Ukandamizaji wa kikoloni wa Italia nchini Eritrea haukuwa tu mradi wa upanuzi wa ushawishi wa kisiasa, bali ulikuwa mfumo uliosimikwa juu ya uvamizi wa kijeshi, ubaguzi wa rangi au apathaidi, ukandamizaji wa upinzani, na utumwa. Mfumo huu wa kikoloni ulifikia kilele mwaka 1938, katikati ya jiji la Roma, hatua ya malalmiko iliyochukuliwa na Zerai Deres ilipofichua wazi unafiki na ukatili wa utawala huo.

Ukoloni na ukandamizaji wa Italia nchini Eritrea, kama ambavyo nyaraka za kihistoria zinavyothibitisha, tangu mwanzo uliundwa juu ya mantiki ya utawala wa mabavu na kulazimisha. Mantiki hii haikujengwa juu ya ridhaa ya watu wa asili, bali juu ya uvamizi wa kijeshi, mikataba isiyo sawa, na miundo ya ubaguzi wa kimfumo. Katika miongo iliyofuata, kwa kupitishwa kwa sheria za kibaguzi za Italia na kuimarishwa kwa fikra za ubabe wa kifashisti, mfumo huu wa kikoloni uligeuka kuwa mfano wa ukoloni mkali na wa ngazi‑ngazi za kitabaka. Maandamano ya mwaka 1938 mjini Roma yalikuwa ni mojawapo tu ya dalili za mlipuko wa ndani wa migongano na migawanyiko iliyojificha ndani ya mfumo huo.

Uwepo wa Italia katika fukwe za Bahari ya Shamu au Bahari Nyekundu ulianza kwa ununuzi wa bandari ya Assab mwaka 1869, na mwaka 1882 bandari hiyo ikawekwa chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa Ufalme wa Italia. Mnamo 1885, majeshi ya Italia yaliiteka bandari ya Massawa, na hatua kwa hatua yakapanua ushawishi wao kuelekea maeneo ya ndani. Kwa kutiwa saini kwa Mkataba wa Wuchale mwaka 1889, ambapo tafsiri tofauti ya kifungu cha 17 ilisababisha mzozo wa kidiplomasia kati ya Italia na Uhabeshi (Ethiopia), Italia ilijenga msingi wa kisheria uliodaiwa kuhalalisha utawala wake juu ya ardhi hiyo. Hatimaye, tarehe 1 Januari 1890, koloni la “Eritrea ya Italia” likatangazwa rasmi. Tangu mwanzo kabisa, utawala wa eneo hili ulikuwa wa kijeshi kwa asili, huku miundo ya mamlaka ikishikiliwa na magavana walioteuliwa moja kwa moja kutoka Roma.

Katika miongo ya mwanzo, sera ya ukoloni wa walowezi ilifuatwa kwa uthabiti. Asmara iligeuzwa kuwa mji mkuu wa kiutawala, na kwa uhamiaji mkubwa wa raia wa Italia, muundo wa idadi ya watu wa mji huo ulibadilika kwa kiasi kikubwa. Kulingana na takwimu zilizopo, wakati wa kukaribia Vita vya Pili vya Dunia, takribani Waitalia 70,000 hadi 75,000 waliishi nchini Eritrea, na Asmara ikawa mojawapo ya vituo muhimu zaidi vya uwepo wa walowezi wa Ulaya barani Afrika. Uhamiaji huu haukuwa tu harakati ya kawaida ya watu, bali ulikuwa chombo mahsusi cha kuimarisha ubeberu wa kisiasa na kiuchumi: ardhi, mtaji, na nafasi muhimu za ajira ziliwekwa kwa kiasi kikubwa mikononi mwa walowezi, huku wenyeji wakiachwa katika ngazi za chini za utawala na jeshi.

Zerai Deres

Kwa kuingia madarakani kwa utawala wa Benito Mussolini mwaka 1922, sera za kibaguzi zilipata sura rasmi zaidi na zikavishwa vazi la kiitikadi. Sheria za ubaguzi wa rangi za Italia za mwaka 1938 zilipiga marufuku ndoa kati ya Waitalia na Waafrika, zikaharamisha mahusiano ya kuishi pamoja bila kufunga ndia baina ya Waafrika na Waitalia yaliyofahamika kama madamato, na zikathibitisha kwa njia ya kisheria wazo la ubora wa Waitalia  kuliko Waaafrika. Sheria hizi hazikubana tu mahusiano ya kijamii, bali pia ziliwanyima wenyeji haki ya upatikanaji sawa wa elimu, nyadhifa za serikali, na haki nyingi za kiraia. Kwa matokeo hayo, muundo wa kisheria wa koloni uligeuzwa kuwa mfumo unaofanana na ubaguzi wa rangi kama ule wa Apertheid au apathaidi wa Afrika Kusini, ambamo uraia na rangi ya ngozi vilikuwa vigezo vinavyoamua hadhi na nafasi ya mtu katika jamii.

Katika nyanja ya kiuchumi pia, miradi ya miundombinu—ikiwemo reli ya Asmara–Massawa na maendeleo ya miji—kwa kiasi kikubwa iliundwa na kuendeshwa kwa ajili ya maslahi ya kijeshi na kiuchumi ya Italia, si kwa ustawi wa jamii za wenyeji. Nguvu‑kazi ya asili, wakiwemo askari wa kikoloni waliotambulika kama Askari, ilitumika kwa upana katika miradi hii na ndani ya mifumo ya kijeshi ya utawala wa kikoloni. Aidha, Eritrea iligeuzwa kuwa ngome ya kimkakati ya operesheni za kijeshi za Italia katika Pembe ya Afrika. Wakati wa Vita ya Pili kati ya Italia na Ethiopia, majeshi ya Italia yalitumia ardhi ya Eritrea kama kituo cha kuanzisha mashambulizi dhidi ya Ethiopia. Katika muktadha wa vita hivyo, jeshi la Italia lilitumia silaha za kemikali, zikiwemo gesi ya haradali, hatua ambayo iliwakilisha ukiukaji wa wazi na wa makusudi wa sheria za kimataifa na kanuni za kibinadamu.

Jambo la msingi ni kwamba “Eritrea ya Italia” katika vita hivyo iligeuzwa kuwa kitovu kikuu cha ugavi wa kijeshi, makao ya kupeleka na kuimarisha majeshi, pamoja na kituo cha operesheni za anga katika uwanja wa mapigano wa kaskazini. Sehemu kubwa ya kusonga mbele kwa kijeshi kwa Italia ilianza kutoka mipaka ya kusini ya Eritrea, na vituo vya anga vilivyokuwa ndani ya koloni hili vilichukua nafasi ya kuamua katika utekelezaji wa mashambulizi ya mabomu. Ndege zilizoruka kutoka vituo hivyo, wakati wa kupenya ndani ya ardhi ya Ethiopia, zilitumia silaha za kemikali. Ingawa mashambulizi ya kemikali hayakutekelezwa ndani ya Eritrea yenyewe, kugeuzwa kwa ardhi hii kuwa jukwaa la kuanzishia vita vya kemikali kuliifanya kuwa sehemu ya miundombinu ya utekelezaji wa mojawapo ya uhalifu wa vita ulio wazi zaidi wa karne ya ishirini. Hili linaonesha kuwa Eritrea haikuwa tu koloni la kiutawala, bali ilikuwa kiungo cha msingi katika mashine ya vita ya utawala wa kifashisti wa Italia. Ingawa sehemu kubwa ya uhalifu huu ilifanyika ndani ya ardhi ya Ethiopia, nafasi ya Eritrea katika muktadha wa vifaa na operesheni za vita hivyo haiwezi kupingwa wala kupuuzwa.

Katika mazingira kama haya ya ubaguzi uliota mizizi kisheria na uhalifu wa kimuundo, tukio la tarehe 15 Juni 1938 mjini Roma lilipata maana iliyoenda mbali zaidi ya tendo la mtu binafsi. Siku hiyo, Zerai Deres, askari kutoka Eritrea aliyekuwa ametumikia katika vitengo vya kikoloni vya Italia, alichukua hatua ya maandamano katika Piazza dei Cinquecento, mbele ya mnara wa kumbukumbu wa Vita vya Dogali, unaofahamika pia kama Obelisko la Dogali. Mnara huo ulikuwa umejengwa kwa heshima ya wanajeshi wa Italia waliouawa katika mapigano ya mwaka 1887 dhidi ya majeshi ya Ethiopia, na katika simulizi rasmi la kifashisti uliwasilishwa kama ishara ya “kujitoa mhanga kwa ajili ya Dola.” Hata hivyo, katika muktadha wa ukoloni wa kibaguzi, uwepo wa mnara huo katikati ya Roma uliwakilisha pia kumbukumbu ya udhalilishaji na unyanyasaji wa watu waliotawaliwa, hali iliyofanya kitendo cha Zerai Deres kuwa sauti ya upinzani iliyochanua kutoka pembezoni mwa himaya hadi moyoni mwa mji mkuu wake.

Kwa mujibu wa simulizi za kihistoria, Zerai Deres alipaza sauti kaulimbiu zenye maudhui ya wazi ya kupinga ukoloni na akatangaza hadharani upinzani wake dhidi ya utawala wa Italia juu ya ardhi za Afrika. Hata hivyo, mwitikio wa mfumo wa mahakama wa Italia ulikuwa wa kutafakari kwa kina. Badala ya kufikishwa katika mchakato wa kawaida wa kisheria, alitangazwa kuwa “hana utulivu wa kiakili” na kupelekwa katika hospitali ya magonjwa ya akili, ambako alizuiliwa hadi mwisho wa maisha yake mwaka 1945. Kwa hakika, uamuzi huu ulifanywa na mamlaka za Italia kwa nia ya kuzuia Zerai Deres asiwe chanzo cha msukumo na hamasa miongoni mwa watu wa makoloni; kwa kuhusisha kitendo chake na kile kilichodaiwa kuwa ni ugonjwa wa akili, waliweza kuondoa maana ya kisiasa ya tukio hilo na kuzuia kuibuka kwa wimbi la mshikamano wa umma. Hata hivyo, katika kumbukumbu ya kihistoria ya Eritrea, Zerai Deres alibaki na hatimaye alitambuliwa kama ishara ya upinzani dhidi ya ukoloni. Baada ya Eritrea kupata uhuru, sanamu na alama za ukumbusho zilisimikwa mjini Asmara kwa heshima yake, zikithibitisha nafasi yake kama sauti ya heshima na upinzani wa Waafrika dhidi ya udhalimu wa kikoloni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *