka.

Nyota huyu alisema licha ya kucheza soka ila amesomea Stashahada ya Ualimu (Diploma of Education), huko kwao Congo japo hajaipa kazi hiyo nafasi kubwa katika maisha yake, kwa sababu alipenda kucheza mpira akiamini ndio utakaomlipa zaidi.

“Niliwahi kufundisha miezi sita tu na baada ya hapo nikaamua kuachana na kazi hiyo na hata nitakapoachana na soka sina uhakika kama nitarudi tena kufundisha, nafikiria nitakapostaafu nifanye mambo mengine tofauti na ufundishaji,” alisema.

Ngoy alisema sababu ya kutokuwa na mzuka wa kufundisha ni kutokana na kuona kazi hiyo haina maslahi zaidi kama kucheza mpira.

“Ni kweli napenda kufundisha ndio maana niliamua kusomea lakini kwa sasa akili zangu zote zipo kwa ajili ya kucheza tu, naiheshimu sana kazi hiyo kwa sababu imenikutanisha na kuniunganisha na watu mbalimbali ambao watabakia moyoni mwangu.”

Nyota wa Namungo, Fabrice Ngoy, ambaye ni raia wa DR Congo. Picha na Namungo FC

FAMILIA YA SOKA

Ngoy alisema kwao ni familia ya mpira na asilimia kubwa ya ukoo wao wameucheza huku akitolea mfano Baba yake mzazi, japo anakiri hakucheza kwa kiwango kikubwa kama alipofikia yeye kwa sasa ingawa ndiye aliyemshawishi kuupenda na kuucheza.

“Baba yangu mzazi alicheza mpira ingawa ni katika madaraja ya katikati, alinivutia na mimi kupenda kucheza hadi leo hapa nilipo, nashukuru amenipa sapoti na amekuwa akiniunga mkono katika kazi yangu, jambo linalonipa motisha ya kupambana.”

Baadhi ya wachezaji wa Namungo, wakishangilia moja ya bao katika mechi ya Ligi Kuu Bara, wapili kushoto ni mshambuliaji wa timu hiyo, Fabrice Ngoy. Picha na Namungo FC

UTOFAUTI WA LIGI KUU

Alisema licha ya kucheza Ligi mbalimbali ila amegundua Tanzania ni miongoni mwa nchi nzuri na salama na ndio sababu ya nyota wengi kutoka mataifa tofauti kukimbilia huku, kutokana na uhuru wanaoupata ambao huwezi kuupata sehemu nyingine.

“Siwezi kusema wachezaji wa DR Congo wanaokuja huku haina maana huko wanapotoka hawalipwi vizuri isipokuwa inategemea tu na mkataba ulioingia na timu husika, kwani wapo wanaocheza nchini kwetu na wanalipwa fedha nyingi kuliko wa Tanzania,” alisema Ngoy.

Mshambuliaji wa Namungo, Fabrice Wa Ngoy, akishangilia moja ya bao lake. Picha na Namungo FC

TUKIO ASILOSAHAU

Ngoy alieleza moja ya changamoto kubwa ambayo amepitia katika soka la Tanzania na hatokaa akaisahau hadi sasa ni kitendo cha kujiunga na Namungo msimu wake wa kwanza, ambao alikaa nje kwa zaidi ya miezi tisa bila kucheza kufuatia majeraha.

“Kipindi najiunga na Namungo FC msimu wa 2023-2024, nilifurahi sana kwani nilitamani kucheza Ligi Kuu Bara na kuonyesha uwezo wangu, ingawa niliingia kwa bahati mbaya kwa sababu nilicheza michezo miwili tu baada ya kuvunjika mfupa wa mguu,” alisema mshambuliaji huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *