Katika wiki iliyopita, hali ya wasiwasi kuhusu uwezekano wa Marekani kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran iliendelea kuathiri maamuzi ya kimkakati katika eneo lote.

Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, washirika wa karibu wa Marekani ambao pia wana mahusiano na Tehran, zilisema hazingeruhusu anga zao kutumiwa kwa shambulio lolote, bila kujali linatoka wapi.

Waziri wa mambo ya nje wa Misri, Badr Abdelatty — ambaye nchi yake imeanza kurejesha mahusiano na Iran lakini bado haijafikia ngazi kamili ya kidiplomasia — alizungumza na mwenzake wa Iran Abbas Araghchi pamoja na mjumbe wa Marekani kwa Mashariki ya Kati Steve Witkoff ili “kufanya kazi kuelekea kupatikana kwa utulivu, kwa lengo la kuepusha eneo hilo kutumbukia katika mzunguko mpya wa misukosuko.”

Wakati huohuo, manowari ya kivita ya Marekani inayotumia nishati ya nyuklia, USS Abraham Lincoln, pamoja na takriban meli 10 za kivita zenye makombora ya kuongozwa, zenye uwezo wa kushambulia kutoka baharini, zilifika katika eneo hilo, kwa mujibu wa tovuti ya ufuatiliaji wa usafirishaji wa majini, MarineTraffic.

Shirika la habari la serikali ya Iran, Press TV, lilitangaza kuwa kuanzia mwanzo wa wiki hii, vikosi vya majini vya Walinzi wa Mapinduzi ya Iran vitaanza mazoezi ya kijeshi ya kutumia risasi halisi katika maji hayo hayo — Mlango wa Hormuz — unaounganisha Saudi Arabia, Iran, Iraq na Umoja wa Falme za Kiarabu na Ghuba ya Oman pamoja na Bahari ya Arabuni.

Wakati huo huo, ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa uliandika kwenye X kwamba “Iran iko tayari kwa mazungumzo yanayozingatia heshima na maslahi ya pande zote — LAKINI IKISUKUMWA, ITAJILINDA NA KUJIBU KWA NJIA AMBAYO HAIJAWAHI KUTOKEA.”

Sambamba na hilo, Ali Shamkhani, mshauri mkuu wa kiongozi wa juu wa Iran, aliandika kwenye X kwamba dhana ya “shambulio dogo” ni ndoto tu.

Alisema kuwa “hatua yoyote ya kijeshi ya Marekani — kutoka chanzo chochote na kwa kiwango chochote — itachukuliwa kama kitendo cha vita, na jibu litakuwa la haraka, kamili na lisilo na mfano, likilenga kiini cha Tel Aviv na wote wanaomuunga mkono mshambuliaji.”

Kwa mujibu wa Sanam Vakil, mkurugenzi wa mpango wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika taasisi ya utafiti ya Chatham House yenye makao yake London, maamuzi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani Donald Trump yanaonyesha kuwa nafuu ya kiuchumi na kurejeshwa kwa Iran katika jumuiya ya kimataifa bado vinawezekana, “lakini ni baada tu ya Iran kukubali vizuwizi vya kudumu na vinavyoweza kuthibitishwa kuhusu mipango yake ya nyuklia na makombora ya masafa marefu, pamoja na mabadiliko ya tabia yake ya kikanda,” aliandika katika makala ya maoni kwenye tovuti ya taasisi hiyo.

Israel bado haijaimarisha kikamilifu ulinzi wake

Mvutano kati ya Marekani na Iran umeendelea kuongezeka tangu Iran ilipoanza ukandamizaji mkali dhidi ya waandamanaji mwezi Desemba 2025.

Kulingana na takwimu za hivi karibuni za shirika la Human Rights Activists in Iran lenye makao Marekani, vifo 6,479 vimethibitishwa, vikiwemo waandamanaji 6,092 na watoto 118 (hadi Ijumaa usiku, Januari 30). Zaidi ya watu 42,450 pia wamekamatwa, shirika hilo lilisema.

Kwa mujibu wa Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei, maadui wakuu wa nchi hiyo — Marekani na Israel — ndio wanaohusika na machafuko hayo.

Kwa Israel, shambulio lolote la Marekani linaweza kusababisha Iran kulipiza kisasi kwa kushambulia ardhi yake, anaeleza Pauline Raabe, mtaalamu wa sayansi ya siasa katika taasisi ya Middle East Minds yenye makao yake mjini Berlin. “Kwa kuzingatia uchaguzi ujao nchini Israel, serikali ya Israel inaunga mkono wito wa sasa wa kujizuia,” aliiambia DW.

Baada ya shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023, vita vya miaka miwili huko Gaza, na vita vya siku 12 mwezi Juni 2025 kati ya Israel na Iran — ambavyo vilishuhudia Marekani ikishambulia vituo vya nyuklia ndani ya Iran — Israel bado haijaweza kujenga upya kikamilifu mifumo yake ya ulinzi, Raabe aliongeza.

Mairav Zonszein, mchambuzi mkuu wa masuala ya Israel katika Shirika la ufuatiliaji wa Migororo la International Crisis Group, anathibitisha hilo. “Makombora ya kuzuia mashambulizi hayajajazwa kwa kiwango cha kutosha,” Zonszein alisema.

Hata hivyo, haamini kuwa Israel inaweza kumwambia Trump asichukue hatua dhidi ya Iran. “Lakini kuna sababu kadhaa zinazonifanya nione kuwa kwa sasa shambulio kama hilo halitakuwa bora kwa Israel,” aliliambia DW.

Kwa miaka mingi, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa akionya kuhusu tishio la silaha za nyuklia za Iran.

“Lakini maafisa wa Israel wangeridhika na makubaliano yanayofanana na mfano wa Libya,” ambayo yalihusisha Libya kuachana na mpango wake wa nyuklia, Zonszein alisema. Pia, kwa maoni yake, si siri kuwa Israel inaunga mkono mabadiliko ya utawala Tehran. “Japokuwa kwa sasa, Israel inahakikisha tu kuwa iko tayari kwa chochote ambacho Trump ataamua,” alisema.

Wasiwasi unaoongezeka katika mataifa ya Ghuba

Mkakati wa kisiasa wa majirani wengine wa kikanda katika kanda ya Ghuba unaendeshwa na maslahi tofauti, Eckart Woertz, mkurugenzi wa Taasisi ya Ujerumani ya Masuala ya Kimataifa na Usalama (GIGA) mjini Hamburg, aliiambia DW mapema mwezi huu.

“Mataifa ya Ghuba yana maslahi makubwa ya kudumisha utulivu wa kikanda, hata kwa kutumia mifumo ya kiimla,” alisema, akiongeza kuwa wasomi wa kisiasa wa mataifa hayo wanaonekana kupendelea kuendelea na tawala walizozoea badala ya kujihusisha na makundi mapya yasiyojulikana.

Pauline Raabe, kwa upande wake, anaamini kuwa mataifa ya Ghuba yataendelea kuweka shinikizo kubwa la kidiplomasia kwa pande zote mbili, kwa hofu kuwa ghasia zinaweza kuongezeka na kutoka nje ya udhibiti iwapo shambulio litatokea.

“Hii inaweza kumaanisha kuwa wao wenyewe wanaweza kuwa walengwa wa mashambulizi ya Iran,” Raabe alisema, akibainisha kuwa kambi za kijeshi za Marekani nchini Qatar, Saudi Arabia na Bahrain zinaweza kuwa miongoni mwa malengo ya kwanza ya mashambulizi ya anga ya Iran. “Hili linayatia wasiwasi mataifa ya Ghuba kwa sababu lingewaletea vita nyumbani kwao wenyewe.”

Tishio la nyuklia linaongezeka

Wasiwasi huu wote wa kikanda unachochewa zaidi na ukweli kwamba mazungumzo kuhusu makubaliano mapya ya nyuklia kati ya Washington na Tehran yamekwama.

Siku ya Jumatano, Rais wa Marekani Donald Trump aliandika kwenye jukwaa lake la Truth Social kwamba anatarajia Iran “kuja mezani haraka” kujadiliana kuhusu “makubaliano ya haki na ya usawa — BILA SILAHA ZA NYUKLIA — yanayofaa kwa pande zote,” akiongeza kuwa “muda unaisha, na suala hili ni la dharura sana.” Hadi sasa, bado haijulikani makubaliano kama hayo yangekuwa na vipengele gani.

Hoja za awali za mazungumzo zilijumuisha kuizuia Iran kurutubisha urani kwa kujitegemea na kupunguza uzalishaji wa makombora ya masafa marefu ya balistiki.

Wasiwasi ni kwamba makombora hayo yanaweza kutolewa kwa makundi ya silaha yanayoungwa mkono na Iran, ambayo yanatajwa kwa upana kama mashirika ya kigaidi, nchini Iraq, Lebanon, Yemen na Gaza.

Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa kiraia. Hata hivyo, viwango vya urutubishaji vinaashiria vinginevyo, kulingana na ripoti kadhaa rasmi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *