Vifusi baada ya shambulio la angani kuzuiwa katika geti la bandari ya Jebel Ali, Dubai.

Chanzo cha picha, Reuters

Muda wa kusoma: Dakika 3

Kwa siku mbili mfululizo, wakaazi wa mji wa Dubai walilazimika kujifungia majumbani kwao, baada ya mji huo kulengwa na makombora na ndege zisizo na rubani.

Iran imekuwa ikilenga mataifa tofauti ya ghuba baada ya kushambuliwa na Marekani na Israel.

Mashambulio ya Iran yaliharibu hoteli kadhaa za kifahari, na uwanja mkubwa wa ndege wa Dubai.

BBC ilizungumza na raia wa falme za kiarabu, pamoja na watalii, wote ambao walielezea kuwa kile ambacho kinatokea si jambo ambalo wamewahi kushuhudia.

Becky Williams, mkazi wa Dubai, anasema aliona makombora takriban 15, yakirushwa kutoka nyuma ya nyumba yake na falme za kiarabu, ili kudungua makombora ya Iran, yaliyokuwa yamelenga mji huo.

Aliongezea kuwa “sauti za kudungua makombora zingesikika angani”

Lakini alisisitiza kuwa yeye na familia yake walibaki watulivu, wakiaminia uwezo wa jeshi la UAE kulinda anga yake, na anaamini kuwa “mambo yatatulia hivi karibuni.”

Aidha Iran imeendelea kutekeleza mashambulizi yake.

Mlipuko mkubwa ulipiga hoteli ya kifahari ya Fairmont Palm kwenye Palm Jumeirah, kisiwa bandia ya kifahari huko Dubai.

Mamlaka za Dubai pia zilitangaza moto mdogo kwenye sehemu ya nje ya hoteli ya kifahari ya Burj Al Arab, uliosababishwa na vifusi vya ndege zisizo na rubani zilizodunguliwa.

Mkazi mmoja wa Dubai aliiambia BBC, “tuliyoyapitia katika saa 24 zilizopita ni sehemu ndogo tu ya yale ambayo wengine wanayapitia katika maeneo ya vita, na sasa tumepata mtazamo wa jinsi hali huwa.”

Kwa Satya Jagannatha, mipango yake ya kufanya matembezi mwishoni mwa wiki ilivurugika siku ya Jumapili baada ya matukio hayo.

Aliongezea kuwa, “hapa tulipo sasa, tunabakia tu ndani ya nyumba zetu.”

Satya, mwenye umri wa miaka 35, aliongeza kuwa dada yake alikuja katika nyumba yake pamoja na familia yake na wanyama wao wa kufugwa, kwa hofu kwamba wangeweza kulengwa kwa sababu anaishi karibu na bandari ya Jebel Ali, ambako kiasi kikubwa cha vifusi vilianguka huko.

Satya alieleza kuwa “hali kwa sasa imetulia, ila kuna sauti ya milipuko ambayo husikika mara kwa mara, ila hali ya hewa huku ni tofauti, si dubai ambayo tumeizoea”

Moshi unaonekana baada ya shambulio la Iran.

Chanzo cha picha, Muskaan Kataria

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dubai umeharibiwa, mamlaka za falme za kiarabu zikitaja kuwa “tukio.”

Maelfu ya safari za ndege kutoka mashariki ya kati zimehairishwa, huu ukiwa uvurugwaji mkubwa wa safari za ndege kuwahi kutokea tangu janga la Covid 19.

Jodie Trotter, raia wa Uingereza alitarajia kurejea mjini London siku ya Jumamosi baada ya likizo yake kumalizika, ila alipofika katika uwanja wa ndege, akafahamishwa kuwa, safari zote za ndege zimesitishwa .

Judy anasema,”Nilikutana na watu waliokuwa wamehuzunika sana baada ya mipango yao ya kusafari kusitishwa. Kulikuwa na maelfu ya watu katika uwanja wa ndege, na wengine waliniambia wamekosa kuhudhuria mazishi.”

Aliongeza kuwa abiria wengi “walikuwa wanapita tu kutoka maeneo mengine , lakini sasa wamekwama katika uwanja wa ndege.”

Judy ni mmoja wa takriban wasafiri elfu moja waliokwama katika uwanja wa ndege wa Dubai. Walipelekwa hotelini na kuonywa wasikaribie madirisha.

Lakini alielezea wasiwasi wake kuwa,”Kuna vioo vingi katika hoteli hii, na hilo linatia hofu,” akiongeza kuwa walisikia “makombora kadhaa siku nzima.”

Kate Fisher, raia mwingine wa Uingereza kutoka Buckinghamshire alituelezea kuwa yeye na familia yake wanaishi kwa uoga.

Anasema yeye na mpenzi wake walikuwa wametayarisha “vifaa vya dharura” watoto wakiwa wamelala, tangu Jumamosi jioni, na kwamba “alikuwa amelowesha nguo za kuoga na taulo” kwa maji akitarajia kuzitumia kujikinga “wakati wa kutoroka ikiwa moto utatokea usiku.”

Anaelezea kuwa siku ya Jumapili ilikuwa “siku ya ajabu”

Kate aliongezea kuwa “ni hali ya ajabu isiyo ya kawaida, kuwaona watu wote wanaokuzunguka wakijaribu kufurahia likizo yao na kuwaburudisha watoto wao, wakati sisi tunaona moshi mzito kutoka maeneo ya karibu yaliyolengwa na droni au makombora.”

Vicky Pattison, aliyewahi kushiriki katika kipindi maarufu cha ushindani wa dansi cha Uingereza, cha “Strictly Come Dancing,” alikuwa miongoni mwa wale waliolazimika kutafuta hifadhi Dubai, mji unaojulikana kwa umaarufu wake wa kuwa sehemu inayopendwa na matajiri.

Vicky alikuwa akifurahia likizo pamoja na mume wake, Ercan Ramada, lakini safari yao ya kwenda Australia ilisitishwa.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *