Manchester United imeendelea kufufuka chini ya kocha wake wa muda, Michael Carrick, baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Everton katika mchezo wa Ligi Kuu England uliopigwa jana usiku kwenye Uwanja wa Hill Dickinson.
Bao pekee la mchezo huo limefungwa na mshambuliaji, Benjamin Šeško, dakika ya 70, akiendeleza makali yake tangu Carrick alipochukua mikoba ya Ruben Amorim.
Ushindi huo ni wa tano kwa United katika mechi sita za hivi karibuni, hatua iliyowapandisha hadi nafasi ya nne wakiipita Chelsea na sasa wakiwa na tofauti ya pointi tatu nyuma ya Aston Villa walio nafasi ya tatu.
Kocha wa muda wa Man United, Michael Carrick, alipokuwa akiwaelekeza jambo wachezaji wake katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Everton. Picha na Mtandao
United walikuwa wageni kwa mara ya kwanza katika uwanja mpya wa Everton, lakini hawakuonekana kuathiriwa na presha ya mashabiki wa nyumbani. Kipindi cha kwanza kilikuwa na ushindani mkali huku pande zote zikikosa umaliziaji wa mwisho.
Everton walipata nafasi ya mapema kupitia mashambulizi ya kasi, lakini kipa wa United, Senne Lammens, alikuwa imara langoni. Kwa upande wa United, Bryan Mbeumo na Bruno Fernandes walitengeneza nafasi kadhaa, lakini walishindwa kuzitumia.
Mshambuliaji wa Man United, Benjamin Sesko, wakati akipiga shuti lililozaa bao pekee katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Everton. Picha na Mtandao
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi huku Everton wakitengeneza nafasi nzuri kupitia Iliman Ndiaye na Harrison Armstrong, lakini walishindwa kumalizia kwa ufanisi.
Dakika ya 70, United walifanya shambulizi la kushtukiza lililozaa matunda. Matheus Cunha alianzisha mpira mrefu uliomkuta Mbeumo, ambaye alimpasia Šeško mpira. Bila kupoteza muda, Šeško alipiga shuti la kwanza lililomshinda kipa Jordan Pickford na kuandika bao pekee la ushindi.
Kipa wa Man United, Senne Lammens, akijaribu kuokoa moja ya jaribio hatari lililopigwa langoni kwakwe. Picha na Mtandao
Everton walijaribu kusawazisha katika dakika za mwisho, lakini safu ya ulinzi ya United ilisimama imara. Lammens aliokoa hatari nyingine dakika za mwisho baada ya kupangua shuti kali la Michael Keane.
Kwa ushindi huo, Manchester United wanaendelea kuonyesha dalili za kurejea katika ushindani wa juu wa Ligi Kuu England, huku Šeško akizidi kuthibitisha kuwa silaha muhimu hata anapoanzia benchi.