
Dar es Salaam. Mchakato wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na viongozi wengine, kama ilivyoelekezwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, umeibua maswali tata kutokana na sintofahamu zilizojitokeza kwenye utekelezaji wa maelekezo hayo.
Februari 13, mwaka huu, Msajili wa Vyama vya Siasa alibatilisha uchaguzi mkuu wa chama hicho wa Desemba 2024, uliomweka madarakani Profesa Ibrahim Lipumba na viongozi wenzake watano, ukiwa umepita miaka miwili tangu ulipofanyika.
Mbali na Profesa Lipumba, wengine walioathirika na uamuzi huo ni Makamu Mwenyekiti, Mbarouk Seif Salim (Zanzibar), Othman Dunga (Bara), Katibu Mkuu, Husna Mohamed Abdallah, Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya (Bara), na Ali Juma Khamis (Zanzibar).
Sababu ya kubatilishwa kwa uchaguzi huo ni kuwa washindi hawakupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa na wajumbe, kinyume na matakwa ya Katiba ya chama inayohitaji mshindi kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura halali.
Katika kutekeleza maelekezo hayo ya msajili, CUF kilifanya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi, na siku hiyo hiyo lilifunguliwa pazia la uchukuaji na urejeshaji fomu, siku iliyofuata mchujo ulifanyika na majina kupelekwa kwenye mkutano mkuu kupigiwa kura.
Mchakato huo ulianza Februari 20, mwaka huu, na kufikia Februari 22, kila kitu kilikuwa kimekamilika, kuanzia kikao cha Baraza Kuu la Uongozi hadi mkutano mkuu uliomchagua mwenyekiti mpya, Mirambo Yusuf.
Katika kutekeleza maelekezo ya msajili aliyetaka uchaguzi huo kurudiwa, Mwananchi linaangazia maswali tata matano yaliyoibuka kwenye mchakato mzima, kuanzia kuitishwa kwa mkutano hadi kupatikana kwa viongozi wapya.
Nani aliitisha mkutano mkuu?
Moja ya maswali yanayoibua sintofahamu ndani ya CUF ni nani aliyeitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi na hatimaye mkutano mkuu. Mchakato mzima wa kupata viongozi umeenda haraka, licha ya miezi mitatu waliyokuwa nayo kutekeleza maelekezo ya msajili.
Kwa mujibu wa Ibara za 72(2) na (3) za Katiba ya CUF ya mwaka 1992, toleo la 2019 na marekebisho yake ya 2024, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) ndicho chombo chenye mamlaka ya kuitisha mkutano mkuu wa taifa wa dharura.
Katiba hiyo inabainisha hata pale ambapo mkutano huo utaitishwa kwa makubaliano ya zaidi ya nusu ya wajumbe wa mkutano mkuu wa taifa kutoka kila upande wa Muungano.
Kwa msingi huo, mkutano huo ulipaswa kuitishwa na Profesa Lipumba, ambaye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF kabla ya uchaguzi wa Desemba 2024 ambao msajili hautambui, lakini hadi sasa haijafahamika, na hata watendaji wake wanashangaa ni nani aliyeandaa mkutano huo.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, amesema jukumu la kuitisha mkutano mkuu maalumu linafanywa na mwenyekiti, na kwa kuwa msajili alieleza kutoutambua uongozi, ilitakiwa kaimu katibu mkuu aitishe kikao hicho.
“Baraza linakaa ili kuangalia namna ya kujaza hizo nafasi. Kaimu katibu mkuu angeitisha baraza kwa utaratibu unaoeleweka, na kwa kuzingatia Katiba yetu, baraza linatakiwa kuitishwa kila baada ya miezi minne,” amesema.
Katika maelezo yake, baraza la mwisho lilifanyika Desemba 2025, hivyo Machi mwaka huu walitakiwa kuitisha baraza ambalo lilipaswa kujadili barua iliyotoka kwa msajili na lingeandaa mkutano mkuu maalumu.
“Baada ya baraza kuitishwa, lingetoa ratiba ya kuchukua fomu na kurejesha, mchakato wa kuchuja, na kuitisha mkutano mkuu ufanyike, lakini kilichofanyika ni ukiukwaji, na haijawahi kutokea,” amesema.
Kwa upande wake, mmoja wa wajumbe wa baraza kuu, upande ulioandaa mkutano huo, Dauda Hassan, amesema hoja hiyo inahusu Katiba, na walitumia Ibara ya 77(4). Amesema walisoma mara kwa mara vifungu na walitumia kifungu kilichowapa fursa wajumbe kuitisha mkutano mkuu.
“Kifungu hicho kinasema wajumbe wa mkutano mkuu wanaweza kuitisha mkutano mkuu kama wataona kuna jambo limejitokeza na kimeenda mbali, ni wangapi wanaweza kuitisha mkutano huo,” amesema.
Amesema mwenyekiti hakuwa halali pamoja na wateule wake wote, kama wangelikuwa halali, basi wangewasilisha kwa akina Sakaya na watendaji wengine wa chama.
Nani amewalipa posho wajumbe?
Mkutano mkuu maalumu ulifanyika ndani ya muda mfupi, huku ukihudhuriwa na wajumbe kutoka mikoani, jambo lililohitaji uwezeshaji wa kifedha kwa ajili ya nauli na posho zao katika kipindi chote walipokuwa Dar es Salaam kuhudhuria mkutano huo.
