
WAKATI wachezaji wakielezea ugumu wa michezo waliyocheza katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) 2025, nyota wa Vijana (City Bulls), Leonard Andrea amesema mchezo dhidi ya Dar City ulikuwa mgumu na kamwe hatausahau. Mchezo huo ulifanyika katika Uwanja wa Donbosco (Upanga), na Dar City ilishinda kwa pointi 80-60.
Andrea aliyecheza BDL kwa miaka miwili akitokea katika kikosi cha pili cha timu hiyo maarufu kama Jogoo, katika mchezo na Dar City alidaka mipira ya ribaundi sita, akazuia (block) mara moja na kufunga pointi 10.
Alisema ugumu wa mchezo huo ulitokana na wachezaji wenye viwango vya kimataifa aliopambana nao kwa mara ya kwanza.
“Nilipambana nao (wachezaji wa timu pinzani). Niliweza kuwadhibiti, ingawaje timu hiyo ilitushinda katika mchezo uliokuwa mgumu. Kilichotufanya mpaka tukafungwa ilitokana na benchi la timu hiyo lilikuwa bora lenye wachezaji nyota ambao kila anayeingia alionekana kuwa bora,”€ alisema Andrea.
Kwa upande wa maandalizi yake ya ligi hiyo msimu huu, alisema amekuwa akifanya mazoezi makali baada ya kukumbuka mchezo huo mgumu kwake.
Andrea anayecheza nafasi ya namba tano maarufu ‘senta’, alisema vitu alivyovikosa katika mchezo dhidi ya Dar City amekuwa akifanyia kazi katika uwanja wa mazoezi.
“Kama vile kwenye kumalizia wakati naenda kufunga, na upande wa ulinzi tatizo lililokuwepo katika mchezo huo ilikuwa ni ngumu kuwazuia,” alisema Andrea aliyedai amekuwa akifanya mazoezi ya kukimbia katika fukwe za bahari kwa saa mbili au tatu lengo likiwa ni kuwa na pumzi ya kutosha uwanjani.
Alitaja ratiba yake ya kila siku ya mazoezi akisema amekuwa akifanya mazoezi binafsi ya kukimbia katika Uwanja wa Mpira wa Kitunda, na nyakati za jioni Shule ya Sekondari ya Zanaki akiwa na wachezaji wenzake.
Alisema ligi inatarajiwa kuwa ngumu kutokana na kila timu kuonyesha kujipanga zaidi mapema na kwamba, wachezaji wa kigeni wamekuwa wakitoa ushindani kwa wazawa akiwamo yeye huku wao wakijifunza mbinu za uchezaji wao.
Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam itaanza baada ya kamati ya mashindano kukutana na uongozi mpya wa Chama cha Kikapu Dar es Salaam (BD).