Afisa wa Uhusiano wa Nje wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR nchini Tanzania Bahia Egeh amesema, wakimbizi wa Burundi walioko nchini humo ambao wanarudi makwao, wanafanya hivyo kwa hiari wala hawashurutishwi.

Bi. Egeh amebainisha kuwa, tangu zoezi la kurejea nyumbani lilipoanza mwaka 2017, wakimbizi wengi wameamua kurudi nyumbani, lakini wengine wangali wana wasiwasi na baadhi wanasema hawawezi  kamwe kurudi Burundi.

Afisa huyo wa UNHCR amesema, mchakato wa wakimbizi hao kurejea nyumbani kwa hiari haukuanza leo wala jana, bali ulianza tangu wakati huo na unafanyika kwa makubaliano maalumu baada ya tathmini kuonesha kuwa hali ya usalama nchini Burundi imetengamaa kwa wakimbizi kurejea.

Zoezi hilo la kurejea kwa hiari limekuwa likiratibiwa kupitia makubaliano ya pande tatu kati ya serikali za Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi.

Kwa mujibu wa Bi. Egeh, wanaochagua kurejea nchini kwao kwa njia ya msaada, UNHCR husaidia kusafirisha familia zao kwa usalama hadi mpakani na kutoa kifurushi cha msaada wa kurejea ili kurahisisha ujumuishwaji wao upya katika jamii wafikapo Burundi.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni, UNHCR ilitangaza kuwa, ufadhili endelevu na wa uhakika unahitajka ili kuendeleza ulinzi kwa wakimbizi wa Burundi na kusaidia urejeaji na ujumuishwaji nchini mwao wakati huu ambapo kambi zinazowahifadhi katika nchi waliko zinakabiliwa na msongamano mkubwa na uhaba wa huduma muhimu…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *