Iringa. Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo amepiga marufuku mtu yeyote kuuza au kununua ardhi ya mashamba ya mpunga yaliyopo ndani ya mradi wa umwagiliaji Mkombozi uliopo Pawaga mkoani Iringa.
Chongolo ameyasema hayo jana Februari 28, 2026 katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji Mkombozi Pawaga wenye thamani ya zaidi ya Sh52 bilioni.
Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kujenga miundombinu ya mifereji na kusambaza maji, hivyo haitaruhusu ardhi hiyo kufanywa bidhaa ya biashara kiholela.
“Mtu anayeuza au kununua ardhi ndani ya mradi huu anapoteza muda wake, ni marufuku na lengo la Serikali ni kuhakikisha wakulima wanalima kwa teknolojia bora ili kuongeza uzalishaji na kufikia uchumi bora kupitia sekta ya kilimo,” amesema Chongolo.
Katika hatua nyingine, Chongolo amesema Serikali inasisitiza marufuku hiyo kwa sababu kumekuwa na utaratibu unaotumiwa vibaya na baadhi ya viongozi wa chini kuuza ardhi kwa siri bila kufuata sheria, hivyo kuanzia sasa uhamishaji wa umiliki utafuata utaratibu maalumu kupitia mamlaka za umwagiliaji ili kuzuia mianya ya rushwa na migogoro.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa amesema mifugo haitaruhusiwa kuingizwa ndani ya eneo la mradi kwa kuwa imekuwa chanzo cha uharibifu wa mifereji na kingo zake.
“Mifugo ikiingia ndani ya skimu inaharibu miundombinu tuliyoijenga kwa gharama kubwa, hivyo katazo hili ni kwa ajili ya matumizi endelevu ya mradi,” amesema Mndolwa.
Waziri wa kilimo, Daniel Chongolo (wa kwanza kutoka kulia), Mkurugenzi wa Umwagiliaji nchini, (NIRC), Raymond Mndolwa, (wa kwanza kutokea kushoto) na Viongozi wengineo wakipokea taarifa ya mradi wa umwagiliaji Mkombozi, uliopo Pawaga kutoka kwa Meneja wa NIRC, Peter Akonaay (wa katikati). Picha na Christina Thobias
Taarifa ya mradi
Meneja wa Umwagiliaji (NIRC), Mkoa wa Iringa, Peter Akonaay amesema mradi huo unahusisha jumla ya vijiji sita kati ya vijiji 15 vya Tarafa ya Pawaga, na ujenzi wa skimu hiyo umegawanyika katika mikataba minne inayotekelezwa na makandarasi Comfix and Engineering Ltd kwa mikataba ya LOT I na LOT II pamoja na CRJE East Africa Ltd kwa LOT III na LOT IV, ambapo jumla ya Sh56 bilioni zinatarajiwa kutumika kukamilisha miundombinu yote.
Akonaay amesema lengo kuu la mradi ni kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika kwa matumizi bora ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wenye tija na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Muonekano wa sehemu ya mradi wa umwagiliaji Mkombozi Pawaga. Picha na Christina Thobias
Amesema kukamilika kwa skimu hiyo kunatarajiwa kuongeza eneo lenye miundombinu ya umwagiliaji kutoka ekari 4,500 zinazotegemea mifumo ya asili hadi kufikia ekari 15,000 zenye miundombinu bora na ya kudumu.
Aidha, amesema mradi umekumbwa na changamoto kadhaa, ikiwemo uelewa mdogo wa matumizi sahihi ya miundombinu kwa baadhi ya wakulima, hali inayokadiriwa kufikia asilimia 73 na elimu imeendelea kutolewa ili kuhakikisha wakulima wanafahamu wajibu wao wa kulinda na kutumia vizuri miundombinu hiyo.
Aidha amesema maji ya mafuriko yamekuwa yakiharibu sehemu ya miundombinu huku shughuli za kilimo zisizoendana na kanuni za umwagiliaji zikiathiri mtiririko wa maji na baadhi ya wafugaji ambao pia ni wakulima, wamekuwa wakiingiza mifugo katika maeneo ya mradi na kusababisha uharibifu wa mifereji na kingo zake.
Baadhi ya wakulima wa Pawaga ambao hulima katika mradi wa umwagiliaji Mkombozi, wakiwa katika mkutano uliofanyika Pawaga wakiwasikiliza viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa kilimo nchini, Daniel Chongolo na Mkurugenzi wa Umwagiliaji nchini (NIRC), Raymond Mndolwa. picha na Christina Thobias
Walichokisema wananchi
Baadhi ya wakulima kutoka Pawaga wamesema katazo la kuuza na kununua ardhi ndani ya mradi wa umwagiliaji linaweza kuwa mkombozi wao endapo litasimamiwa kwa haki na uwazi, wakiamini litapunguza migogoro iliyodumu kwa muda mrefu.
Fatuma Filangi, mwanakijiji wa Pawaga amesema kwa muda mrefu kumekuwa na sintofahamu ya umiliki wa mashamba, jambo lililosababisha hofu na taharuki miongoni mwa wananchi, huku baadhi wakihofia kupoteza maeneo yao.
Sinzo Masanja, mkulima mwenye shamba la takribani ekari mbili, amesema kabla ya mradi kuimarishwa alikuwa analima mtama na mazao mengineyo kwa kutegemea mvua na mafuriko ya msimu, lakini sasa shamba hilo lina mgogoro kutokana na uwepo wa manufaa ya mradi.
“Kiukweli tunaomba msaada hatuna haki kwani mashamba yetu amejimilikisha mtu kitu ambacho si cha haki,” amesema Sinzo
Ally Kivipa kutoka Kimande Pawaga naye amelalamikia changamoto ya umiliki wa ardhi, akidai kuwa baadhi ya maeneo yameuzwa kwa utata na kusababisha migogoro ya muda mrefu ambayo imeathiri uzalishaji.
Baadhi ya mashamba ya mpunga na mfereji wa mradi wa umwagiliaji Mkombozi ukiendelea kutiririsha maji kwa ajili ya shughuli za kilimo hicho. picha na Christina Thobias
Malalamiko yatua Takukuru
Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) Wilaya ya Iringa, Josephat Singano, amesema walipokea malalamiko ya mgogoro wa ardhi unaohusu takribani ekari 50.
Amesema upande unaolalamikiwa uliwasilisha mikataba ikionyesha ardhi ilinunuliwa kutoka kwa watu wanne na kutiwa saini na aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji mstaafu, hivyo uchunguzi unaendelea ili kubaini uhalali wa mikataba hiyo na kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa, Benjamin Sitta, ameiagiza Takukuru kukaa na wahusika wote pamoja na nyaraka zao ili ukweli ujulikane na ni muhimu kila upande ukaonyesha mashahidi na vielelezo vya maneno waliyouziana ili kumaliza mgogoro huo kwa haki.
Waziri Chongolo amesema pamoja na kulinda ardhi, Serikali inalenga kuwawezesha wakulima kifedha ili waweze kunufaika kikamilifu na mradi huo.
Ambapo amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa benki ya ushirika nchini kufika Pawaga kukutana na wakulima na kuwapatia elimu ya fedha pamoja na mikopo ya riba nafuu.