Dar es Salaam. Wakati mapinduzi ya kidijitali yakiendelea kushika kasi duniani, Serikali imeonya kuwa mageuzi hayo yasigeuke kikwazo kipya cha haki kwa wananchi, bali yawe daraja la kuwafikia waliokuwa pembezoni mwa mifumo ya sheria kwa muda mrefu.

Sambamba na hilo Serikali imetaka matumizi ya teknolojia katika sekta ya sheria na utoaji haki kuwa chachu ya kupanua wigo wa upatikanaji wa haki kwa wananchi wote, badala ya kuanzisha aina mpya ya ubaguzi wa kidijitali.

Hayo yameelezwa leo Februari 24, 2026 na Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria, Zainab Katimba, alipofungua kongamano la Afrika Mashariki linalojadili matumizi ya teknolojia katika kupanua wigo wa haki (legal tech), likiwakutanisha wadau kutoka serikalini, mahakama, asasi za kiraia, sekta binafsi na vyuo vikuu lililoandaliwa na Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akizungumza katika kongamano hilo, Katimba amesema licha ya juhudi zinazoendelea, wananchi wengi Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki bado wanakabiliwa na changamoto  za kisheria, ikiwamo migogoro ya ardhi, masuala ya kifamilia, migogoro ya ajira na ukiukwaji wa haki za binadamu, bila kupata msaada wa kisheria kwa wakati au kwa gharama nafuu.

Amebainisha kuwa vikwazo hivyo vinatokana na gharama kubwa za huduma za kisheria, umbali wa kijiografia, ugumu wa taratibu na pengo la kidijitali linalozidi kupanuka.

Naibu Waziri Wizara ya  Katiba na Sheria Zainab Katimba akizungumza wakati wa kongamano la Afrika Mashariki kuhusu matumizi ya teknolojia katika mifumo ya utoaji haki.

“Upatikanaji wa haki si suala la kisheria pekee. Ni ajenda ya maendeleo, ni kipaumbele cha utawala bora na ni suala la heshima ya utu wa binadamu,” amesisitiza.

Katimba amesema mageuzi ya sekta ya sheria ni sehemu ya nguzo muhimu za utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi shindani, jumuishi na unaotegemea maarifa.

Amefafanua kuwa uchumi wa kisasa unahitaji sheria zinazoeleweka na kutabirika, jamii ya kidijitali inahitaji taasisi zinazoaminika, na dola jumuishi inahitaji haki inayopatikana kwa wote bila ubaguzi.

“Kadri tunavyosonga kuelekea 2050, upanuzi wa huduma za msaada wa kisheria, uboreshaji wa mifumo ya mahakama kwa njia ya kidijitali na maboresho ya udhibiti wa teknolojia ni sehemu ya mabadiliko ya kimuundo ya kuimarisha misingi ya maendeleo endelevu,” amesema.

Ameonya kuwa teknolojia ni nyenzo ya kimkakati ya kuwezesha haki, lakini si mbadala wa taasisi za utoaji haki wala uamuzi wa kibinadamu.

Ameitaja misingi muhimu inayopaswa kuzingatiwa katika ujenzi wa haki za kidijitali kuwa ni pamoja na kuwepo kwa misingi thabiti ya kisheria na kiudhibiti, ulinzi wa faragha na taarifa binafsi, miundombinu jumuishi ya kidijitali, uwezo wa taasisi na zaidi ya yote, imani ya umma.

“Bila misingi hiyo, uwekaji wa mifumo ya kidijitali unaweza kuongeza pengo la usawa badala ya kulipunguza, teknolojia inapaswa kurahisisha taratibu, kupunguza gharama na kuleta huduma karibu na wananchi. Haki ya kidijitali isigeuke kuwa ubaguzi wa kidijitali,” amesisitiza.

Akizungumza kwenye kongamano hilo Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria, Esther Msambazi amesema utekelezaji wa  Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 imesaidia kuimarisha huduma za msaada wa kisheria kwa kusisitiza uratibu, utoaji elimu kwa umma na kuimarisha nafasi ya wasaidizi wa kisheria (paralegals) pamoja na mipango inayozingatia jamii.

“Kupitia mfumo huo, huduma zimepanuliwa zaidi kwa makundi yaliyo katika mazingira magumu, wakiwamo wanawake, watoto, watu wenye ulemavu na wananchi wa maeneo ya vijijini na yasiyofikika kirahisi.

Amesema maendeleo ya haraka ya teknolojia ikiwamo ufungaji wa mashauri kwa njia ya mtandao, usikilizwaji wa kesi kwa njia ya mtandao, mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa mashauri na matumizi ya akili bandia (AI) yanabadilisha namna haki inavyopatikana na kutolewa.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa William Anangisye akizungumza wakati wa kongamano la matumizi ya teknolojia katika mifumo ya utoaji haki. Kongamano hilo limeandaliwa na Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

 Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye amesema taasisi hiyo inaamini haki si nadharia ya kufundishia darasani bali ni wajibu wa kila siku unaotekelezwa kwa vitendo na ndiyo sababu kupitia kliniki ya sheria chuoni hapo wameendelea kusaidia maelfu ya Watanzania.

Amesema kliniki hiyo si tu kituo cha huduma, bali pia ni darasa hai linalowalea wanafunzi wa sheria kwa vitendo.

“Hapa ndipo misingi inayofundishwa darasani inapopimwa katika kesi halisi zenye athari za moja kwa moja kwa maisha ya watu. Tunakuza kizazi cha mawakili wanaotambua kuwa taaluma yao ipo kwa ajili ya masilahi ya umma,” amesema.

Mbali na kliniki hiyo, chuo hicho pia kina Kikundi cha Utafiti wa Sheria, Jamii na Teknolojia kinachochunguza namna teknolojia inavyoweza kupanua upatikanaji wa haki huku kikitahadharisha hatari za kutengwa kidijitali, upendeleo wa kimfumo na changamoto za maadili.

Utafiti wa kikundi hicho umeendelea kuishauri Serikali, kuimarisha asasi za kiraia na kuchochea mjadala wa kikanda kuhusu haki ya kidijitali.

Pia, chuo hicho kimeanza kufundisha teknolojia ya sheria kupitia zana za utafiti mtandaoni, mahakama za majaribio kwa njia ya mtandao na mifumo ya kuigiza mashauri, hatua inayolenga kuwajengea wanafunzi ujuzi unaohitajika katika taaluma ya sheria ya kisasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *