Dar es Salaam. Mwanamuziki wa Bongofleva, Harmonize amejizolea mashabiki wengi kutokana na uwezo wake kimuziki pamoja na mtindo wake wa maisha nje ya sanaa ambao umekuwa ukijadiliwa sana mitandaoni.
Akiheshimika kama chapa, tayari Harmonize ameshinda tuzo za ndani na kimataifa, ametoa albamu na ameanzisha lebo ya Konde Music Worldwide ambayo iliwatoa Ibraah na Angella. Fahamu zaidi…!
1. Hadi Harmonize anaondoka WCB Wasafi mwishoni mwa 2019, alikuwa ameshinda tuzo mbili za kimataifa, African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) na African Entertainment Awards USA (AEAUSA) 2016.
2. Ndani ya kipindi cha miaka 10 tangu alipotoka rasmi kimuziki mwaka 2015, Harmonize ameachia albamu tano zenye jumla ya nyimbo 76, zenye urefu (muda) wa dakika 246, sawa na saa nne.
3. Harmonize ndiye msanii pekee Afrika Mashariki ambaye amefanya kolabo mbili na mshindi wa Grammy 2021 kutoka Nigeria, Burna Boy, mkali wa kibao cha Last Last (2022).
4. Burna Boy amesikika katika nyimbo za Harmonize kama ‘Kainama’ kutoka katika Extended Playlist (EP) yake ya kwanza, Afro Bongo (2019), na pia ‘Your Body’ kutoka albamu yake kwanza, Afro East (2020).
5. Hadi anaondoka WCB Wasafi, Harmonize alikuwa ndiye msanii wa pili wa Bongofleva aliyetazamwa zaidi YouTube nyuma ya Diamond Platnumz, ambaye sasa kwa ujumla anashikilia nafasi ya pili Afrika. Lakini, ndani ya kipindi kifupi, Harmonize alipitwa na Rayvanny ambaye Oktoba 2023 aliweka rekodi ya kutazamwa mara bilioni moja YouTube, huku Harmonize akifikia rekodi hiyo Novemba 2023.
6. Video ya wimbo wake, Kwangwaru (2018) akimshirikisha Diamond, hadi sasa ndio iliyofanya vizuri zaidi (most viewed) YouTube upande wa Harmonize ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 137.
7. Harmonize anashikilia rekodi kama msanii pekee wa Bongofleva aliyeweza kutoa albamu kwa miaka mitano mfululizo akifanya hivyo kuanzia mwaka 2020 hadi 2024. Albamu hizo ni Afro East (2020), High School (2021), Made For Us (2022), Visit Bongo (2023) na Muziki wa Samia (2024), huku albamu yake ya sita ’31’ iliyopangwa kuachiwa 2025 ikisogezwa mbele.
8. Kuna nyimbo mbili Harmonize amelitaja jina la mchumba wake Kajala Masanja. Nazo ni Zilipendwa (2018) ambao uliwashirikisha wasanii wote wa WCB Wasafi kwa wakati huo, na mwingine ni Ushamba (2020).
9. Vilevile Harmonize ana wimbo mmoja aliolitaja jina la binti wa Kajala, Paula, nao ni Mtaje (2021) kutoka katika albamu yake ya pili chini ya Konde Music Worldwide, High School (2021) yenye nyimbo 20.
10. Harmonize amefanya video nyingi za nyimbo zake na baadhi ya warembo ambao amewahi kuwa na uhusiano nao, lakini ile ya Kajala, Nitaubeba (2022) ndio imetazamwa zaidi YouTube. Hiyo ya Kajala ambayo tayari imetazamwa zaidi ya mara milioni 42 imezipita zile Harmonize alizoshirikiana na Jacqueline Wolper (Niambie – 2017) na Sarah Michelotti (My Boo Remix – 2019, & Niteke – 2019).