Hata hivyo, bado haijulikani ni nani amewalipa posho wajumbe, kwani viongozi waliokuwa madarakani hawajaidhinisha fedha kutolewa kwa ajili ya posho za wajumbe wa baraza kuu na mkutano mkuu.
Mwananchi lilishuhudia wajumbe wakiitwa kwenda kulipwa posho zao, na kulikuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wajumbe waliolalamikia kutorudishiwa nauli walizotumia kuja Dar es Salaam na posho nyingine za kujikimu.
Akizungumzia hilo, Sakaya amesema haijulikani ni nani aliyetoa gharama za kuendesha mchakato mzima, kwa kuwa uongozi uliokuwepo haukushiriki kwenye vikao vilivyofanyika wala haukuviitisha kwa mujibu wa Katiba yao.
“Chama hakijatoa fedha yoyote, wala hatukushirikishwa. Tulishangaa kuona taarifa za baadhi ya wajumbe wakipiga simu kuulizia kuitishwa kwa mkutano mkuu, na tuliwakatalia. Chama hakijagharamia mchakato huo kwa namna yoyote,” amesema Sakaya.
Sakaya amesema mkutano mkuu unatakiwa kuwa na wajumbe 640 hadi 670. Hata hivyo, mkutano mkuu maalumu uliofanyika juzi ulihudhuriwa na wajumbe 533, kwa mujibu wa mwenyekiti wa uchaguzi, Said Miraji.
“Katika mkutano uliopita ambao umefutwa na msajili, mchakato mzima tulitumia Sh800 milioni, zinazohusisha kurejesha gharama za wajumbe walizotumia kuja katika mkutano mkuu na baraza kuu, kisha kuwapa kiasi kingine cha fedha za kujikimu,” amesema.
Hata hivyo, Dauda, aliyekuwa akiwalipa wajumbe, amesema walipata fedha kutoka kwa mfadhili mmoja aliyewasaidia kuandaa mkutano huo, hata hivyo, hakuwa tayari kumtaja mfadhili huyo.
“Katiba yetu inasema chama kinaweza kupata mfadhili mwingine wa ndani au nje ya chama. Mfadhili wa nje tuliyempata hatuwezi kumtaja hadharani kwa sasa,” amesema mjumbe huyo na kuongeza:
“Ametusaidia kutoa chake, na alichokitoa hakina ukaguzi, na hajakitoa kwa niaba ya chama. Alitupatia kusaidia mkutano mkuu, na kuna kiasi kingi tulipata, mfadhili huyo alikuwa anakagua mwenyewe, na biashara imeisha.”
Fomu kutolewa bure
Katika kikao cha baraza kuu la uongozi, shughuli ya uchukuaji na urejeshaji fomu ilifunguliwa rasmi, na hakukuwa na masharti yoyote, hususan ya kulipia ada kama kanuni za chama hicho zinavyoelekeza.
Katika uchaguzi uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024, gharama ya fomu inayoelekezwa na kanuni za chama hicho ilikuwa Sh500,000 kwa nafasi ya mwenyekiti. Hata hivyo, safari hii hali imekuwa tofauti, fomu zimetolewa bure.
“Kiwango hicho ni kanuni ya chama, lazima anayegombea nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti atoe kiwango hicho, na mwaka juzi tulikuwa na wagombea wanane na wote walitoa kiwango hicho,” amesema.
Kuhusu hoja hiyo, Dauda amesema walifanya hivyo kwa kuwa waliona baraza kuu lina maazimio, na Katiba ya chama hicho haijasema.
“Katiba yetu inasema baraza kuu ndilo linatunga kanuni na lina mamlaka ya kutengua. Kwa hiyo, kanuni ya kuchukua fomu kwa fedha ilitenguliwa na baraza kuu kwa kuwa muda ulikuwa mdogo ili tusiwanyime watu haki ya kushiriki uchaguzi,” amesema.
Msajili kutohudhuria mkutano
Kwa kawaida, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa huhudhuria mikutano mikuu ya vyama vya siasa na hata kupewa nafasi ya kutoa salamu. Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwenye mkutano huo, kwani hakukuwa na uwakilishi wowote kutoka ofisi hiyo.
Mwananchi limezungumza na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, kutaka ufafanuzi kuhusu msajili kutohudhuria mkutano huo. Nyahoza amesema kisheria si lazima wahudhurie, kwa sababu tayari walishatoa taarifa ya kufanya mkutano wao.
“Kisheria si lazima ofisi ya msajili ihudhurie, lakini taarifa ya mkutano walitoa. Taarifa yao ilikuwa ya ghafla, na nilikuwa Dodoma, ndiyo maana nilishindwa kuhudhuria,” amesema msaidizi huyo wa msajili.
Uhalali wa wajumbe
Mkutano mkuu maalumu umefanyika ndani ya muda mfupi, jambo linaloibua maswali kuhusu wajumbe 533 walioshiriki kama ni halali au la. Baadhi ya wagombea kwenye uchaguzi huo walilalamikia suala hilo.
Mgombea wa nafasi ya mwenyekiti, Omar Dunga, aliyeshika nafasi ya pili kwa kura 177, alilalamikia aina ya wajumbe waliohudhuria, akisema wengi wao hawakuwa halali, kwani walikuwa wageni.
“Nina mashaka makubwa na wajumbe wengi si halali, wajumbe wa mkutano mkuu wanafahamika hata kwa haiba yao. Ni kama wameenda kuchukuliwa mtaani na kuletwa hapa,” amesema Dunga, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF Tanzania Bara.