Geita. Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (Stamico) imesaini mkataba wa ushirikiano na kampuni ya uchimbaji madini ya Plantcor kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya utafiti na uchimbaji wa madini katika Pori na Hifadhi ya Msitu wa Kigosi, uliopo wilayani Bukombe mkoani Geita.

Hafla ya utiaji saini wa mradi huo imefanyika leo, Jumanne Februari 24, 2026, katika Ukumbi wa CCM wilayani Bukombe, ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kiruswa ametoa rai kwa mwekezaji kuhakikisha kuwa utafiti utakaofanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya ndege nyuki kabla ya kuanza uchimbaji wa dhahabu, unazingatia uwazi wa utoaji taarifa kwa wananchi ili nao waweze kunufaika na taarifa hizo.

Naibu Waziri wa madini, Steven Kiruswa, akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ubia baina ya Shirika la Madini la Stamico na kampuni ya Plantcor, wilayani Bukombe Mkoa wa Geita. Picha na Geofrey Chubwa.

Pia, Kiruswa amemtaka mwekezaji huyo kuboresha miundombinu, ikiwemo barabara, kupitia utaratibu wa Urejeshaji kwa Jamii (CSR), ili kurahisisha upatikanaji wa maeneo ya uchimbaji kwa wachimbaji wadogo, kwani hali ya sasa hairidhishi.

“Nitoe rai kwa mwekezaji, fungueni njia ili wananchi wafike mgodini. Natambua kuwa njia hazipitiki,” amesema.

Eneo la Kigosi awali lilikuwa Hifadhi ya Taifa. Hata hivyo, mwaka 2023, akiwa Bungeni, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo, Mohamed Mchengerwa, alieleza kuwa Serikali imelishusha hadhi eneo hilo kutoka Hifadhi ya Taifa na kuwa Hifadhi ya Msitu chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), na kuruhusu shughuli za kibinadamu kufanyika.

Hatua hiyo ilifuatia kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi yenye ukubwa wa kilomita za mraba 7,460 chini ya Sheria ya Misitu, Sura ya 323.

Mbunge wa Bukombe Doto Biteko,akizungumza katika hafla hiyo.

Mradi huo unatarajiwa kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi katika wilaya hiyo kupitia mapato ya kodi na mirabaha, uboreshaji wa miundombinu, utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi, pamoja na ajira za muda mfupi na mrefu zipatazo 2,000.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Plantcor, Joseph Wilmans, amesema kuwa kupitia uwekezaji huo, wananchi wanaozunguka eneo la mradi watanufaika kwa kupata ajira na kushirikishwa katika shughuli za utafiti wa madini kwa kutumia teknolojia ya kisasa

“Tumekuja kuunganisha ujuzi baina yetu na Stamico kupitia leseni ya uchimbaji ya Kigosi, pia lengo kuu ni kuwanufaisha wananchi wa Bukombe na Mkoa wa Geita kwa kuongeza thamani ya madini yaliyopo ili kuwanufaisha wananchi wote.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico, Balozi Simon Sirro, ametoa wito kwa wabia hao, kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za nchi katika sekta ya madini.

Pia, amesisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji wa shughuli hizo, pamoja na kulinda maslahi ya wananchi wanaozunguka mradi huo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico, Balozi Simon Sirro ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, akizungumza katika hafla ya utiaji saini ushirikiano wa utafiti na uchimbaji madini baina ya Stamico na Kampuni ya Plantcor kutoka Afrika Kusini. Picha na Geofrey Chubwa.

Aidha, Balozi Sirro amewatahadharisha wananchi wanaoishi jirani na eneo la uwekezaji kuheshimu mipaka ya mradi na kuepuka kuvuruga shughuli hizo, hali ambayo inaweza kuathiri utekelezaji wake.

“Najua Kigosi vijana wetu walikuwa wakiingia kwa kuibia kujitafutia riziki. Tumezoea kuingia kwenye lile chaka, lakini niwaombe wananchi wasiwe wa kwanza kuvuruga ubia huu. Tuheshimu mipaka,” amesema Balozi Sirro.

Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dotto Biteko, amesema maendeleo ya sekta ya madini katika wilaya hiyo yamesaidia kupunguza matukio ya uhalifu ambayo awali yaliwafanya baadhi ya wawekezaji kuhofia usalama wao.

Aidha, amewataka wananchi kuchangamkia fursa zitokanazo na uwekezaji huo ili kunufaika na ukuaji wa uchumi unaotarajiwa.

“Mkiona fursa zinakuja, tuanze kuzichangamkia. Wilaya inafunguka. Nami nimekuja kushuhudia utiaji saini huu ili wakati wa uzee wetu tutasimulia kuwa tulikuwepo siku wanasaini mkataba, na baadaye tukashuhudia uwekezaji ukiwa mkubwa,” amesema Biteko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *