Tume moja ya Palestina inayoshughulikia masuala ya Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye jela za utawala wa kizayuni wa Israel imezishutumu mamlaka za jela hizo kwa kuwafanya Wapalestina hao washindwe kufunga Saumu zao “kwa wakati sahihi” katika mfungo huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi usiku, Tume ya Palestina ya Masuala ya Wafungwa imesema, mamlaka katika Gereza la Ofer kwenye mji wa Ramallah wa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu zinakataa kuwataarifu wafungwa kuhusu nyakati za kuchomoza na kuzama kwa jua ili waweze kuanza kufunga na kufungua Saumu zao kwa wakati.

Wakili wa tume hiyo Khaled Mahajneh, ameiambia redio rasmi ya Sauti ya Palestina: “Wafungwa wanafunga Ramadhani bila ya kula daku na kuufanya wakati wa kufuturu uwe mtihani mrefu na mgumu”. 

Mahajneh amesema, wafungwa Wapalestina katika Gereza la Gilboa lililoko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu iliyopachikwa jina bandia la Israel hawakuarifiwa hata kuhusu kuanza kwa Saumu ya mwezi wa Ramadhani, mwezi mtakatifu zaidi katika kalenda ya Kiislamu ya Hijria Qamaria.

Amebainisha kuwa, mmoja wa wafungwa aliweza kutambua kwamba Ramadhani imeanza, wakati alipofikishwa kwenye kikao cha kesi katika mahakama ya Israel.

“Kwa zaidi ya miaka miwili, Wapalestina walioko vizuizini wanalazimishwa kula mabaki ya takataka za chakula kwa ajili ya futari”, amefichua Mahajneh.

Wakili huyo wa Tume ya Palestina ya Masuala ya Wafungwa amesema: “Utawala ghasibu unajaribu kuifuta furaha ya wafungwa Wapalestina ya matukio ya kidini, na kufanya makusudi furaha ya familia zao isikamilike na iwe ya machungu kutokana na unyanyasaji na mateso wanayowapa watoto wao walioko magerezani”.

Kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Palestina na Israel,  zaidi ya Wapalestina 9,300 hivi sasa wanashikiliwa katika magereza ya utawala wa kizayuni, wakiwemo watoto 350, na wanakabiliwa na mateso, njaa, na kupuuzwa kupatiwa matibabu, hali ambayo imesababisha vifo vya Wapalestina kadhaa…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *